29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

AJALI NYINGINE YAUA WATANO MBEYA

 

Na PENDO FUNDISHA-MBEYA

JINAMIZI la ajali limeendelea kulikumba Jiji la Mbeya na katika kipindi cha wiki moja, watu 25 wamepoteza maisha katika ajali mbili tofauti.

Ajali ya kwanza ilitokea Julai mosi, mwaka huu katika eneo la mteremko wa Mlima Mbalizi iliyotokana na magari manne kugongana na kusababisha vifo vya watu 20 na kujeruhi 45 na nyingine ilitokea juzi katika mteremko wa Mlima Igawilo na kusababisha vifo vya watu watano na kujeruhi mmoja.

Akithibitisha kutokea kwa ajali ya pili, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mussa Taibu, alisema ajali hiyo ilitokea saa tatu za usiku juzi katika eneo la Igawilo na kuhusisha magari manne ambayo ni lori la Kampuni ya Coca Cola, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Transit goods na gari ndogo aina ya Noah.

Alisema katika ajali hiyo watu watano akiwamo Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mbeya, Izack  Nchembi, wamepoteza maisha papo hapo na mmoja kujeruhiwa na chanzo cha ajali hiyo ni kufeli kwa breki ya lori lililokuwa likitokea Mpaka wa Kasumulu.

“Watatu walikuwa katika lori lililobeba sukari ambao mmoja ni mtumishi wa TRA, dereva na utingo, wengine wawili walikuwa katika Noah,” alisema.

Akizungumzia ajali hiyo, Meneja wa TRA Mkoa wa Mbeya, Charles Bajungu, alisema lori hilo lilikuwa limebeba sukari iliyokuwa ikisafirishwa kwenda Rwanda na Izack alikuwa akilisindikiza kwa ajili ya ulinzi na usalama wa bidhaa hiyo.

“Bidhaa muhimu kama sukari inaposafirishwa kwenda nchi jirani ni lazima iwekewe ulinzi hadi pale inapopokelewa hivyo safari ya lori hili ilikuwa ikiishia katika Mpaka wa Rwanda na Tanzania, lakini ndiyo hivyo imeishia hapa na kupoteza uhai wa mtumishi mwenzetu, dereva na utingo,” alisema.

Alisema mwili wa Nchembi unatarajiwa kusafirishwa nyumbani kwao Tabora leo wa ajili ya maziko na alikuwa ni mwajiriwa mpya wa TRA.

Kutokea mfululizo kwa matukio hayo ya ajali, kumezua hofu kwa baadhi ya wakazi wa Mbeya na wengi wamehoji iweje mazingira yake yafanane.

“Ukiangalia ajali ya Mbalizi, chanzo tunaambiwa ni breki, ajali imehusisha gari nne, gari ndogo moja ilifunikwa na kontena na hii ya leo (juzi) tunaambiwa ni kufeli kwa breki, gari nne na moja ndogo imefunikwa na kontena, hapa wananchi tunapatwa na hofu,” alisema Ismail Mwambapa, ambaye ni mkazi wa Uyole

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles