Na AVELINE KITOMARY
DAKTARI bingwa wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Patience Njenje amesema ajali imekuwa ikichangia asilimia 10 ya ugonjwa wa kifafa, huku vijana wakiathirika zaidi.
Dk. Njenje alisema katika mahojiano maalumu na MTANZANIA Jumapili ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kifafa Duniani Februari 10 kila mwaka ambapo kwa mwaka huu kaulimbiu ikiwa ni ‘je, unafahamu dalili za kifafa?’.
“Ajali imekuwa sababu kubwa ya kifafa kwa Tanzania, kati ya hao wenye kifafa vijana wameathirika zaidi – wastani wa miaka 15 ukilinganisha na wazee, ukipata ajali inaweza ikasababisha kuumia ubongo, au damu kuvujia kwenye ubongo, kovu kwenye ubongo na hata ubongo kutikisika.
“Kwahiyo kwa bahati mbaya wengi wakipata ajali wanaangalia kwa nje kuwa amevuja damu wapi, kuna wakati unaweza kupata ajali usione damu, lakini ukapoteza fahamu, hii ndio dalili kuwa umeumia kwenye ubongo, baada ya hata miaka 10 mtu anaanza kuanguka, fikra ya kwanza ni imani potofu, lakini kumbe akija hospitali tunamuhoji ili tujue historia yake,” alieleza Dk. Njenje.
Kwa mujibu wa Dk. Njenje, utafiti uliofanyika hapa nchini unaonyesha katika kila watu 1,000 watu 37 wana tatizo la kifafa, huku zaidi ya watu milioni 60 wakikumbwa na tatizo hilo duniani.
“Kwa kila mwaka kuna ongezeko la watu 70 kati ya watu 100,000 duniani kote, hivyo kidunia ugonjwa huu una kasi kubwa, hasa kwa upande wa Afrika ugonjwa huu uko mbele mno ambapo katika kila watu 1,000 watu 50 wameathirika na kifafa, asilimia kubwa wanatoka Afrika.
“Tafiti zilizofanyika kama ule wa Mahenge, Morogoro wa ugonjwa wa kifafa kwa Afrika, Tanzania inaongoza kwahiyo hili ni tatizo kubwa, wagonjwa wana hatari ya kufa mara sita zaidi ya mtu ambaye hana kifafa,” alibainisha Dk. Njenje.
Alisema asilimia 36 ya jamii wana imani potofu kuhusu ugonjwa huo, hali hiyo imesababisha wagonjwa wengi kutokufika hospitali kwa wakati au kabisa.
“Kwa sababu hiyo tunafanya tukio hili kufahamisha jamii kuondokana na imani potofu kama kulogwa au kutupiwa majini, hii itasaidia watu kwenda hospitali kupata matibabu kwani ni ugonjwa unaotibika na dawa zipo,” alisema Dk. Njenje.
Aidha alieleza kuwa kifafa ni ugonjwa ambao sio wa kuambukizwa na unaanza baada ya ubongo kupata hitilafu, hivyo njia ya kushughulikia imekuwa ndogo, wameamua kuongeza nguvu zaidi kuhusu ugonjwa huo ili kuelimisha jamii.
“Ubongo unaendesha kila kitu katika mwili wa binadamu na umegawanyika katika sehemu mbili, upande wa kulia na kushoto. Upande wa kulia una uwezo wa kutoa amri kwa upande wa mwili wa kushoto, kwa mfano kutoa amri ya kunyanyua mkono wa kushoto au mguu.
“Kifafa ni hitilafu ya muda inayotokea ambapo ubongo unatoa amri kwamba sasa nyoosha mikono au miguu, hivi vyote inatokana na ubongo kupewa ujumbe ambao sio wa kawaida, ili tuseme hiki ni kifafa inabidi upate degedege mbili.
“Sababu ya pili kusiwe na ugonjwa ambao upo kwa wakati huo, kitu cha tatu apate degedege zaidi ya mbili inayotenganishwa na saa 24 ila kubwa zaidi ni hitilafu katika ubongo, kama watu wanapata dalili mbalimbali zinazofanana na degedege lazima mtaalamu athibitishe,” alifafanua Dk. Njenje.