Na ZAHOR A. ZAHOR
SUALA la aina gani ya kuku wanafaa kufugwa, limekuwa zito kwa watu wengi, ambapo majibu yake yamekuwa ni ya kisiasa zaidi. Wapo wanaosema tufuge kuku wa kienyeji, wapo wanaosema tufuge kuku wa kitaalamu na wengine wanasema chotara wanaofaa zaidi.
Mara nyingi tunapozungumzia kuku kwa Tanzania tunakusudia makundi ya aina tano: Kuku wa asili, nyama, mayai, nyama na mayai na chotara.
Kuku wa asili: Hawa ni wale kuku wetu ambao tumezaliwa na kuwaona katika majumba yetu toka enzi na enzi, kati yao kuna kuku wenye umbo zuri kwa ajili ya nyama na wapo ambao wanamaumbile mazuri ya kutaga mayai mengi. Kuna wakubwa na wadogo wenye rangi mchanganyiko kwa mfano; kuchi, bukini, kinyavu, nungunungu/kuchere/njachama.
Tafiti nyingi za kuku zinatokana na kuku hawa, watalamu huwaweka katika makundi maalumu ili kuwezesha kupata kuku wa nyama na mayai kwa kutumia taaluma maalumu.
Aina za kuku wa asili wanaopatikana hapa nchini ni pamaja na Kuchi (Kuza), pori (Kishingo), Njachama, Kinyavu, Mbuni na Tongwe (Msumbiji).
Kuku wa nyama: Hawa ni wale ambao mara nyingi hufugwa kwa mfumo ndani, ambao tuliwahi kuelezea katika masomo yaliyopita. Hawa ni wale ambao wamefanyia utafiti wa kitaalamu na kuchaguliwa katika mfumo maalumu ambao watakuwa wakubwa katika muda mdogo. Pia wamefanyiwa utafiti na kutumika kwa matumizi ya nyama tu kwa kuwa wanao uwezo wa kukua. Rangi za kuku hawa kuna wekundu, weupe, wanaofanana na kanga ambao wanapatikana katika makundi mawili, wakubwa na wadogo.
Mayai: Kuku hawa ni wale ambao wamefanyiwa utafiti wa kina kwa sababu hutaga mayai mengi. Mfumo wa ufugaji wa kuku hawa ni kama ule wa nyama, ni wa ndani ambao huku hupata huduma zote kutoka kwa mfugaji. Rangi za kuku hawa wamo weusi, weupe na wekundu.
Kuku wa nyama na mayai:
Kuku hawa wamefanyiwa utafiti wa kitaalamu ili kumuwezesha mfugaji wanapofika umri wa miezi miwili hadi minne, kuwa wakubwa na kuwauza kama nyama na anapowacha katika umri wa kutaga ambao mara nyingi kama matunzo mazuri ni miezi minne na nusu wawe wanatanga na kumpa mayai. Kuku hawa utagaji wake si kama wale wa mayai, mara nyingi ni nusu huria. Wanafanana na kuku wa kienyeji lakini hawatamii.
Miongoni mwao, wapo ambao utagaji na ukuaji wake ni mzuri, aina za kuku hawa ni kama Kuroiler Sasso na Rhode Island Red. Wafugaji wengi hivi sasa wanashauriwa kufuga kuku hawa kwa kuwa mfugaji anaweza kupata mayai mengi na hapo hapo akauza kuku hawa kama wa nyama kwa kumuongezea kipato.
Watu wengi huwachanganya na chotara lakini si chotara, ni aina ya kuku ambao unafuga kwa kujua kusudio lako.
Chotara:
Hivi sasa kumekuwapo aina mpya ya kuku ambao wanajulina kwa jina la Chotara, hupatikana kwa kuchanganya kati ya kuku wa kisasa na wa asili na kupata kuku wenye sifa na maumbile tofauti tofati. Mara nyingi wafugaji huwa tunachanganya bila kupata ushauri wa kitaalamu au kutumia njia bora ya kuchanganya.
Mfugaji kila wakati anashauriwa anapotaka kuchanganya kuku awe anajua nini anachotaka kukizalisha hivyo, anaweza kuongeza uzalishaji kwa kuchagua kuku mwenye sifa zifuatazo:
- Uwezo wa kutaga mayai mengi kati ya 15-200 katika mzunguko mmoja wa utagaji
- Uwezo wa kuatamia na kuangua vifaranga wengi,
- Uwezo wa kustahimili magonjwa
- Umbo kubwa na kukua haraka.
Kwanini tufuge kuku wa kienyeji?
Unapowauliza ni kwanini tufuge kuku wa kienyeji, wengi watakujibu kuwa hawapati maradhi mara kwa mara na hawana gharama kubwa za ufugaji. Lakini unapomuuliza mtu kuwa kuku wako alitotoa vifaranga 12 lakini mwisho mbona wamebakia wane, hatokuwa na jibu.
Kwa kawaida vifaranga hufa kwa maradhi ambayo wakati mwingine hutokana na kutowapa chanjo na wakati mwingine ni lishe duni.
Kweli kuku wa kitaalamu wanamatatizo?
Watu wengi wanadhani kuwa kuku wa kitalaamu wana matatizo wakati wa kuwafuga, lakini unapowauliza matatizo gani hayo, wengi wao hujibu kuwa wanahitaji gharama kubwa katika kuwatunza. Kitu ambacho si kweli kwa kuwa kila biashara inahitaji gharama. Kwa upande mwingine, wapo wafugaji si waaminifu hivyo husababisha baadhi ya watu kudhani kuwa kuku hawa hupewa dawa za binadama ili kuwa wakubwa.
Je, unaweza kufuga kuku bila gharama?
Kitu muhimu ni lazima tujue kwamba kitu chochote unachokifanya kwa biashara basi ni lazima ukifanye kitaalamu na kwa uweledi mkubwa. Kama unataka kufuga kuku lazima utimize masharti ya ufugaji bora ikiwamo kuwapa chanjo, chakula bora na dawa pindi wanapopata matatizo. Vitu vyote hivyo ni gharama.