24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Aliyetengeneza helikopta alianza na gereji inayotembea

NDEGE

Na Eliud Ngondo, Songwe

HAPA nchini kuna vipaji mbalimbali ambavyo vinatakiwa kuendelezwa ili viendelee kukua na kufahamika kwa mataifa mengine.

Tumekuwa tukisikia na kusoma katika vyombo vya habari juu ya Watanzania wenzetu wabunifu wa vitu mbalimbali wakitangazwa lakini ajabu ni kwamba wengi wamekuwa hawaendelezwi.

Adam Kinyekile ambaye ni mzaliwa wa Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa ametengeneza ndege aina ya helikopta mwenyewe bila kusaidiwa na mtu mwingine.
Kijana huyo ambaye kwa sasa anaishi katika Mji wa Tunduma, mkoani Songwe ni miongoni mwa Watanzania ambao wanaingia kwenye historia ya kutengeneza ndege aina ya helikopta.

Kinyekile anasema alianza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Mkubo iliyopo wilayani Mufindi mkoani Iringa na baada ya kuhitimu hakuweza kuchaguliwa na elimu ya juu hivvyo akaamua kuanza kujifunza ufundi wa magari.

Anasema kutokana na familia yake kutokuwa na uwezo alikwenda kwenye gereji ya mtu binafsi aitwaye Vicent Mng’ong’o ili kuweza kujifunza ufundi huo.

Anasema alijifunza katika gereji hiyo kuanzia mwaka 1998 hadi 1999 alipojiona kuwa amefuzu.

“Ilipofika mwaka 1999 mwenye gereji alinieleza kuwa nina uwezo wa kutengeneza magari hata nikiwa peke yangu ndipo mwaka 2000 nikaamua kufungua ya kwangu,” anasema Kinyekile.

Anasema baada ya mwaka mmoja alihama kutoka Mafinga na kuja katika Mji wa Tunduma ambapo alikutana na wazungu na kuanza kufanya nao kazi ya kusafirisha magari kutoka Tanzania hadi nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Anasema alifanya kazi hiyo kwa miaka mitatu na baada ya hapo aliwaomba wamruhusu arudi nyumbani kuendeleza ufundi wake.

Kijana huyo anasema mwaka 2004 baada ya kurudi Tunduma alifungua gereji na kuendeleza shughuli zake za ufundi wa magari ambao aliona ni fani inayoweza kumwinua kiuchumi.

“Niliendelea kutoa huduma hiyo kwa wateja wangu hadi mwaka 2010 ambapo aliamua kujipanua zaidi katika utoaji huduma ya utengenezaji wa magari,” anasema.

Kinyekile anasema baada ya kuona amekwisha fahamika na wateja wake aliamua kubuni njia ambayo anaweza kuwafikia kiurahisi wateja wake.

Anasema aliunda gereji inayotembea ambapo hata gari likiharibika porini alikuwa analifuata na kulitengeneza.

“Niliwaza sana na kuona kuna ulazima wa kuunda gereji inayotembea baada ya kuona kuna magari unakuta yanaharibika sehemu za mbali hivyo hata kulibeba inakuwa ni gharama kubwa,” anasema Kinyekile.

Anasema gereji hiyo inayotembea ina mfumo mzima wa gereji ambapo inakuwa ni rahisi kutengeneza gari hata likiwa
porini bila kubebwa na mteja akaendelea na shughuli zake kama za kusafirisha bidhaa.
“Gereji yangu ilikuwa iwe inatembea yenyewe lakini kutokana na mahitaji ya wateja kuwa makubwa niliamua kuikatisha na kuifanya kuwa gereji ya kuvutwa ambayo inavutwa kwa kutumia gari na kumfikia mteja popote pale ambapo gari lake limeharibika,” anasema.

HELIKOPTA

Anasema wazo la kutengeneza ndege lilidumu kwa muda wa
mwaka mmoja ambapo alikuwa akiumiza kichwa juu ya kitu kinachosababisha helikopta iruke na kushuka ikiwa salama.

“Wazo hilo lilinijia baada ya kuona nimetengeneza gereji inayotembea na kuona kuna umuhimu wa kuanza kupambanua akili kwa kubuni jambo lingine ambalo lingeweza kuwa kivutio kwangu,” anasema.

Anasema shauku hiyo ya kuona ndege ikiruka ilimtia hamasa ya kuiga na kuona kuwa ana uwezo wa kutengeneza ndege iweze kuruka kama zingine zinavyoruka.

“Nilianza kwa kuangalia ni kitu gani kinachosababisha ndege iruke na kubaini kuwa ni nguvu ya upepo ambayo ikitengenezwa itakuwa na uwezo wa kuinua ndege.

“Ndege yangu nimeitengeneza kwa vifaa vya magari vyote bila kuwepo kwa kifaa chochote cha ndege za nyuma ambazo zimewahi kuharibika,” anasema.

Anasema injini anayotumia ni ya gari aina ya Ipson 3S ambayo inaweza kuruka umbali wa kilomita 1000 bila wasiwasi na kuifanya kuwa na uwezo mkubwa wa kuenda sehemu yoyote ya hapa nchini.

Kijana huyo anasema injini hiyo inatumia lita 70 za mafuta na hata kwenye gari uwezo wake ni kuweza kutembea umbali wa kilomita 1000 bila kuzimwa.

Anasema injini hiyo ina kazi ya kuzungusha mapanga yote mawili ya mbele na nyuma.

“Nimeweka injini katika eneo ambalo abiria akikaa atakuwa anakanyaga miguu yake na haiwezi kuleta madhara yoyote kwa ndege wala abiria,” anasema.

Anasema injini yenye uwezo wa kuunda upepo mkubwa inampa uhakika wa ndege kuruka bila kupata matatizo yoyote na kwamba ndege hiyo inatumia mafuta aina ya Petroli huku mfumo mzima ukitumia mfumo wa gari.

Kijana huyo anasema ndege hiyo imeundwa na kila kitu kutoka kwenye gari hivyo inakuwa ni rahisi kuweza kufanikisha ndoto ambayo imekuwa ikimtesa kwa muda mrefu kuona inaelekea kukamilika.

Adam anasema helikopta hiyo inaonekana ni tofauti na watu wanavyozifahamu hususa zile za kijeshi ambazo zimekuwa zikionyeshwa kwenye picha pia hata zile ambazo zimetengenezwa na wazungu.

Mgunduzi huyo anasema katika utengenezaji alikuwa akisumbuka sana na jinsi ndege hiyo inavyoweza kutengeneza nguvu ya upepo wa kuisababisha iweze kuruka na kutua bila kuwepo na matatizo yoyote.

Anasema aliwaomba wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (MUST) wamtembelee na kuiona ndege hiyo kisha kumshauri juu ya mambo kadhaa ambayo yanasababisha ndege iweze kuruka na kutua bila wasiwasi.

Kinyekile anasema wataalamu hao walimshauri kutengeneza mfumo mzima wa kuipasha joto ndege na kuipoza hali ambayo itafanya iweze kuruka angani na kutua bila kikwazo chochote.

Licha ya kutengeneza helikopta kijana huyo pia ana wazo la mashine ya kutengeneza vijiti vya kuchokonolea meno (Toothpick).
“Haiwezekani Watanzania tukawa tunanunua vijiti vinavyotengenezwa nchi zingine wakati malighafi tunazo,” anasema.

CHANGAMOTO

 Changamota anazokutana nazo kijana huyo ni kukatishwa tamaa na baadhi ya watu.

Anasema changamoto nyingine ni juu ya kupata fedha kwani angeweza kutengeneza ndege hiyo kwa kuchanganya na baadhi ya vifaa ambavyo ni muhimu vya ndege.

MUST

Mwalimu kutoka Chuo cha Sayansi na Teknolojia (MUST), Lukas Sikudhan, anasema ubunifu wa kijana huyo unaweza kufanikisha ndege hiyo kuweza kuruka bila kuwepo kwa tatizo lolote.

Anasema walipomtembelea walikuta kuna tatizo la kitaalamu ambapo kama ndege hiyo ingeruka juu ingeshindwa kutua hali ambayo ilikuwa ni hatari kwa watumiaji.

“Ndege hiyo ingeweza kuruka lakini ingeshindwa kutua kwa sababu kuna baadhi ya mambo ambayo yalitakiwa kuwepo yalikuwa yamekoseka,” anasema.

Anaeleza kuwa ili ndege iweze kuruka na kutua ni lazima kuwepo kwa mfumo wa Mean Rotter na Tone Rotter ambazo zinaifanya ndege ikiruka iweze kuwa na wastani wa kushuka na kupaa bila tatizo.

“Maen Rotter inasaidia ndege kutengeneza mfumo wa kuweza kukata kona, kuinuka na kuweza kuruka kisha kupaa lakini unapoanza kubadilisha gia inakuwa ni vigumu kutokana na kuzunguka kama Pia.

“Tone Rotter inaisaidia ndege kutokuzunguka kama Pia, lakini hiki kifaa kinasaidia ndege kuwa na uwiano (balance) zaidi na kuifanya iweze kuruka bila kuleta madhara,” anasema Mwalimu Sikudhan.

Mwalimu huyo anasema ndege hiyo kwa mbele imechongoka hali ambayo mgunduzi huyo alizingatia sana kutokana na kuwa ikichongoka hivyo inaifanya ndege iweze kukata mawimbi kwa urahisi zaidi.

Pia anasema ndege yenye mapanga matatu hadi manne inawezesha ndege kuruka kwa urahisi ambapo Mean Rotter yake inakuwa na uwezo mzuri wa kuisaidia kuruka angani.

Anaeleza kuwa ndege kama iliyotengenezwa na Adam yenye mapanga mawili inaweza kuruka mara baada ya speed ya ndege hiyo kuwa kubwa, lakini ikitumia mapanga manne inaweza kufaulu kuruka hata speed ikiwa ni kidogo.

“Kawaida ili ndege iweze kuruka inatakiwa nyuzi ianzie 0 hadi 16 hapo ndege inaweza kuanza kuinuka na kuweza kupaa angani bila kuwepo kwa wasiwasi na ikatua salama,” anaeleza mtaalamu huyo.

“Ndege ikiwa kwenye nyuzi 16 nguvu ya upepo wa chini inakuwa ni kubwa zaidi hali inayoisaidia ndege iweze kuruka bila tatizo,” anasema.

Anasema changamoto kwa kijana huyo ni juu ya kutambua uzito wa ndege hiyo kutokana na kutumia vyuma mbalimbali ambavyo inakuwa ni vigumu kuweza kutambua kuwa ndege hiyo ina uzito gani.

Lucas anasema serikali inatakiwa kumsaidia kijana huyo kwa kumwezesha kifedha ili aweze kununua vitu ambavyo ni dira mara baada ya ndege kuruka angani.

Mwalimu huyo anasema nchi ya Tanzania bado ni changa hivyo serikali inatakiwa kuwawezesha wagunduzi ambao wamekuwa wakionyesha vipaji vyao, na kushauri Watanzania kuacha tabia ya kuwakatisha tamaa watu wanaogundua vitu mbalimbali.

“Adam akiwezeshwa anaweza kufanikisha zaidi utengenezaji wa ndege hiyo ikawa bora kuliko watu wanavyodhani kuwa haitaweza kuruka na kupaa again,” anasema.

Naye Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Songwe, Victory Carlson, anesema tangazo lililotolewa hivi karibuni na Mamlaka ya Usafiri wa Anga halilengi kuwazuia wabunifu wa ndege kutobuni bali wanatakiwa kufuata na kuzingatia vigezo vilivyowekwa.

Kuhusu ubunifu uliofanywa na kijana huyo, anasema anatakiwa awepo mshauri kwa ajili ya kuangalia ndege hiyo ilivyoundwa na inavyoendelea kutengenezwa.

Carlson anasema katika ndege kuna vitu mbalimbali ambavyo vinazingatiwa na kwamba kitu cha kwanza ni lazima kuwepo kwa mawasiliano kati ya rubani na watu wa chini ambao wanaongoza ndege wakiwa uwanjani.

“Dira ni kitu muhimu sana katika ndege pamoja na redio ya mawasiliano ambayo itakusaidia wakati wa kuruka ili ndege isije ikogongana na ndege nyingine ambayo inapita katika njia hiyo hiyo,” anasema Carlson.

Anasema kama wakijiridhisha kuwa ndege hiyo inaweza kuruka basi wanaweza kumruhusu ili aweze kuendelea na utoaji wa huduma.

“Katika ndege iliyotengenezwa na Kinyekile kuna vitu vichache ambavyo vinatakiwa kurekebishwa na kuifanya iwe katika uimara ambao unatakiwa na kuendelea kutoa huduma,” anasema Carlson.

 0757670059, 0782338802, 0652664939.

[email protected] / [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles