Nora Damian na Esther Mnyika, Monduli
Waziri Mkuu wa zamani, Hayati Edward Lowassa ametajwa kuwa aliunganisha uchumi wa mikutano na utalii hatua iliyochangia kuongezeka kwa mapato katika sekta hiyo.
Lowassa alifanya kazi kama Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) miaka 35 iliyopita.
Akizungumza leo Februari 16,2024 wakati wa kutoa salamu baada ya ibada iliyofanyika nyumbani kwake Kijiji cha Ngarash wilayani Monduli Mkoa wa Arusha, Mtendaji Mkuu wa AICC, Lawrence Mafuru, amesema alifanya mambo mengi katika uongozi wake ambayo wanaendelea kuyakumbuka hadi sasa.
“Aliunganisha uchumi wa mikutano na utalii ili wageni wanaokuja katika mikutano waweze kutembelea vivutio mbalimbali ili uchumi wa sekta ya utalii uongezeke.
“Wafanyakazi wengi walipata nafasi kwenda kusomea utalii wa mikutano na kabla simu janja hazijaja alihakikisha wakurugenzi wote wanakuwa na ‘redio call’ ili akitaka kujua chochote aweze kukipata kirahisi,” amesema Mafuru.
Amesema pia alianzisha kampeni ya kutunza mazingira kwa kupanda miti na kuahidi kuyaenzi yote aliyofanya ili kukuza uchumi wa utalii na mikutano.
Naye Waziri Mkuu mstaafu, Mizego Pinda, amesema Lowassa ni mwalimu wake kwa sababu alipenda kufanya kazi na alikuwa hana utani.
“Nilifanya kazi chini yake nikiwa Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa, nilijifunza mengi, yapo mengine mengi pengine mnaponiona leo ni kwa sababu nimejifunza kutoka kwake.
“Ilikuwa ukimwambia pole kwa kazi nyingi anasema tupeana hongera kwa sababu tumetimiza kile ambacho tulitaka kifanyike na katika hilo hana utani,” amesema Pinda.
Kwa upande Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenister Mhagama, amesema Lowassa ameacha alama akiwa mtumishi na mtendaji ndani ya Serikali.
“Tutaendelea kutambua yale yote aliyoyafanya katika uhai wake akiwa mtumishi na mtendaji ndani ya Serikali, kila mtu ajifunze kutokana na mifano ya yale mema aliyoyafanya,” amesema Mhagama.
Katika ibada fupi iliyoongozwa na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk. Godson Mollel, amesema watamkumbuka Lowassa kwa mchango mkubwa alioutoa wa maendeleo na ustawi wa kanisa hilo.
“Maisha ya kiroho ya mheshimiwa Lowassa hayatiliwi mashaka, alikuwa mshirika mwaminifu, hakuna dhehebu lolote ambalo hajaweka nguvu katika suala la maendeleo na ustawi.
“Alipenda nyimbo tatu na mmoja naona mmeuandika kwenye bango, kwa heshima naomba tuuimbe wimbo namba 180 (Bwana u sehemu yangu kutoka katika kitabu cha Tumwabudu Mungu Wetu),” amesema Askofu Mollel.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na wananchi, viongozi wa kisiasa na kimila ambao walipata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho.
Lowassa alifariki Februari 10,2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa akipatiwa matibabu na anatarajiwa kuzikwa Februari 17,2024 nyumbani kwake Ngarash, Monduli mkoani Arusha.