Na PENDO FUNDISHA – MBEYA
JESHI la Polisi limefanikiwa kumtia nguvuni Happy Charles (24), kwa tuhuma za wizi wa mtoto mchanga katika wodi ya watoto ya Hospitali ya Mkoa wa Mbeya.
Imeelezwa kuwa mama huyo alifikia uamuzi huo baada ya kuishi miaka miwili ya ndoa bila kupata mtoto.
Akielezea tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga, alisema Happy anadaiwa kutenda kosa hilo Februari 1, saa nne za usiku katika wodi ya watoto ya Hospitali ya Mkoa wa Mbeya.
Alidai kuwa Happy ambaye ni mkazi wa eneo la Uwanja wa Ndege, kabla ya kufanikiwa kuiba kichanga hicho, alifika Hospitali ya Wazazi ya Meta akiwa ameongozana na mume wake, Chiluba Peter, akidai kwamba ni mjamzito na uchungu umemshika, hivyo anahitaji huduma ya kuzaa.
“Akiwa hospitalini hapo, inasemekana mtuhumiwa alimtaka mume wake aende nyumbani kumwandalia chai na ndipo yeye alipopata nafasi ya kuchukua pikipiki hadi Hospitali ya Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kuingia kwenye wodi ya watoto na kuondoka na kichanga hicho cha kike,” alisema Kamanda Mpinga.
Kwa mujibu wa Kamanda Mpinga, imeelezwa kwamba mtuhumiwa huyo akiwa amevalia mavazi ya kawaida, alifanikiwa kuondoka na kichanga hicho na kuelekea nyumbani kwa mama yake mzazi anayeishi Kata ya Uyole jijini hapa.
Alisema kuwa uchunguzi zaidi unafanyika na utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani, lakini Kamanda Mpinga, amewahasa wanawake au wazazi kutotumia njia za haraka na rahisi kutafuta dawa ya matatizo yao.
Aidha, akizungumzia tukio hilo, mama wa kichanga hicho, Sarah Mwasanga (35), alisema kuwa alifanikiwa kujifungua mtoto wa kike Februari 1, usiku katika Hospitali ya Mkoa wa Mbeya.
Alisema akiwa katika wodi hiyo na wanawake wengine ambao baadhi walikuwa tayari wamejifungua na wengine wakisubiri kuingia leba, alitokea mwanamke huyo akiwa amevaa nguo za kawaida na kuwaeleza kwamba wanatakiwa kupeleka watoto kupata chanjo.
“Hongereni sana wanawake wenzangu, Mungu amewasaidia kupata mtoto, lakini leo ni siku ya chanjo, hivyo mnatakiwa kupeleka watoto wenu kupata huduma hii, lakini kabla ya kwenda subirini nikaangalie kama ofisi ipo wazi,” Sarah alinukuu maneno yaliyosemwa na mtuhumiwa akiwaeleza wanawake wote waliokuwa ndani ya wodi hiyo.
Sarah, alisema baada ya hapo mwanamke huyo alifika na kumchukua mtoto wake na kuondoka naye, lakini cha ajabu aliona muda unaenda na mtoto wake ajarejeshwa, ndipo alipopata akili ya kwenda kuulizia kwa manesi waliokuwa zamu siku hiyo.
“Wakati nawaelezea manesi, niliona wakinishangaa na kunihoji ni chanjo gani inatolewa usiku, ndipo walipobaini kwamba mtoto wangu atakuwa ameibwa, hivyo kutoa taarifa polisi na hatimaye kupatikana,” alisema Sarah.
MTANZANIA lilifanikiwa kuzungumza na baadhi ya majirani wa eneo alilokuwa akiishi mtuhumiwa, ambao wameeleza kwamba mazingira magumu ya ndoa ya binti huyo ndiyo yaliyomsababishia kufanya uamuzi wa kuiba mtoto.
“Unajua binti huyu aliolewa mwaka 2015, lakini inasemekana kila akishika ujauzito unatoka, na ndugu nao wameshikilia bango, hivyo nahisi alikosa washauri wazuri na hatimaye kutenda kosa hilo ambalo kwa sasa analijutia,” alisema Yohana Mwinuka mkazi wa eneo la Uwanja wa Ndege.