25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

AHADI TANO ZA RAIS WEAH KWA WALIBERIA MONROVIA, LIBERIA

 

RAIS mpya wa Liberia, George Weah amewaahidi wananchi wa taifa hilo kuwa katika kipindi cha utawala wake atakabiliana na changamoto tano za kiuchumi na kijamii.

Rais Weah ambaye ni nyota wa zamani wa kimataifa wa soka wa Liberia, alitoa ahadi hizo juzi alipokuwa akiapishwa kushika madaraka katika tukio la kwanza la kubadilishana  madaraka kidemokrasia baada ya miaka 70.

Ahadi za Rais Weah ni kupambana na rushwa, kusaidia sekta binafsi, kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana, uwazi na kuheshimu haki na demokrasia.

Taarifa kutoka nchini humo zilieleza kuwa kushindwa kukabiliana rushwa na ufisadi miongoni mwa maofisa wa umma ni moja ya mambo ambayo mtangulizi wake, Ellen Johnson Sirleaf alaumiwa kwa kushindwa kuyavalia njuga.

Katika hotuba yake baada ya kuapishwa, Rais Weah alisema wapiga kura wamempa kazi ya kung’oa mizizi ya ufisadi.

“Naamini jukumu kubwa nililopewa na watu wa Liberia ni kukomesha rushwa katika utumishi wa umma. Naahidi kulishughulikia vema jukumu hili.

“Kwa maofisa wa serikali wakati umefika kuweka mbele maslahi ya watu wetu kabla ya maslahi yenu binafsi. Ni wakati wa kuwa wawazi kwa watu wetu. Ijapokuwa rushwa ni tabia iliyozoeleka miongoni mwa watu wetu, lazima tuikomeshe,” alisema Rais Weah.

Akizungumzia sekta binafsi, alisema ataondoa vikwazo visivyo vya lazima vya kibiashara ili kulikwamua taifa kutoka mkiani katika orodha ya kimataifa ya mazingira ya kibiashara licha ya uwapo wa utajiri wa maliasili.

“Kwa sekta binafsi, nawaambia, Liberia iko wazi kwa ajili yenu Tutafanya kila linalowezekana ndani ya uwezo wetu kutoa mazingira ambayo yatakuwa rafiki kuendesha biashara kwa uwazi na uaminifu,” alisema.

Hata hivyo, alisema kamwe hapendi kuona Waliberia wakiwa ‘watazamaji’ katika uchumi wao wakati wahamiaji wa India na Lebanon wakitawala biashara za rejareja na huduma huku kampuni za Magharibi zikimiliki sehemu kubwa ya shughuli za uvunaji mpira, mafuta ya alizeti na madini ya chuma.

Kuhusu ajira kwa vijana, Rais Weah alisema anaamini mafunzo ya ufundi stadi ni jibu kwa kizazi kilichokosa elimu rasmi wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe ya 1989-2003.

“Tunahitaji walimu waliofuzu zaidi si tu katika taasisi zetu za ufundi stadi bali pia kwa shule na vyuo vyetu vikuu.

“Taasisi za ufundi stadi ni njia nzuri ya kuwezesha vijana wakubwa kuingia katika soko la ajira haraka kwa vile wengi wao tayari wako katika majukumu ya kifamilia,” alisema Rais Weah.

Aidha, aliahidi kutenga fungu la kutosha katika bajeti ijayo ya taifa hilo kwa ajili ya shule na vyuo vya ufundi stadi.

Kuhusu uwazi, Rais Weah alisema uhuru wa kutoa maoni uliimarika wakati wa utawala wa Sirleaf na yeye afungua milango zaidi katika uendeshaji wa serikali.

Alisema moja ya mambo yaliyolalamikiwa wakati wa utawala uliopita ni uwapo wa usiri katika masuala ya matumizi ya ardhi ya umma na hivyo kusababisha migogoro ya mara kwa mara baina ya watu na kampuni binafsi nchini Liberia.

“Kwa pamoja, tunawaahidi raia wetu kuwa wazi katika masuala muhimu kama manufaa ya ardhi zilizopo maeneo yenu, uhuru wa kutoa maoni na namna ya kufaidika na maliasili za taifa,” alisema.

Weah aliwakumbuka mamia kwa maelfu ya watu waliokufa wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe na kusema somo la gharama iliyotumika ni kubwa.

“Hii ni misingi ya haki za binadamu ambazo watu wetu wanastahili na yapaswa ipimwe dhidi ya vitendo vyetu, sera na sheria zetu,” alisema.

Pia aliutaka umma kuweka kando ukabila na ukanda na kujihesabu wote kama ‘Waliberia kwanza.’

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles