Na GUSTAPHU HAULE ,PWANII
MAMLAKA ya Usafirishaji Majini na Nchi kavu (SUMATRA) Mkoa wa Pwani pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini, wanadaiwa kupuuza agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo la kutaka wasafirishaji wa abiria kwa njia ya daladala waliopo Mlandizi kuendelea kutumia stendi yao ya zamani, badala ya ile ya mtu binafsi inayotambulika kwa jina la Mama Salmini.
Waziri Jafo,alitoa agizo hilo Machi 11, mwaka huu, wakati akizungumza na wasafirishaji wa magari ya Mbezi- Mlandizi-Bagamoyo –Chalinze mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama,viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wengine wa Serikali akiwemo mkurugenzi wa halmashauri hiyo.
Katika agizo hilo, Waziri Jafo alisema alitembelea stendi ya Mama Salmini na kujionea upungufu mkubwa, ukiwamo kupitiwa na Gridi ya Taifa na hata kuwapo miundombinu mibovu na ni hatari kwa wananchi kutumia eneo hilo kama stendi na kuagiza kutumia stendi yao ya zamani iliyopo kando kando ya barabara ya Morogoro.
“Nimetembelea stendi hii ya kwa Mama Salmini nimekuta ipo katika mazingira hatari ya kupitiwa na Gridi ya Taifa kwa hiyo nikazungumza na Waziri wa Nishati akasema hapafai kwa matumizi ya stendi na pia miundombinu yake mibovu, hivyo wasafirishaji waendelee kutumia stendi yao ya zamani wakati Serikali ikiendelea kuweka mipango ya kujenga stendi mpya”,aliagiza Jafo.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Usafirishaji kwa njia ya barabara Tanzania (Tarotwu) Salum Abdallah,alisema kuwa pamoja na waziri kutoa agizo hilo lakini hali imeendelea kuwa mbaya kwani Sumatra na Halmashauri hiyo wanaendelea kuwalazimisha madereva kupeleka magari katika stendi hiyo jambo ambalo linapingana na kauli ya waziri huyo.
Alisema Aprili 9, walipata barua ya kutoka Sumatra Mkoa wa Pwani na mkuu wa polisi Mlandizi aliwaita juu ya kuwepo kwa barua hiyo ikiwataka lazima madereva wa abiria wapeleke magari yao katika stendi ya Mama Salmini na anayekahidi kupewa adhabu ya kutozwa faini.
“Tunashangaa jana magari ya abiria yamekamatwa na kutozwa faini ya Sh .30,000 kila moja kwa kugoma kwenda stendi ya Mama Salmini wakati Waziri aliagiza tutumie stendi yetu ya zamani jambo ambalo linaleta usumbua mkubwa kwa abiria hivyo tunamuomba Waziri haweze kusaidia jambo hili,”alisema Abdallah
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha Vijijini, Lemmy Ludovick,alisema waziri alipofika na kujionea alisema eneo la Mama Salmini sio salama kuwa stendi ya magari ya abiria na kusema waendelee na stendi yao ya zamani mpaka hapo stendi mpya itakapojengwa.
Alisema Serikali inafanya mpango wa kupata kiasi cha Sh.bilioni 7 kwa ajili ya kujenga stendi mpya hivyo kimsingi utaratibu wa kusaini mikataba ya kutumia stendi ya Mama Salmini imekosewa kwakuwa hapakuwa na ushirikishwaji wa wadau.
Meneja wa Sumatra Mkoa wa Pwani, Omary Ayubu,alisema kazi yao ni kutoa huduma kwa maeneo ambayo yanamahitaji hivyo wanaopaswa kuulizwa zaidi ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini pamoja na viongozi wengine wa Serikali akiwemo mkuu wa wilaya ya Kibaha.