MAHAKAMA ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) juzi ilizitaka Afrika Kusini na Burundi kufikiria upya uamuzi wao wa kujitoa kutoka chombo hicho kilichoanzishwa kukabiliana na uhalifu mbaya wa dunia.
“Ijapokuwa kujitoa kutoka chombo hiki ni hiari ya taifa huru, ninasikitika maamuzi haya na kuzikaribisha Afrika Kusini na Burundi kufikiria upya,” alisema Sidiki Kaba, Rais wa baraza kuu la mataifa yanayounda ICC.
“Ninaziomba kufanya kazi na mataifa mengine kukabiliana na vitendo vinavyotoa mwanya wa uhalifu, ambavyo mara nyingi husababisha ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu,” Kaba alisema katika taarifa yake.
Kauli hiyo ilikuja siku moja tu baada ya Afrika Kusini kutangaza kujitoa kutoka ICC, uamuzi ambao ni pigo kubwa kwa chombo hicho.
Hilo linatokana na utata wa mwaka jana wakati Rais wa Sudan Omar al-Bashir alipozuru taifa hilo na kushinikizwa kumkamata kutokana na tuhuma za uhalifu wa kivita katika eneo la Darfur nchini Sudan anazohusishwa nazo.
Mapema mwezi huu, Burundi ilisema itaondoka katika mahakama hiyo huko Namibia na Kenya zikieleza uwezekano kama huo.
ICC iliyoanzishwa mwaka 2002 mara nyingi inashutumiwa kwa kuwalenga zaidi viongozi wa Afrika na kushindwa kushughulikua uhalifu unaofanywa na mataifa makubwa kama Marekani ambayo haijasaini mkataba huo.
“Machafuko yako njiani. Maamuzi ya Afrika Kusini na Burundi yatasafisha njia kwa mataifa mengine ya Afrika kujitoa kutoka mahakama hii iliyopewa kazi ya kuhukumu uhalifu mbaya,” Kaba alisema kwa masikitiko.
Mwendesha mashitaka wa zamani wa mahakama hiyo, Luis Moreno Ocampo alizikosoa Burundi na Afrika Kusini akizituhumu kutoa fursa ya uhuru kwa viongozi wa Afrika kuendesha mauaji ya kimbari.
Ocampo, ambaye alikuwa mwendesha mashitaka mkuu wa kwanza wa mahakama hiyo alisema kitendo cha Burundi kujitoa kinatokana na hofu ya kushitakiwa kutokana na uhalifu unaotendeka nchini humo,
Burundi imekumbwa na machafuko yanayotokana na kitendo cha Rais Pierre Nkurunzinza kuwania urais kwa muhula wa tatu.