Na Charles Mtoi, HakiElimu.
HIVI majuzi nilikuwa nimekaa kwenye kibanda cha mjasiriamali mmoja, fundi wa viatu, nikisubiri usafiri wa daladala kwenda kibaruani. Kibanda kilikuwa kimefunikwa kwa turubai moja lenye nembo ya mtandao mmoja wa simu hapa nchini.Ilikuwa ni muda wa saa 11:30 asubuhi na mvua kubwa ilikuwa ikinyesha.
Kadri muda ulivyozidi kusogea, umati wa watu hapo kituoni waliokuwa wakija kupanda magari (daladala) ulizidi kuongezeka.
Pembeni yangu alikuwa amesimama mtoto wa kike aliyekuwa amebeba begi la vitabu na madaftari mgongoni, akiwa ameshikilia viatu ilivisilowe na maji ya mvua. Pia alikuwa na sare za shule; ni dhahiri mtoto huyu alikuwa akiwahi kwenda shuleni.
Lakini kila gari lililofika kituoni hapo halikuchukua wanafunzi maana tayari lilikuwa liamejaa. Lakini hata yaliyofika yakiwa nanafasi, watu wazima waligombania na kuingia. Aidha, takribani makondakta wote walikuwa wakimkataza mwanafunzi huyo kuingia katika daladala zao utadhani walishakubaliana tangu awali.
Ingawa watu wazima walikuwapo, hakuna hata mmoja wao aliyepaza sauti kumsaidia mtoto huyu. Kila mtu alijijali yeye pekee ilimradi apande daladala na kumuacha mtoto yule akiwa hana msaada wowote.
Hali hii ya manyanyaso ya makondakta wa daladala kwa wanafunzi imekuwa ni jambo la kawaida kwa miaka nenda rudi. Iwe asubuhi wakati wa kwenda shule au jioni wakati wa kurudi nyumbani hali ya mateso ni ile ile. Hata baadhi yetu waliobahatika kuwa na usafiri wao binafsi wa kuwatoa sehemu moja kwenda nyingine ni kama hawayaoni masahibu ya watoto hawa.
Ni, mara ngapi wamekuwa wakikuta makundi ya watoto wakihangaika kutafuta usafiri ama kwenda shule au kurudi nyumbani lakini wakipita kwa kasi huku wakiwa wamefunga vioo ili kupata kiyoyozi? Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba baadhi ya watu hawa ni wafanyakazi kwenye sekta ya elimu – iwe serikalini ama taasisi zisizo za kiserikali. Lakinihakuna wa kuwasaidia wanafunzi, kama mtoto huyu, ili wafike waendako.
Hali hii imekuwa moja ya mifano mingi ya jinsi watoto wanavyohangaika kutafuta elimu katika mazingira magumu na yenye shida nyingi. Changamoto hizi wamekuwa wakikabiliana nazo kukiwa na msaada mdogo kutoka katika jamii inayowazunguka; si wazazi, walezi wala taasisi za elimu.
Watoto wengi wa rika mbalimbali wamekuwa wakihangaika kutafuta elimu katika mazingira magumu. Mfano nilioutoa hapo juu ni kwa watoto wanaoishi mijini ambako wengi tunaamini kuwa kuna mazingira sahihi na salama kwa watoto kupata elimu. Lakini hata kwa wanafunzi wa vijijini mazingira ya watoto kupata elimuyamekuwa na changamoto lukuki. Ukiacha umbali ambao watoto hutembea kwenda nakurudi shuleni, kuna changamoto yakupata mahitaji muhimu kama vile chakula. Shule nyingi za kutwa hazitoi hudumaya chakula cha mchana.
Lakini kama binadamu wa kawaida, kuna siku tulishawahikujiuliza kuwa mtu mwenye njaa huwa anajisikiaje na anawezaje kufanya kazi mchana kutwa bila kuweka kitu chochote tumboni? Watu wazima baada ya kufanya kazi kwa muda huwa tunajiona tuna haki ya kupata angalau kitu cha kuweka tumboni ilituendelee na majukumu yetu.
Inakuwaje hatuoni kuwa huyu mtoto mdogo pia anahitaji kupata chakula ili aweze kuendelea na masomo vizuri?
Kama vile changamoto hizi hazitoshi, pia tumesikia pia ukatiliwa naofanyiwa watoto hata wakiwa katika mazingira ya nyumbani. Mathalani, tumesikiawatoto wakitekwa, wakipigwa hata wakibakwa. Tungetegemea kuona kuwa mazingiraya nyumbani ndiyo salama kwa watoto wetu, lakini kumbe si hivyo. Kutokana nahali ya upatikanaji wa kipato kuwa mgumu wazazi wengi wamekuwawakijishughulisha na shughuli za kuzalisha mali.
Hali hii imewaacha watoto kulelewa na majirani ama walezi ambao ndio wamekuwa vinara wa ukatili wa watoto wakiwa nyumbani. Hivyo ukweli ni kuwa sasa hivi mazingira ya nyumbani ndiyo yamekuwa chanzo kikuu cha kukithiri kwa ukatili kwa watoto.
Hivyo swali ambalo tunapaswa kujiuliza kama wadau wa elimu na jamii kwa jumla ni hatua gani gani zinapaswa kuchukuliwa kupunguza adha lukuki zinazopwakabili wanafunzi nchini?
Charles Mtoi ni Mratibu katika Idara ya , shirika la HakiElimu na unaweza kumtumia maoni kupitia barua pepe media@hakielimu.or.tz