NA MWANDISHI WETU - DAR ES SALAAM
ADHA ya usafiri imeendelea kuwakumba abiria wanaokwenda mikoani katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo kutokana na uchache wa mabasi kipindi hiki cha msimu wa Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.
Jana, gazeti hili lilishuhudia abiria wakiwa wamekaa chini kwa makundi ndani ya kituo hicho, huku wengine wakiwa katika harakati za kukata tiketi za mabasi ambayo si rasmi yakiwamo yanayotoa huduma ya usafiri jijini Dar es Salaam – daladala, ili kukamilisha safari zao.
Ndani ya kituo hicho, pamoja na mabasi yanayofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani, pia kulikuwa na daladala zilizokuwa zinapakia abiria kwenda mikoa ya Kaskazini.
Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa abiria aliyekuwa akielekea mkoani Kilimanjaro, Teddy Kiria, alisema kuwa alifika katika kituo hicho tangu saa 12 asubuhi akiwa na ndugu zake wanne, lakini wameshindwa kusafiri kwa wakati waliopanga baada ya kushindwa kumudu nauli kubwa iliyokuwa ikitozwa.
“Tumekuja hapa na ndugu zangu, tupo watano, akatokea wakala mmoja wa mabasi, akatuambia tiketi kwa sasa ni Sh 30,000 tukampa, baada ya muda aliturudishia hela akasema tumrudishie tiketi kwakuwa nauli imepanda kwa Sh 5,000 zaidi, yaani kutoka 30,000 hadi 35,000 na sisi tumeshindwa tumewarudishia tiketi zao,” alisema Teddy.
Alisema wameshindwa kulipa fedha hizo kwa sababu ni kiasi kikubwa sana wakisema nauli ya kutoka Dar es Salaam hadi Moshi inayotambulika na Sumatra ni Sh 19,500.
Mmoja wa mawakala wa mabasi aliyejitambulisha kwa jina la Silvan Msofe, alisema tatizo la usafiri, hasa kipindi cha sikukuu, linachangiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kwa kushindwa kusimamia vizuri wasafiri na wasafirishaji.
Alisema Sumatra wamekuwa wakitilia mkazo wa nauli na masharti kipindi cha sikukuu ambacho kinakuwa na abiria wengi wanaohitaji usafiri wa ziada.
“Sumatra wanaweka masharti magumu kipindi hiki bila kujua kama wanawasumbua wananchi, mfano katika upande wa nauli wameweka katika madaraja matatu daraja la chini ni Sh 19,500 na juu ni Sh 35,000 sasa huwezi kutumia nauli hizo kwa sasa kwa sababu watu ni wengi, wengine wanahitaji tuwasaidie tuwakodishie magari ili wasafiri kwahiyo nauli lazima iwe kubwa,” alisema Msofe.
Alisema utaratibu wa kukata kibali kwa magari ambayo si ya mikoani, unachukua muda mrefu na kusababisha watu kuchelewa.
“Hapa mtu binafsi nazungumzia hawa wenye madaladala, wakitaka kusafirisha watu wa mikoani wanaenda kufuata kibali Sumatra makao makuu kwa gharama ya Sh 7,000. Kwanini wasiwe na ofisi humu ndani wakapunguza usumbufu?” alisema Msofe.
Akijibu malalamiko hayo, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano, alisema tatizo la abiria kupandishiwa nauli linachangiwa na wenyewe kutotoa ushirikiano kwa taasisi hiyo.
“Hili tatizo la nauli linatokana na abiria kutokuwa na ushirikiano, mfano mtu analalamika kapandishiwa nauli hadi Sh 50,000 lakini katika gari hilo hilo mwingine anakataa hajalipa hiyo fedha na anakuonyesha tiketi iliyoandikwa nauli elekezi za Sumatra, katika mazingira hayo sasa mtu unamsaidiaje au huyo mwenye gari unaenda kumdai nini, abiria sio waaminifu,” alisema Kahatano.
Akizungumzia kuhusu utaratibu wa utoaji wa vibali na umbali wa ofisi, alisema vibali hivyo vinatolewa kwa njia ya kielektroniki – kwa njia ya mtandao na eneo pekee lenye kasi ya mtandao ni makao makuu ya Sumatra.