26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

ACT yaitaka Serikali kuchukua hatua kunusuru migogoro ya wakulima na wafugaji

Na Mwandishi Wetu, Lindi

Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kuchukua hatua za dharura kushughulikia migogoro ya Wakulima na wafugaji ili kuzuia maafa makubwa zaidi kutokea.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa ACT, Ado Shaibu Ado wakati akizungumza na Wanachama na Viongozi wa chama hicho katika Kata ya Kikole Jimbo la Kilwa Kusini wilayani Kilwa mkoani Lindi.

Sehemu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo.

“Migogoro ya Wakulima na wafugaji ni bomu linalosubiri kuripuka. Tayari migogoro hii imeshaleta maafa kwenye maeneo mengi nchini ikiwemo kutokea kwa mapigano makali baina ya wafugaji na wakulima. Hata hapa Kata ya Kikole nimeelezwa kuwa kuna mapigano yametokea leo na kuna mtu mmoja amefariki. Serikali isipochukua hatua za haraka, maafa makubwa zaidi yatatokea,” amesema Ado.

Amesema kuna mambo mengi yanayopaswa kufanywa na serikali katika kuhakikisha kuwa migogoro hiyo inakoma.

“Mosi, tunahitaji mipango bora ya matumizi ya ardhi. Yatengwe maeneo ya Wakulima na wafugaji na pasiwe na muingiliano. Mathalani, katika Mkoa wa Lindi, ardhi inayofaa kwa kipimo ni hekta 1,000,000 huku, zilizotumika ni hekta 400,000 sawa na 40%.

“Upande wa mifugo, hekta zinazofaa kwa mifugo ni hekta 450,000 huku zilizotumika zikiwa hekta 22,000 sawa na 5% tu. Hivyo basi, Mkoa wa Lindi hauna shida ya ardhi kwa ajili ya ufugaji na kilimo. Kinachokosekana ni mipango mizuri ya matumizi ya ardhi.

“Pili ni lazima Wananchi wa vijiji husika wasikilizwe na maamuzi yao yaheshimiwe. Mathalani, nimeelezwa kuwa hapa kuwa katika Kijiji cha Kikole, hakuna sehemu iliyotengwa kwa ajili ya wafugaji, lakini mifugo mingi inaingizwa na kuharibu mazao.

“Nani anayeruhusu mifugo hiyo? Ni dhahiri hapa patakuwa na mtandao wa rushwa inayonufaisha viongozi. Ni lazima Waziri Mwenye dhamana ya mifugo awajibike kwa kuchukua hatua kumaliza tatizo hili. La sivyo, ACT Wazalendo tutakuja na kampeni kumtaka ajiuzulu kama suala hili la migogoro ya wafugaji na wakulima halitopatiwa ufumbuzi,” amesema Ado.

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo akiambatana na Katibu wa Sera na Utafiti, Idrisa Kweweta yupo kwenye ziara ya Kata kwa Kata kwenye Jimbo la Kilwa Kusini yenye lengo la kuhakiki uhai wa Chama, kuhamasisha usajili wa Wanachama kwenye Mfumo wa ACT Kiganjani na kutoa mwelekeo wa kisiasa wa nchi ikiwemo kufafanua jitihada ambazo zinachukuliwa na chama hicho katika kupigania Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles