NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM
WABUNGE 21 na madiwani tisa wa Chama cha Wananchi (CUF) wamejiunga na Chama cha ACT Wazalendo.
Kati ya wabunge hao 19 wanatoka Zanzibar na kwa upande wa madiwani wanatoka katika manispaa za Temeke, Ilala na Ubungo.
Akizungumza baada ya kuwapokea wabunge na madiwani hao, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema chama hicho hakina muasisi na kwamba yeyote anayejiunga ni sawa na wanachama wengine.
“Wote ambao leo (jana) tunawakaribisha walikuwa ni wanachama wa Cuf, wakati tunateremsha tanga wenzetu hawa walikuwa na wakati mgumu sana, lakini kwa uzalendo waliokuwa nao walituambia tuwaache wamalize muda wao…walikuwa Cuf kiwiliwili lakini mioyoni mwao walikuwa ni ACT Wazalendo.
“Mnawapaka matope sana kwamba ni wasaliti, hawa si wasaliti tumekuwa nao bega kwa bega, sisi ruzuku yetu ni ndogo sana mambo mengi tunawategemea wao. Walikuwa wanajitoa, hawa ni mashujaa wetu, waheshimuni sana,” alisema Maalim Seif.
Wabunge hao na majimbo yao kwenye mabano ni Juma Kombo Hamad (Wingwi), Masoud Abdallah Salim (Mtambile), Ally Saleh Ally (Malindi), Ali Salim Khamis (Mwanakwerekwe) na Hamad Salim Maalim (Kojani).
Wengine ni Khalifa Mohamed Issa (Mtambwe), Mohamed Juma Khatib (Chonga), Twahir Awesu Mohamed (Mkoani), Khatib Said Haji (Konde), Haji Khatib Kai (Micheweni), Othman Omar Haji (Gando), Dk. Suleiman Ali Yussuf (Mgogoni) na Suleiman Bungara (Kilwa Kusini).
Katika orodha hiyo pia wamo Mbarouk Salim Ali (Wete), Nassor Suleiman Omar (Ziwani), Yussuf Salim Hussein (Chambani), Abdallah Haji Ali (Kiwani), Yussuf Haji Khamis (Nungwi), Mohamed Amour Mohamed (Bumbwini) na Mgeni Jadi Kadika (Viti Maalumu).
MADIWANI
Kwa upande wa madiwani na Ramadhan Kwangaya (Manzese), Jumanne Mbunju (Tandale), Ali Mohamed (Makumbusho), Omar Thabiti (Makurumla), Jumanne Kambangwa (Mbagala), Abdul Matogoro (Azimio), Abdalah Kipende (Mianzini), Safina Mgumba (Viti Maalumu Ilala) na Leila Madibi (Viti Maalumu Ubungo).
WATIA NIA
Maalim Seif pia aliwaasa wanachama wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu kuepuka kuwakashifu wenzao badala yake wanadi sera zitakazosaidia kuleta maendeleo kwenye kata na majimbo watakayogombea.
“Hatutaki mtumie majina yetu, kiongozi, mwenyekiti, makamu wangu hawana mgombea, katibu mkuu, manaibu katibu hawana mgombea, sisi kwetu wanachama wote ni sawa.
“Mtu yeyote atakayesema kwamba kiongozi kaniambia huyo ana ‘disqualified’ na ‘Iam very serious’, mimi ndiye mwenyekiti wa chama hiki, kila mmoja afuate kanuni na taratibu zetu za chama,” alisema.
Alisema wamekusudia kuingia kwenye uchaguzi kwa ajili ya kushinda kwani wao si chama sindikiza huku akijitapa watapata wagombea wazuri na wanaoaminika.
“Tunakwenda kwenye uchaguzi msitegemee mambo laini, lazima tujipange, sisi hatuna sababu kwanini tusishinde. Tuna viongozi wazuri ambao wanataka kuona Tanzania inabadilika,” alisema Maalim Seif.
ZITTO
Kwa upande wake Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe, alisema wanaingia kwenye uchaguzi wakiwa na matumaini makubwa na kwamba wanazo sababu zaidi ya 1,000 za kushinda uchaguzi mkuu ambazo wataziweka wazi wakati wa kampeni.
“Nchi yetu inahitaji sera ambazo zitainua hali ya maisha ya wananchi, Serikali ambayo itawapa katiba mpya, marekebisho ya muungano ili uwe wa haki sawa na kuheshimiana,” alisema Zitto.
ALLY SALEHE
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wenzake, Ally alisema mwanzoni walihofia kujiunga na chama hicho kwa sababu ungehitishwa uchaguzi mdogo wangeweza kupoteza nafasi zao.
“Tangu Machi 18 tulikuwa tunataka tujiunge lakini kwa sababu mbalimbali hasa kimkakati tukaendelea kubaki Cuf lakini tuliona siku haziendi. Kulikuwa na vitisho ili tumtii Lipumba na hatukushiriki mkutano wowote na hatukutoa hata ‘ndururu’…tulikuwa ni kiwiliwili utii wetu ni kwa ACT Wazalendo,” alisema Ally.
KAMATI KUU KUKUTANA
Katika hatua nyingine, Maalim Seif alisema kamati kuu ya chama hicho inatarajiwa kukutana leo kwa ajili ya kupanga maandalizi ya uchaguzi na kwamba kesho utaratibu mzima utaelezwa.
Alisema pia Juni 28 ataweka wazi msimamo wake kuhusu kugombea urais Zanzibar.