24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

UJENZI WA DARAJA LA WAMI KUFUNGUA FURSA NYINGI KIUCHUMI

Mwandishi Wetu-Pwani

SERIKALI imesema ukamilishaji wa ujenzi wa Daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 510 linalounganisha nchi yetu kupitia mikoa ya Kaskazini na nchi jirani za Afrika Mashariki litaongeza fursa nyingi za kiuchumi kwa Taifa kupitia Usafiri na Usafirishaji wa abiria na mazao.

Aidha imemtaka mkandarasi Power Construction Corporation anayejenga
Daraja hilo kutumia muda uliopo kufidia kazi zilizosimama kufanyika hasa nyakati za mvua nyingi.

Hayo ameyasema Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, katika ziara yake mkoani Pwani ambapo amekagua hatua zilizofikiwa za mradi huo na kuridhishwa na kasi ya mkandarasi ambapo kwa ujumla mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia 40.

“Watanzania niwahakikishie kuwa mradi huu utakamilika mapema kwa kuwa Serikali inahitaji daraja hili litumike haraka sana kwani litapunguza shida na adha nyingi ambazo watumiaji wa barabara hii wanapata ikiwemo upotevu wa mali nyingi”, amesema Naibu Waziri huyo.

Amesisitiza kuwa mradi huo hautakuwa na sababu yoyote ya kutoendelea kwa kuwa fedha zimetolewa kwa mkandarasi na ataendelea kulipwa kwa wakati ili kuhakikisha watanzania wanapata manufaa makubwa kwa nchi yao na rasilimali zao.

Kuhusu daraja la sasa linalotumika, Naibu Waziri huyo amesema kuwa mkandarasi anayejenga daraja jipya atafanya ukarabati wa daraja hilo baada ya kufanyiwa ukaguzi wa kina na wataalamu wa madaraja ili kuhakikisha daraja hilo linaendelea kuwa imara kila wakati.

Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa zaidi ya kiasi cha shilingi bilioni 723 zimelipwa kwa wakandarasi wote nchini wanaoendelea na miradi ya ujenzi ya miundombinu ili kuhakikisha hakuna miradi itakayosimama na wala kuwa na changamoto yoyote ya malipo.

“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutuamini kusimamia miradi hii mikubwa ya Kitaifa na sisi kama Sekta ya Ujenzi kazi yetu ni moja ya kuwezesha watanzania wawe na miundombinu sahihi ya kuwafanya waweze kutoa mchango wao wa kiuchumi,” amesema Kwandikwa.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo amekutana na mmiliki wa lori lililozama katika daraja hilo majuma mawili yaliyopita Mwajuma Selemani, na kutoa pole kwa uharibifu wa mali na kifo cha dereva wake.

Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Pwani Mhandisi Yudas Msangi, ameeleza kuwa kazi ya upimaji na uchimbaji wa msingi ya nguzo za daraja zimekamilika kwa asilimia 100 huku kazi zingine zikiendelea vizuri na wanaendelea kumsiamamia na kushirikiana na mkandarasi kwa karibu ili asicheleweshe mradi huo.

Ameongeza kuwa mpaka sasa kilometa 3 kati ya 4.3 ya barabara unganishi zimeshafanyiwa usafishaji na ufukuaji kwacha asilimia 70 ya barabara unganishi na kazi ya kukata vilima ili kupata usawa wa barabara nayo inaendelea vizuri kwa pande zote za daraja.

Ujenzi wa daraja jipya la wami ni mkakati wa Serikali wa kuondoa adha wanaoipata wasafirishaji na wasafiri wanaopita katika daraja hilo lililojengwa toka mwaka 1959 na kuonesha kutokidhi mahitaji ya magari yanayopita na kuwa jembamba na lenye njia ya kuwezesha kupitisha gari moja tu.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,310FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles