27.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

ACT-WAZALENDO SASA WAMTEGA CAG SUALA LA CHAKULA

Ado Shaibu
Ado Shaibu

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

CHAMA cha ACT – Wazalendo kimemwomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu katika maghala ya chakula kubaini ukweli juu ya kuwapo upungufu wa chakula nchini.

Hivi majuzi wakati akizungumza mkoani Dodoma, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alikaririwa na vyombo vya habari akisema serikali itaanza kusambaza tani milioni 1.5 za chakula zilizobaki msimu uliopita katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.

Alisema katika msimu uliopita kulikuwa na zaidi ya tani milioni tatu na kwamba baada ya wabunge kuitaka serikali kuruhusu kuuza vyakula nje, tani milioni 1.5 ziliuzwa na kubakia tani milioni 1.5.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Itikadi, Mawasiliano ya Umma na Uenezi wa chama hicho, Ado Shaibu, alisema kinapinga propaganda hiyo ya kusambaza tani milioni 1.5.

Shaibu alidai   hadi Oktoba mwaka jana chakula pekee kilichopo Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), ni tani 90,476.

Hata hivyo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, alisema hadi kufikia Januari 12, mwaka huu, NFRA ina akiba ya tani 88,152 za mahindi na kusisitiza kuwa hali ya chakula nchini inaridhisha.

“Mwenye njaa hahitaji kuambiwa ana njaa, njaa ni hali halisi na si jambo la kuambiwa au kutangaziwa, hasira na vijembe havitasaidia kutatua matatizo ya wananchi yakiwamo njaa.

“Wanaposema ipo akiba ya tani milioni 1.5, je zitatoka wapi, kwa sababu taarifa za Oktoba mwaka jana zinaonyesha akiba ya chakula iliyokuwapo ilikuwa tani 90, 476 tu. Je, serikali inaahidi kusambaza chakula hewa?” alihoji Shaibu na kuongeza:

“Tunaamini kukabiliana na matatizo ya wananchi ndiyo mtaji sahihi wa siasa kwa chama cha siasa. “Tunaikumbusha CCM kutekeleza jukumu lake la msingi la kuisimamia serikali badala ya kuhangaika na vyama vya upinzani vinavyotekeleza wajibu wake wa kikatiba na kisheria”.

Tayari viongozi mbalimbali wa dini wamewataka waumini wao wafanye maombi na kufunga kwa lengo la kukabiliana na ukame unaolikabili Taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles