NA FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam imemhukumu kifungo cha miaka minne jela au kulipa faini Sh milioni moja sambamba na kulipa fidia ya Sh milioni 20, Vishal Pandia (33) raia wa India, baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa Sh milioni 20.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Ilala, Flora Haule, alidai mahakama ilijiridhisha na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka ambao ulikuwa na mashahidi wanne.
“Mahakama imejiridhisha na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, hivyo inakutia hatiani kutumikia kifungo cha miaka minne jela au kulipa faini ya Sh milioni moja, pia unatakiwa kumlipa mlalamikaji fidia ya Sh milioni 20 ambazo unatakiwa kuzilipa kabla ya kulipa faini au kwenda jela, ili iwe onyo na fundisho kwa wote wenye tabia za wizi,” alisema Hakimu Haule.
Mtuhumiwa ambaye ni mhasibu, hakupewa nafasi ya kujitetea kwa kuwa alikuwa ameruka dhamana, na hivyo kuilazimu mahakama hiyo kutoa hukumu Novemba mwaka huu kabla ya kukamatwa tena jana na kusomewa hukumu upya.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, ilidaiwa kuwa mtuhumiwa katika tarehe isiyofahamika kati ya mwezi Aprili na Mei 2013, maeneo ya Kiwalani Dar es Salaam, aliiba Sh milioni 17.7 mali ya Kampuni ya Guru Engineering Work Ltd akiwa ameaminiwa fedha hizo kwenda kulipa ushuru TRA na badala yake alitoweka nazo. Mshtakiwa anatumikia kifungo.