NA AGATHA CHARLES
LICHA ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kukishauri Chama cha ACT-Tanzania kurudisha muundo wa uongozi uliokuwepo kabla ya kufukuzana ili kumaliza tofauti zao,lakini ushauri huo umekataliwa.
Katibu Mkuu wamuda wa chama hicho, Samson Mwigamba, alifanya mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam janana kutangaza kupeleka barua ya kupinga ushauri huo.
Akizungumza katika ofisi za chama hicho zilizopo Kijitonyama, Dar es Salaam, Mwigamba, alisema anaandaa barua hiyo kisha ataifikisha kwa Jaji Mutungi kwa nia ya kuutambua uongozi mpya.
“Huo ushauri tunamuomba Jaji Mutungi au kumtaarifu kuwa asonge mbele na kurekebisha mabadiliko, tunapeleka barua kwa Msajili leo (jana) kupitia fomu ya PP7 ili kuutambua uongozi huu uliopo na si wa kina Limbu,” alisema Mwigamba.
Alisema kwa kuwa Jaji Mutungi alijiridhisha kwamba mabadiliko yaliyofanywa na mkutano mkuu ni halali, wanaomba kumwondoa Kadawi Limbu katika nafasi ya mwenyekiti na kumweka kwa muda, Shaaban Mambo.
Alisema pia wanamwondoa Leopold Mahona na kumweka Mohamed Masaga katika nafasi yaNaibu Katibu Mkuu (Bara) na nafasi ya Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ofisi hiyo imtambue Hassan Abdalah Omary badala ya Grayson Nyakarungu.
Alisema kuna sababu tatu za kutochukua ushauri waJaji Mutungi wa kuwaacha viongozi hao madarakani ikiwemo kupinga kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wa kudumu ndani ya chama ambapo tayari ofisi hiyo imekitaka ACT kuufanya kabla ya Mei 5, mwaka huu.
“Sasa Limbu akirudi kuwa mwenyekiti atashikilia msimamo wake kuwa usifanyike uchaguzi na usipofanyika kuna tishio la kukifuta chama kwa mujibu wa sheria. Sababu ya pili ni kuwa hawa watu hawavumiliki ndani ya chama na tumejitahidikadiri ya uwezo wetu lakini imeshindikana, watu wanaotaka chama kifutwe,” alisema Mwigamba.
Alitaja sababu nyingine kuwa uamuzi uliowavua nyadhifa zao ni halali na ulitolewa na Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ambao hauwezi kufutika.
Katika hatua nyingine, alisema hakuna mgogoro ndani ya chama hicho na kuwataka wanachama hao kufanya kazi za chama kwa kuendelea na mchakato wa uchaguzi ujao.
Alisema hata kama kina Limbu wakikimbilia mahakamani kwa kuona kuwa wameonewa, wao wako tayari kwenda kutetea chama hicho popote ili kuilinda demokrasia.
Alisema Limbu pamoja na wenzake bado ni wanachama wa ACTna wanakaribishwa kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi ujao.
Alitoa ratiba za uchaguzi ndani ya chama hicho kuwa Machi 24, mwaka huu watakuwa na uchaguzi wa ngome ya wanawake huku Machi 25, mwaka huu ukifanyika uchaguzi wa ngome ya wazee na vijana.
“Machi 26 kutakuwa mkutano wa Halmashauri Kuu utakaochagua mwenyekiti wa taifa na makamu wake huku Machi 27 kunakuwa na mkutano mkuu. Machi 28,mwaka huu halmashauri kuu chini ya Mwenyekiti mpya itakutana kumchagua katibu mkuu na kuidhinisha manaibu na baadaya hapo Mei 29 kutafanyika mkutano mkuu wa kwanza Taifa utakaoambatana na uzinduzi wa chama utakaokuwa Dar es Salaam,” alisema Mwigamba.
Pia alisema Jumapili iliyopita Kamati Kuu ilikutana kwa dharura kwa ajili ya kupokea mapendekezo ya chama na ilichagua makatibu wengine wakiwemo Katibu wa Mipango na Matumizi, Nyanjura Tarimbo na Katibu wa Mawasiliano na Uenezi, Msafiri Mtemelwa aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa kampeni Chadema.
Kwa muda sasa kumekuwa na msuguano wa madaraka ndani ya chama hicho na kusababisha mpasuko wa pande mbili ikiwemo ya Limbu na nyingine upande wa Mwigamba hatua iliyofikishwa kwa Jaji Mutungi.