25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Lipumba awanusuru vijana wake na kipigo cha polisi

Ibrahim lipumbaNa Elizabeth Mjatta na Asifiwe George
MWENYEKITI wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba amezuia maandamano ya Jumuia ya Vijana wa chama hicho Taifa (JUVICUF) kwa kile alichokieleza kuwa ni hofu yake ya kupigwa , kuumizwa na hata kuuawa na Jeshi la Polisi waliokuwa wamejipanga kuzima maandamano yao.
JUVICUF walipanga kuandamana kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuishinikiza kuongeza muda wa uandikishaji katika daftari la wapiga kura.
Maandamano hayo pia yangefika hadi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kulishinikiza Jeshi hilo kuacha kuvunja haki za binaadamu ikiwemo kutumia nguvu kuwapiga raia.
Akizungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya chama hicho jana, Profesa Lipumba alisema kutokana na mazingira hayo mapema asubuhi aliamua kumpigia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam Kamishna Suleiman Kova, kumtaarifu kuwa vijana hawataandamana.
“Baada ya kuona mazingira hayo asubuhi nilimpigia Kamanda Kova simu kuwa vijana hawataandamana ili kuepuka polisi kuwavamia vijana na hata kuwajeruhi, nimewasihi vijana waache kuepuka matatizo hayo,” alisema Profesa Lipumba.
“Sababu za vijana wetu ni za msingi lakini nawaomba wasifanye tena maandamano kwasababu kuna hatari, wanaweza wakapigwa hata kwa risasi wakaumizwa na hata kuuawa.
Alisema NEC inapaswa kuyafanyia kazi malalamiko ya vijana wa chama hicho kwani ni ukweli usiopingika kama watanzania milioni 23 wakaandikishwa katika daftari kwa wiki moja.
“NEC inafanya ubabaishaji mtupu, hata jana (juzi) katika kikao chate na wao wametueleza mambo mengi lakini tumeona bado wanafanya kazi kwa usiri mkubwa na kwa kuamini hilo angalia hata tovuti yao haifanyi kazi,” alisema Profesa Lipumba.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa JUVICUF Hamidu Bobali alisema wamesitisha maandamano hayo kwa heshima ya Mwenyekiti wao Profesa Lipumba na si kwasababu alizozitoa Kamanda wa Polisi mkoa wa Dar es Salaam Suleiman Kova.
“Tumesitisha maandamano kwa heshima ya Mwenyekiti wetu, Kamanda Kova hana mamlaka ya kikatiba kutuzuia sisi kufanya maandamano, yeye anapaswa kutupatia ulinzi na si vinginevyo, isingekuwa mwenyekiti vijana tungeingia barabarani kwasababu tulishajiandaa kwa kila kitu” alisema Bobali.
Alisema NEC inapaswa kufanyia kazi malalamiko yao kwani wasipofanya hivyo baadaye yanaweza yakatokea machafuko.
“Huwezi kusema unawaandikisha watanzania wote kwa wiki moja, na serikali ielewe kuwa watanzania wa sasa wameelimika na wanafuatilia mambo, kama wasipotoa muda zaidi wa kujiandikisha watu hawatakubali kukosa haki yao ya kikatiba ya kupiga kura na mwisho wake yanaweza kutokea machafuko,”alisema Bobali.
Bobali ameitaka NEC kuzingatia dai la msingi la kuongeza muda wa kujiandikisha ili kila mtanzania aliyetimiza muda aweze kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
“Tunaoiomba NEC iongeze muda kutoka siku saba hadi siku 14 ili kila mtu apate fursa ya kutimiza hai yake ya kikatiba, endapo mambo haya hayatatekelezwa tutaendelea kupaza sauti na hatutasita kuingia tena barabarani,” alisema Bobali.
KOVA
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, amempongeza Mwenyekiti wa CUF Taifa Profesa Ibrahimu Lipumba kwa busara zake alizozifanya za kusitisha maandamano ambayo yaliyotakiwa kufanyika jana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamishna Kova alisema Prof. Lipumba alifanya mawasiliano hayo kutokana na vijana wa JUVICUF kujaribu kulazimisha kufanya maandamano baada ya Jeshi hilo kukataa vijana hao wasiandamane.
Kamishna Kova alisema Profesa Lipumba alimtumia ujumbe mfupi wa maandishi akiliomba Jeshi la Polisi kuendelea na shughuli zao za kawaida kwani tayari ameshafanya mazungumzo na vijana hao na tayari wamesitisha maandamano’.
“Namshukuru Profesa Lipumba kwa busara zake kwani baada ya kuona kwamba yangeweza kutokea mapambano ambayo yangesababisha madhara mbalimabli au hata umwagaji wa damu na wakati mwingine hata kwa watu ambao hawahusiki.
“Mimi naamini kwamba huu ni ukurasa mpya uliofunguka na ni fursa nzuri ambayo ilijitokeza kwa faida ya pande zote mbili kati yetu na chama hicho na hata vyama vingine vya siasa.
Polisi wajipanga
Katika kuhakikisha vijana waliokuwa wamejitokeza kushiriki maandamano hayo hawana njia ya kupita, askari wa kikosi cha kutuliza Ghasia (FFU) waliegesha magari yao kuelekea zilipo ofisi za chama hicho eneo la Buguruni.
Baadhi ya magari yalikuwa yakifanya doria kuzunguka eneo la Buguruni kuimarisha ulinzi na mengine yakisimama katika makutano ya barabara zinazoelekea katika ofisi hizo.
Juzi NEC ilitangaza kusogeza mbele uandikishaji wa wapiga kura kutoka Februari16 hadi 23 mwaka huu.
Uamuzi huo ulitangazwa na Mwenyekiti wa NEC Jaji mstaafu Damian Lubuva ambapo alisema wamesogeza mbele ili wapate muda wa kufanya maandalizi ya kutosha lakini pia vyama viweze kuandaa mawakala pindi kazi hiyo itakapoanza.
Hata hivyo hatua hiyo ilipingwa na viongozi wa vyama vya siasa ikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles