29.9 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wasira azua gumzo nchini

wassira_vifungoNA MWANDISHI WETU
KITENDO cha Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira, kukosea kufunga vishikizo vya koti lake kimegeuka gumzo katika mitandao ya kijamii nchini.
Wasira alikumbwa na kadhia hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa sherehe za Utume zilizoandaliwa na Kanisa la Waadventista Wasabato(SDA) huku Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, akiwa mgeni rasmi.

Katika tukio hilo lililohudhuriwa na kiongozi wa waumini wa dhehebu la Waadventista Wasabato Duniani, Askofu Ted Wilson, Wasira, alionekana katika mavazi nadhifu ya suti lakini koti alilokuwa amelivaa lilifungwa vishikizo kwa kukosewa.

Kabla ya tukio la kupiga picha ya pamoja, vazi la Wasira halikuwa na kasoro yoyote, lakini ilipofika hatua ya kupiga picha na viongozi mbalimbali waliohudhuria sherehe hiyo, mwanasiasa huyo mkongwe katika medani za siasa, alifunga kwa makosa vishikizo vya koti lake hatua iliyozua mjadala katika mitandao ya kijamii wengine wakichukulia kama kituko na kufanya utani.
Tangu kitendo hicho kitokee takriban wiki moja iliyopita, picha za Wasira akiwa katika vazi hilo la koti lililokosewa kufungwa vishikizo zimekuwa zikisambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwemo WhatsApp, Instagram, Facebook, Twitter na blog mbalimbali.
Kama haitoshi, baadhi ya watu ambao hawajafahamika nao wamepiga picha huku wakiwa wamevaa makoti kwa staili ya kupishanisha vishikizo na kisha kuzisambaza katika mitandao hiyo.
Baadhi ya watu wameanza kukihusisha kitendo hicho na harakati za kisiasa, hasa kutokana na jina la Wasira kutajwa katika nafasi ya urais.
Wapo wanaoamini kuwa kutokana na kasi kubwa ya kusambaa picha hizo, wapinzani wake wanaweza kuwa wametumia kama kete ya kisiasa kuhalalisha kauli ambazo zimeanza kuzagaa mapema kuhusu umakini wake.
Wapo ambao wameanza kuhoji kuhusu si tu umakini wa mwanasiasa huyo bali pia unadhifu hasa endapo akipewa madaraka makubwa kama ya urais.
Katika mjadala huu, kundi la vijana ndilo linaloonekana kuvutiwa zaidi na mtindo huo ambao wameupachika jina la ‘Wasira Staili’.
Katika mitandao mbalimbali ya kijamii wanaonekana baadhi ya vijana, wengine wakiwa wamevaa makoti ya sutina lile linalovaliwa na madaktari huku yakiwa yamekosewa kufungwa vishikizo.
Hata hivyo, wakati picha hizo zikiendelea kusambaa, katikati ya wiki hii picha nyingine zikaibuka zikimuonyesha Wasira akipimwa vipimo vya nguo na mbunifu wa mavazi, Sheria Ngowi.
Ngowi amekuwa akiwabunia mavazi viongozi mbalimbali nchini akiwemo Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na sasa Wasira.
Gazeti hili lilimtafuta Wasira kwa njia ya simu ya mkononi ili aelezee kitendo hicho jinsi kilivyotokea lakini hakupokea simu yake kila alipopigiwa.
Hata hivyo, chanzo cha karibu na Wasira kimedokeza kuwa ameziona picha hizo zinazosambazwa lakini amepuuza kwa kusema ni jambo dogo hivyo hawezi kulizungumzia.
Lakini alikiri kuchukuliwa vipimo kwa ajili ya kutengenezewa suti na Ngowi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles