Na Malima Lubasha, Musoma
Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Tarime/Rorya, Mara, ACP Mark Njera amewataka waandishi wa habari wasiwe wanyonge wakati wanatekeleza majukumu yao ya kihabari bali wazingatie weledi,maadili, sheria ili kuondoa migongano kati yao.
ACP Njera amesema hayo kwenye mdahalo baina ya Jeshi la Polisi na waandishi wa habari juu ya ulinzi na usalama uliofanyika katika ukumbi wa Blue Sky mjini Tarime.
Amesema mdahalo huo umefungua ukurasa mpya na uwe chanzo cha kuondoa tofauti kwa kuimarisha ushirikiano baina ya Jeshi la Polisi na waandishi wa habari katika kutekeleza majukumu yao kwa kuwa kazi zao zinaendana.
Ameeleza kuwa kila mmoja anapotekeleza majukumu yake ni lazima kuzingatia kanuni na sheria na kwamba Jeshi la Polisi limekuwa linatoa taarifa chache kwani kila jambo lina mipaka yake kuhusu usalama wao.
“Waandishi wa habari mnatakiwa kuandika habari za kweli zilizothibitishwa zinazoibua mambo yanayoleta tija kwa jamii kinyume chake zinaweza kuleta migongano baina ya taasisi na viongozi,” amesema Kamanda Njera.
Amesema amebaini baadhi ya changamoto zinazowakabili waandishi wa habari katika kutekeleza majukumu yao kwamba usalama ni mdogo ambapo ametaka uanze kwa mwandishi mwenyewe na wamiliki wa vyombo vya habari wawape mafunzo kuhusu usalama ikiwemo kuvaa mavazi maalum ya kumtambulisha anapokuwa kazini.
Aidha ACP Njera ameshukuru UTPC kwa kuandaa mdahalo huo baina ya Jeshi la Polisi na waandishi wa habari ambapo kwa matarajio ya kuwa na wazo moja kujadiliana ili kuondoa changamoto zao katika kulinda jamii na mali zao.
Mwakilishi wa UTPC katika mdahalo huo Edmund Kipingu, amesema mdahalo huo umeandaliwa ili kuboresha mahusiano baina ya Jeshi la Polisi ambao huchukua hatua kwa wakosaji na waandishi wa habari ambao kazi yao kuandika kuhabarisha umma hali inayoleta migangano.
Amesema ili wawe marafiki wanatakiwa kushirikiana wanapotekeleza majukumu yao kwenye mabonanza, washirikishwe katika kutoa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia kwani hiyo itakuwa ndiyo njia ya kuondoa changamoto baina yao.