Na MWANDISHI WETU,
UTATA na ubishani uliojitokeza hivi karibuni kuhusu makontena yenye makinikia ya madini ya dhahabu, shaba na fedha yaliyopo kwenye Bandari ya Dar es Salaam ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na uelewa mdogo wa mchakato mzima wa uchimbaji wa dhahabu na taratibu za usafirishaji wa makinikia nje ya nchi kwa ajili ya uchenjuaji.
Maafisa wa Acacia Mining Plc wanaeleza kushangazwa kwao na mjadala unaoendelea nchini hivi sasa kuhusu makontena hayo yaliyokutwa bandarini wakati Rais John Magufuli alipofanya ziara ya kushitukiza.
Kwa maoni ya maafisa hao, watu wengi hawajui kwamba makontena hayo yaliyopo bandarini hayakukamatwa kama ilivyoripotiwa, bali yalikuwa chini ya mamlaka za serikali baada ya mchakato wenye uwazi mkubwa wa kuyasafirisha ulioanzia migodini.
Baada ya kutoka mgodini, makinikia huwekwa kwenye makontena kwa kusimamiwa na maafisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA), afisa wa Forodha kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), afisa mwakilishi wa wakala wa meli, mwakilishi wa kampuni ya mgodi husika pamoja na mwakilishi wa kampuni inayotoa huduma ya kitaalamu ya maabara.
Utaratibu uliopo ni kwamba sampuli ya makanikia huchukuliwa na TMAA kwa niaba ya serikali pamoja na mgodi husika ili kubaini kiwango cha madini yenye thamani; dhahabu, shaba na fedha.
“Baada ya majibu ya maabara kuonesha kiwango cha madini yaliyomo ndani ya makanikia, thamani ya madini hayo hukokotolewa, kisha mrahaba (royalty) stahiki unakokotolewa, kisha kampuni hufanya malipo hayo kwa wizara ya nishati na madini, kabla ya kutolewa leseni ya kusafirishwa (export permit),” inaeleza sehemu ya taarifa ya Acacia.
Inaongeza kuwa makontena yenye makanikia huweza kuondolewa mgodini tayari kwa kusafirishwa endapo tu michakato hii imekamilika, ikiwa ni pamoja na uhakiki wa madini yaliyopo kwenye makinikia na kodi stahiki kulipwa serikalini.
Wanaeleza pia kuwa mpaka wakati makontena hayo yanakabidhiwa kwa mamlaka husika, Acacia ilikuwa imekwishailipa serikali Dola za Marekani milioni 1.319,777 sawa na Sh bilioni 2.94 za Kitanzania kwa mrahaba na kiasi kingine cha dola za Marekani 128,270.70 (Sh 286,043,661) kama kodi.
“Inashangaza watu wanaposema makontena yale yalikamatwa bandarini. Ukweli ni kwamba makontena hupelekwa Container Freight Services (CFS) na baadaye kwenye skena (scanner) ya Forodha kabla ya kuingizwa kwenye meli. Kuanzia mgodini mamlaka zote za serikali zinahusika katika kuthibitisha kilichomo ndani ya makontena kwa kuchukua sampuli na kupima kwenye maabara,” anafafanua Ofisa wa Acacia.
“Kwa utaratibu wa kiforodha makontena yale yote yapo chini ya usimamizi wa mamlaka ya Serikali. Kwa hiyo, unawezaje kusema yamekamatwa?” anahoji ofisa huyo na kuongeza kuwa makontena 20 yaliyokutwa na Rais Magufuli bandarini yalikuwa tayari yamepata meli ya kuyasafirisha huku mengine 256 yakiwa kwenye mchakato wa awali.
Anaeleza kuwa hakuna utaratibu uliokiukwa katika mchakato wa kusafirisha makontena hayo na kwamba zuio lililotolewa na Rais lilikuja wakati makontena hayo yamekwishaondoka migodini, Bulyanhulu na Buzwagi.
Wakati wa ziara ya Rais Magufuli siku kadhaa zilizopita, vyombo vya habari viliripoti kuwa makontena 20 ‘yamekamatwa’ bandarini yakiwa katika hatua ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi. Siku tatu baadaye, iliripotiwa kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) ‘ilikamata’ makontena mengine 256 yenye makinia ya dhahabu yaliyokuwa yamehifadhiwa katika bandari kavu ya MOFED Kurasini yakisubiri taratibu za kiforodha kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.
Taarifa hizo zilimshtua Spika wa Bunge la Muungano wa Tanzania, Job Ndugai na kumlazimu kutembelea Bandari ya Dar es Salaam akiongozana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini katika jitihada za kubaini ukweli kuhusu makontena hayo yenye makinikia.
Akiwa bandarini, Ndugai alizungumza na waandishi wa habari na kueleza azma yake ya kuunda kamati ya Bunge itakayochunguza uchimbaji na usafirishwaji wa makinikia hayo, huku Rais naye akiunda kamati ya wataalamu watakaofanya uchunguzi ili kubaini kiwango cha madini kilichomo ndani ya makontena yaliyozuiwa.
Haya yametokea baada ya Machi 2 mwaka huu, Rais Magufuli kuzuia usafirishaji wa makinikia nje ya nchi kwa ajili ya kuyeyushwa ili kupata mabaki ya madini yaliyoshindikana baada ya hatua ya kwanza ya uchenjuaji kufanyika mgodini.
Wakati huo huo, Maafisa wa Acacia wamefafanua kuwa katika mchakato mzima wa uzalishaji wa dhahabu serikali ndio inayonufaika zaidi, tofauti na taarifa za upotoshwaji zinazotolewa mara kwa mara.
Wanasema serikali huchukua asilimia 15 kama kodi mbalimbali na mirahaba, wakati asilimia 10 hulipa mikopo na riba, huku asilimia 57 ya mapato yote yakitumika kwa ajili ya gharama za uzalishaji na asilimia 10 huenda kwa wenye hisa waliowekeza fedha zao na asilimia kumi ni uwekezaji mpya kwenye mitaji na mashine zinazotumika katika uchimbaji.
“Kwa hiyo, ukweli ni kwamba serikali ndio inayochukua kiasi kikubwa cha mapato ya uzalishaji mzima wa dhahabu,” anaeleza afisa mwingine na kufafanua kwamba mrahaba wa asilimia nne unaotolewa na Acacia ni wa juu zaidi katika uzalishaji wa dhahabu duniani kwani nchi nyingi hulipa mrahaba chini ya hapo.
Anasema itakuwa vema Bunge likiunda kamati ili kujiridhisha na masuala mbalimbali yanayohusu uchimbaji wa dhahabu, ikiwa ni pamoja na thamani halisi ya kilichomo kwenye makinia ya dhahabu, kama alivyoahidi Spika Ndugai.
Akiwa bandarini Ndugai alitilia shaka kile kinachoelezwa kuwamo kwenye kontena moja ambapo dhahabu ni asilimia 0.02 tu ya uzito wote.
Lakini maafisa hao wanafafanua kuwa pamoja na kwamba uzito wa dhahabu kwenye kontena la tani 20 ni asilimia 0.02 tu, dhahabu inayopatikana baada ya uchenjuaji ni kilo 3.1 kwa kontena. Madini mengine yanayopatikana baada ya uchenjuaji ni shaba na fedha.
Kumekuwa na taarifa potofu kwamba kila kontena moja la makinikia limejaa dhahabu kiasi cha asilimia 90 ya uzito wote wa kontena. Hii inamaanisha kwamba makontena yote 276 yaliyopo bandarini kwa sasa yana dhahabu kiasi cha tani 4,968, jambo ambalo si sahihi. Jumla ya uzalishaji wa dhahabu yote duniani kwa mwaka haizidi tani 3,000.
“Haiingii akilini mtu anaposema kwamba uzalishaji wa migodi miwili ya dhahabu Tanzania kwa muda wa miezi miwili unazidi uzalishaji wa dhahabu wa mwaka mzima duniani,” anafafanua afisa mmoja.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, pamoja na kuonekana kuwa na asilimia ndogo zaidi ya uzito (asilimia 0.02), thamani ya dhahabu inayopatikana baada ya uchenjuaji ni asilimia 86, huku thamani ya madini ya fedha huwa ni asilimia 0.94 na shaba asilimia 12. Thamani ya uchafu (waste) huwa ni asilimia sifuri licha ya kuwa na uzito wa asilimia 86.
Kwa wastani migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu kwa ujumla huzalisha jumla ya makontena 200 kwa mwezi, ambayo ni wastani wa makontena 2,400 kwa mwaka.
Kwa bei ya sasa, thamani ya dhahabu kwenye kontena moja ni karibu Dola za Marekani 120,000; shaba dola 15,000 na fedha dola 1,700. Nusu ya mapato ya migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu inatokana na kilichomo kwenye makinikia, kwa mujibu wa Acacia.
Usafirishaji wa makinikia kwenda nchi za nje kwa ajili ya uchenjuaji ni jambo la kawaida katika sekta ya madini na hufanywa na nchi mbalimbali zinazozalisha makinikia, zikiwamo zenye uzalishaji mkubwa na mdogo. Baadhi ya nchi hizo ni pamoja na Peru, Australia, Papua New Guinea, Saudi Arabia na Argentina. Nchi za Afrika ni pamoja na Morocco, Eritrea na Mauritania.
Utafiti uliofanywa na TMAA mwaka 2001 ulionesha kuwa hakuna manufaa ya kibiashara kujenga mtambo ya kuyeyusha makinikia (smelter) nchini kutokana na uzalishaji mdogo wa mchanga huo pamoja na gharama kubwa itakayotumika.