26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

RIPOTI MAALUMU: SABABU TANZANIA KUSHIKA MKIA VIWANGO VYA FURAHA DUNIANI

Ukosefu wa ajira kwa vijana unachangia kwa kiasi kikubwa kuwakosesha wananchi furaha
KILA mwaka, Mtandao wa Umoja wa Mataifa wa Suluhu za Maendeleo Endelevu (UN-SDSN) hutoa ripoti inayoorodhesha mataifa yenye furaha zaidi duniani.

Tangu ripoti hizo zianze kutolewa wakati wa uongozi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyepita, Ban Ki-Moon, nchi za Scandinavia zimekuwa zikitawala katika nafasi 10 za juu za orodha hiyo.

Mataifa tajiri ya magharibi yakiongozwa Marekani (14) na Uingereza (19) yako ndani ya 20 na 30 bora na hivyo kuashiria utajiri si sababu pekee ya kuwafanya watu kuwa na furaha. 

Nchi ya Norway imeshika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Denmark, ambayo kwa muda mrefu ilikuwa kinara katika orodha hiyo ikifuatiwa na Iceland na Uswisi.

Kama kawaida mwaka huu mataifa yaliyoshika nafasi za mwisho yanatokea kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika pamoja na mataifa yanayoandamwa na vita.

Nchi hizo zimepata alama za chini; kwa mfano Syria iliyosambaratika kwa vita za wenyewe kwa wenyewe imeshika nafasi ya 152 huku Yemen na Sudan Kusini, ambazo mbali ya vita zimeathirika kwa baa la njaa zikichukua nafasi za 146 na 147 kati ya mataifa 155.

Taifa ambalo hakuna shaka limewashangaza wengi si tu wananchi wake bali pia wataalamu wa nje ni Tanzania.

Tanzania pamoja na kuwa tangu ripoti hizo zianze kuchapishwa imekuwa ikishuka katika orodha hiyo mwaka hadi mwaka, mwaka huu imefanya vibaya zaidi baada ya kushika nafasi ya tatu kutoka mkiani.

Mshangao huo, unatokana na ukweli Tanzania haiko vitani na haina matatizo makubwa ya kijamii, baa la njaa na ina utawala unaosifika kwa kupambana na ufisadi kete iliyotosha kupaisha alama zake.

Ina hali ambayo huwezi kuilinganisha na mataifa kama Somalia, DRC, Zimbabwe, Sudan Kusini na nyinginezo ambazo zimelipiku taifa hili linalojulikana kama kisiwa cha amani.

Orodha hiyo iliandaliwa kwa kuangazia pato la mtu kwa mwaka, wastani wa umri wa kuishi, utegemezi wa usaidizi, dhana ya kuwapo uhuru wa kufanya uamuzi maishani, kutokuwapo ufisadi na ukarimu.

Mwaka jana, Tanzania ikiwa katika kundi la mwisho la nchi 10 ambazo zilikuwa Madagascar, Tanzania, Liberia, Guinea, Rwanda, Benin, Afghanistan, Togo, Syria na Burundi, ilishika  nafasi ya 149 kati ya nchi 157 ikiwa na alama 3.695 kati ya alama 10.

Kwa maana hiyo Tanzania mwaka 2016 ilishika nafasi ya nane kutoka mkiani, lakini mwaka huu imeshuka zaidi hadi ya tatu kutoka mkiani ikiwa na alama 3.349.

Waandishi wa ripoti hiyo walishangazwa na Tanzania kupata alama za chini mno kiasi hicho.

 “Ina thamani inayotabirika, iliyoegemea katika ufanisi wao kwenye vigezo muhimu sita; nguvu ya uchumi, msaada wa kijamii, wastani wa umri wa kuishi, uhuru wa kuchagua, ukarimu na kiwango cha rushwa, ambavyo vilitosha kuipatia alama za juu kuliko ilizopata katika utafiti huo.”

Ni Burundi na Jamhuri ya Afrika ya Kati tu pekee ambazo zina matatizo ya kisiasa na kivita zilizopitwa, ikimaanisha kama zisingekuwapo Tanzania ingeshika mkia duniani.

Kwingineko ukanda wa Afrika Mashariki Rwanda imeshika nafasi ya tano kutoka mwisho, Uganda 23 na Kenya 44 huku Somalia ikishika nafasi ya tano barani Afrika kwa watu wake kuwa na furaha.

Mwaka jana Somalia ilishika nafasi ya 76 duniani baada ya kupata alama 5.44 kati ya nchi 156 duniani.

Aidha, katika ripoti ya Furaha Duniani mwaka 2013, Tanzania ilishika nafasi ya 39 barani Afrika ikiwa ya tatu miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki, baada ya Uganda na Kenya.

Katika ripoti hiyo, Tanzania ilipitwa na taifa kama Somaliland ambayo imejitenga kutoka Somalia iliyoko katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 1991 alipopinduliwa Rais Siad Barre.

Wakati baadhi ya mataifa ya magharibi yakijiuliza sababu ya kuwa nyuma ya mataifa kama Norway licha ya ustawi na utajiri wao mkubwa, Tanzania nayo yajiuliza sababu ya kushika mkia, mbaya zaidi ikipitwa na mataifa yaliyokithiri kwa vita na umasikini kama Somalia na Sudan Kusini.

Kwanini furaha miongoni mwa Watanzania inashuka mwaka hadi mwaka huku ikiwa ya chini kulinganisha na mataifa kama Zimbabwe, DRC, Somalia iliyosambaratishwa na vita?

Kwanza tuangalie kile wanachosema waandishi wa ripoti kwa ujumla na kuchambua walichoandika katika baadhi ya nchi.

Pamoja na mambo mengine ripoti ilihitimisha kwa kuzishauri nchi za Afrika kuwekeza zaidi miongoni mwa vijana ili kuimarisha viwango vyao vya furaha.’

Kwamba mataifa ya Afrika yawaangazie zaidi vijana wake kuwawekea mazingira yatakayowafanya wawe na ndoto zenye matumaini na ustawi kwa maisha yao ya baadaye.

Kwa kufanya hivyo vijana watajijengea imani na ari ya ujasiliamali na uwekezaji katika maendeleo yao.

Katika hilo, wanaamini nchi za Afrika, ambazo hazipo ndani ya 50 bora zitaingia katika orodha ya mataifa yenye ustawi na furaha duniani.

Aidha, ripoti inaonesha Somalia licha ya kusambaratika kwa vita wakiwa wanasikia miziki ya mabomu kila uchwao, watu wake wameweza kuwa na furaha kuhusu nchi yao.

Katika suala la kipato (GDP), wastani wa umri mzuri wa kuishi hazikutoa mchango wa kutosha katika kuchangia alama za kiwango cha furaha ilizopata Somalia.

Watafiti waliona zaidi hisia za ukarimu miongoni mwa Wasomali ‘wakishikana vilivyo’ kutokana na masaibu yanayowakabili pamoja na kile watafiti walichokiita ‘masazo ya furaha’ kuwa ndizo zilizowabeba Wasomali na  kuwafanya waonekane kuwa na furaha kuliko taifa lolote lile la Afrika Mashariki.

Kwa Tanzania nini tatizo?

Kwa kuangalia mfano wa Somalia, watafiti hawakutumia vigezo vilivyowekwa kwa uzito sawa katika kulinganisha viwango vya furaha kutoka taifa moja hadi lingine.

Tanzania huwezi kuilinganisha na Somalia kwa kila hali na hivyo vigezo vinaangaliwa kwa uzito tofauti ikimaanisha kwamba ina safari ndefu kuboresha furaha kwa watu wake.

Kwa mujibu wa ripoti, alama 3.349 ilizopata Tanzania zilichangiwa kidogo na utegemezi wa kijamii, ikifuatiwa na GDP pamoja na ‘masazo ya furaha’.

La kushangaza kigezo cha ‘kiwango cha ufisadi kama ilivyo kwa mataifa mengine kilishika mkia kwa mchango mdogo katika alama hizo.

Licha ya amani na ustawi usiolingana na mataifa mengine yenye matatizo luluki, Watanzania wanaonekana kukata tamaa, hawana furaha ya maisha yao, vijana hawajui hatima yao ya baadaye na hawafurahishwi na mwenendo wa mambo wanaouona nchini.

Hali hiyo tunaweza kuifananisha na ile inayolikabili kundi fulani la jamii lisilofurahishwa na hali ya mambo kuanzia ufisadi hadi kuhisi kutengwa au kuishi katika udhalili nchini Marekani.

Ni kundi hilo lililolikosesha taifa hilo tajiri duniani kuwamo ndani ya 10 bora za mataifa yenye furaha.

Tofauti na Marekani, Norway, ambako mbali ya ustawi wa kijamii kuna kiwango kidogo cha ufisadi na huduma za kijamii au afya zinazoeleweka na hivyo wananchi wake hawana wasiwasi na maisha au hatima ya maisha yao.

Ukiachana na mfano huo wa Marekani na Norway, nchini Tanzania kama ilivyo sehemu nyingine za Afrika kuna kundi kubwa la vijana, ambao kwa mujibu wa utafiti wanachuka asilimia 70 ya watu wote Afrika.

Ni kundi linalokabiliwa na ukosefu wa ajira na sintofahamu kuhusu hatima ya maisha yao na hivyo kukosa furaha.

Katika suala la vita dhidi ya ufisadi lilipaswa kuipatia Tanzania alama kutokana na utawala wake wa sasa kuonekana kulivalia njuga suala hilo.

Lakini miongoni mwa vigezo sita vilivyotumika kutathimini furaha kigezo hicho cha ‘kiwango cha ufisadi’ kilishika mkia katika kuichangia alama za furaha.

Tafsiri ya hiyo ni nini? Watanzania wana hasira na uchungu wanaokumbana nao, kiasi kwamba hawaoni vita inayoendelea dhidi ya ufisadi wala furaha ya kuishi ndani ya ‘kisiwa cha amani.’

Ripoti hiyo inakuja huku nyingine iliyotolewa hivi karibuni na Benki ya Dunia ikionesha Tanzania na Uganda zikishika mkia Afrika Mashariki kwa wananchi wake kukosa utayari wa kuripoti matukio ya rushwa zikifuatiwa na Kenya, Burundi na Rwanda ambayo ina rekodi nzuri.

Aidha, kuna ripoti nyingine kuhusu ukarimu, ambayo imeiweka Tanzania mkiani miongoni mwa mataifa ambayo watu wake ni wakarimu duniani.

Hili linaweza kushangaza kwa vile, Watanzania wanajulikana kwa ukarimu kulinganisha na Wakenya, lakini ripoti imeziweka Kenya na Uganda juu.

Katika hili, ukarimu wa Watanzania unaonekana mdomoni kuliko kwa vitendo kulinganisha na Wakenya, ambao kwa mujibu wa utafiti harambee wanazoendesha kuchangia maendeleo ikiwamo elimu, miundo mbinu ya kijamii na kadhalika zinawabeba mno.

Ni tofauti na Watanzania, ambao wanaonekana kuwa wazuri zaidi kuchangia michango ya harusi, ambayo kwa vile si ya kimaendeleo haiwezi kutumika katika kigezo cha ukarimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles