TOKYO, JAPAN
WAZIRI Mkuu wa Japan, Shinzo Abe ameshinda kwa kishindo uchaguzi wa mapema, ambao umempatia mamlaka inayoimarisha msimamo wake mkali dhidi ya Korea Kaskazini.
Chama chake cha kihafidhina cha Liberal Democratic (LDP kilipata ushindi wa viti 311 katika Bunge lenye viti 465, kwa mujibu wa matokeo ya awali.
Ushindi huo utamfanya Abe kuwa kiongozi aliyekaa madarakani muda mrefu zaidi nchini hapa.
Aidha ushindi huo bila shaka utaongezea nguvu dhamira ya Abe kupambana na hatari ya nyuklia inayoletwa na Korea Kaskazini.
Mamilioni ya Wajapan walijitokeza kupiga kura licha ya mvua kubwa na upepo mkali, wakati kimbunga kiliposhambulia taifa hilo.
Wengi walipiga kura zao mapema baada ya kutolewa tahadhari ya kimbunga hicho.
“Naunga mkono msimamo wa Abe katika kuipa Korea Kaskazini mbinyo,” alisema mpiga kura mmoja, Yoshihisa Lemori, wakati akipiga kura yake huku mvua kubwa ikinyesha mjini Tokyo.
Hata hivyo, LDP imefaidika kutokana na upinzani dhaifu na uliogawika huku vyama vikuu viwili vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi huo vikiwa vimeundwa wiki kadhaa tu zilizopita.