Na Brighiter Masaki, Dar es Salaam
Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo nchini (TCCIA) kimeingia makubaliano na Mwimbaji wa Nyimbo za Injili, Abigail Chamungwana ‘Abby Chams’ kuwa Balozi wa kutoa elimu ya kuwahamasisha vijana wanasoma vyuo mbalimbali kujiunga na ujasiriamali.
TCCIA imekuja na programu hiyo baada ya kubaini kunachangamoto ya ajira na vijana hawana hamasa ya kutosha kujiunga na ujasiriamali licha ya kwamba ni sehemu ambayo wanaweza kujiajiri.
Akizungumza Dar es Salaam Ijumaa Julai 16, 2021 mara baada ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA, Gedfrid Muganda, amesema wameingia mkataba wa miaka mitatu na dhamira yao ni kuwafikia vijana wote waliopo nchini.
“Tumeanzisha programu hii ya utoaji elimu kuwahamasisha vijana hasa wanaosama vyuo vikuu ili wajiunge na ujasiriamali kwa kuwa ni kazi kama zilivyokazi zingine lakini wanakuwa fursa kubwa ya kujiajiri,” amesema Muganda.
Muganda amesema hadi kumchagua Abby walizingatia sifa mbalimbali ikiwemo ushawishi wake kulingana na kazi anayoifanya ya uimbaji, hivyo wanaamini atakuwa na uwezo wa kuwashawishi vijana kujiunga na ‘TCCIA youth member’
Kwa upande wake mwimbaji huyo ameishukuru TCCIA, kwa kumpatia fursa hiyo na kuwahakikishia atatumia kipawa alichojaliwa na Mungu kuwashawishi vijana kujiunga na chama hicho.
“Asilimia kubwa ya Watanzania ni vijana na mimi nipo kwenye kundi hilo nimepewa nafasi hii nitaitumia vizuri kuona vijana wanajiunga na ujasiriamali kwa lengo la kujiajiri,”amesema Abby.
Abby ni Msanii wa kuimba na kupiga vyombo mbalimbali vya muziki kama kinanda, trampest na saxaphone pia ni mwandaaji wa matamasha ya watoto wakike na vijana kuhusiana na mahusiano.