Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
Wazazi nchini wameombwa kutowazuia watoto pindi wanapoonesha vipaji vyao badala yake waviendeleze kwa manufaa yao na ustawi wa jamii.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Afisa Elimu wa Kata ya Bunju, George Mwamasangula, kwenye mahafali ya 10, ya Shule ya Awali Lavender, iliyopo Bunju ‘A’ Manispaa ya Kinondoni.
“Naomba wazazi niwaase kuwa endapo mtoto akionesha kipaji chake asizuiwe mwacheni badala yake mtoe ushirikiano na walimu kusudi kuzingatia ratiba yake ya kusoma na michezo, kwani wengi wamefanikiwa kupitia vipaji walivyonavyo,” amesema Mwamasangula.
Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Shule hiyo, Vida Ngowi, amesema mbali na mahafali hayo kituo kinaadhimisha miaka 10, tangu kilipoanzishwa.
Amesema kituo hicho kilianza kikiwa na wanafunzi watatu na mwalimu mmoja, mwaka 2010 ila kwa sasa kina jumla ya  wanafunzi 70.
“Hapa tunafundisha masomo mbali mbali ya awali kwa mwongozo wa Serikali pamoja na kuwaandaa watoto kimwili,kisaikolojia pamoja na elimu kwa njia ya michezo,” amesema Ngowi.