27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

TMA: Joto kuongezeka nchini

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa juu ya hali ya ongezeko la joto katika baadhi ya maeneo nchini.

Taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Sakaam na TMA, imesema kuwa kwa kawaida kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Machi kila mwaka jua la utosi linakuwa katika maeneo ya kizio cha kusini mwa dunia.

“Tanzania ikiwa ni moja ya nchi zilizopo katika kizio cha kusini, huwa na hali ya joto kali katika maeneo mengi ikilinganishwa na miezi mingine.

“Hapa nchini, vipindi vya jua la utosi vinafikia kilele kati ya mwishoni mwa mwezi Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa).

“Jua la utosi huambatana na hali ya Joto kali kwa sababu kipindi hicho ndipo uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine,” imeeleza Taarifa hiyo na kiuongeza kuwa;

“Nyakati za usiku pia kunaonekana kuwa na hali ya joto kutokana na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha unyevunyevu angani kinachofika asilimia themanini na zaidi kwa baadhi ya maeneo.

“Unyevunyevu huo hutunza hali ya joto litokanalo na mionzi ya jua na hivyo kuleta hali ya fukuto.

“Katika kipindi hiki cha mwezi Disemba, 2020 upungufu wa mvua unatarajiwa kujitokeza katika baadhi ya maeneo yanayopata mvua za Vuli (ukanda wa ziwa Viktoria, nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na pwani ya kaskazini).

“Hali hii inatarajiwa kuendelea kusababisha uwepo wa hali ya joto katika maeneo hayo. Hata hivyo, hali ya joto inatarajiwa kupungua kidogo katika kipindi cha mwezi Januari, 2021 kutokana na mvua zinazotarajiwa katika baadhi ya maeneo,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha,imeongeza kuwa, vipindi hivi vya joto vinatarajiwa kuendelea kuongezeka katika mwezi Februari 2021 wakati jua litakapokuwa la utosi hapa nchini.

“Baada ya kipindi hicho hali ya joto inatarajiwa kuanza kupungua hasa kuelekea mwezi Machi ambapo mtawanyiko wa mvua unatarajiwa kuongezeka katika maeneo yanayopata mvua za msimu na kuanza kwa msimu wa mvua za masika.

“Taarifa za mwenendo wa joto, zinaendelea kutolewa katika utabiri wa kila siku na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, hivyo tunatoa wito kwa wananchi kuendelea kufuatilia taarifa hizo na kuchukua hatua stahiki kila inapobidi,”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles