Kiongozi wa Tigray Debretsion Gebremichael ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba mji wa Mekelle unashambuliwa vikali kwa mizinga.
Katika tamko lake serikali ya jimbo la Tigray limetoa wito kwa wote wenye dhamira ya kweli, ikiwa pamoja na jumuya ya kimataifa kulaani mashambulio ya mizinga na ya ndege pamoja na mauaji ya halaiki yanayofanyika.
Mwanadiplomasia mmoja aliyewasiliana moja kwa moja na wakaazi wa mji huo pamoja na kiongozi wa jeshi la jimbo la Tigray amesema hayo. Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo milipuko ilisikika kaskazini mwa mji wa Mekelle. Mwanadiplomasia mwingine amethibitisha kuwa majeshi ya serikali kuu yameanza kuushambulia mji wa Mekelle.
Msemaji wa waziri mkuu wa Ethiopia amesema majeshi ya serikali kuu hayakupewa jukumu la kuupiga mabomu mji wa Mekelle na wakaazi wake. Msemaji huyo Billene Seyoum ameeleza kuwa Mekelle ni mji muhimu wa Ethiopia na kwamba juhudi za kuwafikisha wahalifu wachache mbele ya sheria hazitamaanisha kuupiga mabomu mji huo kiholela kama inavyodawiwa na viongozi wa jeshi la Tigray la TPLF na waendesha propaganda wao. Msemaji huyo amehakikisha kwamba usalama wa wananchi wa Ethiopia katika mji wa Mekelle na katika jimbo lote la Tigray utaendelea kupewa kipaumbele na serikali kuu ya Ethiopia.