29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi wa dini waombwa kuongeza elimu ya masuala ya Ukimwi

Na MWANDISHI WETU,KILIMANJARO

Kueleekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duaniani Deseba mosi, Viongozi wa dini wameombwa kuongeza elimu ya masuala ya Ukimwi mbali na ile ya kiroho.

Wito huo umetolewa leo Novemba 28, na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko wakati akizungumza kwenye kwenye Kongamano la vijana, lililokutanisha vijana wa vyuo vya elimu ya juu kutoka mikoa mbalimbali na Viongozi wa dini lengo likiwa ni kutathmini mwitikio wa kitaifa wa Ukimwi katika kundi la vijana.

Kongaano hilo ni muendelezo wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani ambayo kitaifa yanafanyikia mkoani Kilimanjaro.

Dk. Maboko amesema kuwa kuwa kundi la vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 ndilo linaloongoza kwa maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 40, ambapo asilimia 80 yake ni vijana wa kike, hatua ambayo amewaomba viongozi wa dini kuwa na elimu ya Ukimwi nje ya masuala ya kiroho ili kuweza kudhibiti maambukizi mapya ya VVU hapa nchini.

“Wakati hapa vijana wanatoa michango yao niliangalia kama kuna tafiti ambazo zimefanyika hapa nchini zinazoonyesha ni miaka gani vijana ndio wanaanza ngono na nimeshtuka kukuta kumbe kuna tafiti 10 zimefanyika na tafiti zote zinaonyesha vijana wa umri wa miaka 10-19 wanaoanza ngono wa umri huo ni asilimia 20-70.

“Tafiti hizo zimebainisha kuwa kati ya asilimia 14-70.5 ya vijana hao wanawapenzi zaidi ya mmoja, ambapo wanaojua na kutumia Kondomu ni asilimia 50, hivyo viongozi wa dini Taasisi mbalimbali kwa kushirikiana na Tacaids tunatakiwa kuwekeza zaidi katika kundi hilo kwa kuandaa elimu za Ukimwi, kukaa karibu nao pamoja na kuwasikiliza ili kuweza kupunguza kudhibiti maambukizi mapya ya VVU kwa vijana.

“Viongozi wetu wa dini wakati nyinyi mkiendelea kuiasa jamii iishi kwa kufuata maagizo ya dini na sisi pia kama Serikali tunaomba mtuelewe tunapoelimisha na kuhamasisha matumizi sahihi na endelevu ya kondomu tunataka nchi nzima kondomu iwe inapatikana ili wale ambao hawawezi kabisa kabisa kuacha hata baada ya kuhubiriwa na viongozi wao wa kidini basi watumie kinga,” amesema  Dk. Maboko.

Upande wao, Vijana wamewaomba wazazi na walezi kuwa karibu nao na kuwafanya marafiki, ikiwa ni pamoja na kutenga muda na kuzungumza nao hatua ambayo itawawezesha kuwa huru kuzungumzia mwenendo mzima wa maisha yao ikiwa ni pamoja na kupata taarifa sahihi za kujikinga na maambukizi mapya ya Virusi vya UKimwi.

Josephine Mbise kutoka Mtandao wa Vijana wanaoishi na VVU wa (NY+PLUS) amesema kuwa wazazi na walezi wamekuwa muda mwingi wakiutumia kutafuta riziki na kuhakikisha mtoto, anaenda shule, anakula vizuri na kulala mahali pazuri lakini wanasahahu kipengele cha kuwa karibu na vijana na kuzungumza nao kwa uwazi na kujadiliana nao masuala yao ya kiafya ikiwa ni pamoja na kujikinga na ngono isiyosalama.

Mbise amesema kwa wazazi na walezi kutokufanya hivyo kunachochea vijana na kujiingiza katika ngono katika umri mdogo na kupata magonjwa ya ngono pamoja na maambukizi ya VVU.

Amebainisha kuwa wazazi na walezi wanayo nafasi kubwa ya kuwawezesha vijana kutimiza malengo yao hata kwa vijana wanaoishi na VVU kwa kuwa, kuwa na VVU siyo mwisho wa maisha hivyo kongamano hilo ni fursa nzuri ya viongozi wa Serikali pamoja na viongozi wa dini kufikisha ujumbe huo kwa wazazi na walezi.

“Tunawaomba viongozi wa dini, mnanafasi kubwa sana, tusaidieni kuzungumza na wazazi wetu, muwaeleze tunapenda wakae na sisi waongee na sisi wawe wazi kwetu ili na sisi tuwe wazazi wa kesho na walezi bora.

“Kwa kufanya hivyo itasaidia kupunguza maambukizi mapya ya VVU, kundi letu la vijana ndilo linaloongoza kwa kupata maambukizi zaidi,” amesema Mbise.

Amebainisha kuwa vijana wanatamani sana wazazi wao wawe mstari wa mbele katika kuwasimamia wale ambao wamekwisha ambukizwa VVU kuwafuatilia ili waweze kutumia dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI (VVU) kwa usahihi ili kuweza kufikia lengo la 95 tatu ambapo wanaoishi na VVU wanamchango mkubwa wa kufikia lengo iwapo watakuwa na ufuasi mzuri na endelevu wa dawa za ARV.

Awali, akizungumzia kongamano hilo, Mratibu wa vijana na makundi maalum wa Tacaids, Dk. William Kafura amesema lengo la kongamano hilo ni kujadili changamoto za vijana na wajibu wa viongozi wa dini katika kudhibiti maambukizi ya VVU kwa kundi la vijana.

“Kongamano hili limelenga katika kuleta matokeo chanya katika utekelezaji wa afua mbalimbali za kudhibiti maambukizi mapya ya VVU katika kundi la vijana ambapo kupitia kongamano hili imekua ni fursa nzuri ya kuwasikia vijana, kuwasikia viongozi wa kidini pamoja na kutathmini mwitikio wa kitaifa na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla,amesema Dk. Kafura.

Aidha, amewataka vijana wa mkoanikim Kilimanjaro na mikoa ya jirani kutembelea maonyesho ya Maadhimisho hayo yanayofanyikia viwanja vya Shule ya Msingi Mandela kata ya Pasua mkoani hapa, ambapo katika maonyesho hayo kuna Kijiji cha Vijana ambapo elimu ya VVU na Ukimwi, huduma za kupima huduma za kuona kazi za wajasiriamali vijana, ushauri nasaha vinatolewa bila malipo kila siku hadi ifikapo kilele cha maadhimisho Desemba 1.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles