Na AVELINE KITOMARY
DAKTARI bingwa wa afya ya akili na uraibu wa dawa za kulevya wa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, Dk. Sostesjofu Mongu ameeleza unywaji wa pombe unaofaa kiafya ili kuepukana kuwa tegemezi na magonjwa yasiyoambukiza.
Kwa mujibu daktari huyo kiafya mwanamke anashauriwa kunywa chupa saba za bia kwa wiki moja huku mwanaume akishauriwa kunywa chupa 14 za bia kwa wiki moja.
Katika mahojiano maalumu na MTANZANIA yaliyolenga athari ya matumizi ya pombe, Dar es Salaam jana, Dk Mongu alisema pombe ni kilevi chochote ambacho mtu akinywa kinabadilisha mtazamo ,hisia na mawazo ya mnywaji.
“Kiwango cha ulevi wa pombe inategemea na ujazo wa pombe kuna za mill 100, zingine 250 hadi 500 kwahiyo kila pombe inaujazo wake na kiwango cha ‘alcohol’ inategemea na aina ya pombe.
“Tunasema kuna aina ya unywaji ambao unaboresha afya huu ni unywaji usiokuwa na madhara kwa lugha nyepesi tunaita unywaji wenye afya ambao unaboresha mzunguko wa damu.
“Kwa mwanamke kwa wiki moja anatakiwa asinywe zaidi ya chupa saba za bia na kwa mtoko mmoja anatakiwa kunywa chupa moja hadi tatu tu na kwa mwanaume kwa wiki asizidi chupa 14 na kwa mtoko mmoja anatakiwa kunywa chupa mmoja mpaka nne huo ndio unywaji salama kwa afya,”alibainisha.
Alisema unywaji wenye madhara ni ule ambao mtu akinywa siku ya pili anajikuta yuko polisi kwa kufanya uharibifu au hospitali kupata matibabu.
“Utakuta mtu anakunywa pombe hadi anajikuta anashindwa kufanya majukumu yako kwasababu alikunywa jana ametapika anaamka anaumwa na unashindwa kwenda kazi ,unywaji wa aina hiyo tunasema huo ni unywaji wenye madhara.
Alieleza aina nyingine ya tatu ya unywaji ni unywaji hatari ambapo husababisha madhara katika afya ya muhusika.
“Huu ni unywaji ambao kwa idadi ya pombe unazokunywa inapelekea madhara kiafya unakunywa pombe lakini tayari umeshakuwa na tatizo la kiafya ,unakunywa pombe wakati tayari umeshapata magonjwa ya moyo,stroke,ugonjwa wa ini ,na kansa,”alifafanua.
Alisema hatua ya nne, ni utegemezi wa pombe kwamba mtu hawezi kufanya kitu chochote hadi apate pombe.
“Umeamka asubuhi huwezi kupata nguvu ya kupiga hata mswaki ,kwenda kazini lazima uhitaji pombe ,ukifikia kiwango cha utegemezi wa pombe maana yake hata kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii inakuwa shida huwezi kwenda kwenye msiba,harusi,shughuli za uzalishaji kwasababu unakuwa umelewa muda wote.
“Mwisho wa siku kama huwezi kuacha pombe unapata magonjwa yasiyoambukiza na kwasababu huwezi kuacha pombe na maradhi unayo unapunguza muda wa kuishi na mwisho wa siku ni kifo,”alisema.
Alisema ni muhimu jamii kuelewa unywaji gani ambao hauna hatari na bila kupata maradhi .
“Unywaji wa pombe kupindukia unaathari katika familia kwasababu kama ni mzazi anashindwa kuhudumia familia na kusahau majukumu yote hivyo familia itateseka hata akipata kazi anashindwa kufanya kwasababu ameshakuwa tegemezi.
Alibainisha kuwa asilimia 40 ya magonjwa yasiyoambukiza yanasababishwa na madhara ya matumizi mabaya ya pombe.
“ Ukienda MOI utakuta kuna majeruhi ambao chanzo ni ulevi,Jamii sehemu kubwa inahitaji elimu juu ya matumizi ya pombe serikali kupitia wizara ya afya ijaribu kuweka mtaala wa matumizi ya vinywaji kama pombe, dawa za kulevya iwe inafundishwa shuleni na tupate wataalamu wa kutosha katika kuelimisha jamii ,”alishairi Dk Mungo.