Mwandishi Wetu- Songea
WAGONJWA watano sawa na asilimia 2.4, kati watu 203 waliobainika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu walioibuliwa kupitia kampeni ya uelimishaji na uibuaji ya ugonjwa huo inayofanywa na Hospitali ya Wilaya Tunduru mkoani Ruvuma, wamepoteza maisha kati ya Julai hadi Septemba, mwaka huu.
Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Wilaya ya Tunduru, Dk. Mkasange Kihongole alisema hayo jana, wakati wa kampeni ya uelimishaji na upimaji wa ugonjwa huo kwa watu na makundi mbalimbali, ikiwemo mama lishe na waendesha bodaboda.
Alisema idadi ya vifo, ni ongezeko la mtu mmoja ikilinganisha na watu wanne walipoteza maisha mwaka jana kati ya 145 waliokutwa na maradhi hayo.
Alisema kwa upande wa watoto walio chini ya umri wa miaka 15 waliokutwa na ugonjwa huo mwaka 2020, walikuwa 75 sawa na asilimia 36.9 na mwaka jana waliokutwa n 25 sawa na silimia 17.2.
Alisema mwaka jana, wahisiwa(waliofanyiwa uchunguzi)wa ugonjwa watu 1,654 waliokutwa na vimelea vya ugonjwa huo, ni 145 na hadi kufikia Septemba, mwaka huu wahisiwa walikuwa 4,073 kati yao 203 walikutwa na maambukizi.
Baadhi ya wananchi, waliishukuru Serikali kwa mpango wake wa kufanya kampeni ya kuibua wahisiwa wa ugonjwa wa kifua kikuu ambao umesaidia sana kuokoa maisha ya wananchi wengi.
Walisema mpango huo, umewezesha kuibuliwa kwa wananchi wengi wenye ugonjwa huo majumbani ambao hawakufahamu maradhi yanayowasumbua kwa muda mrefu.
Juma Makumbusya, alisema kampeni itaokoa maisha ya baadhi ya watu wanaogua ugonjwa huo kwa muda mrefu hasa katika vijiji vilivyopo mpakani mwa wilaya ya Tunduru na nchi jirani ya Msumbiji
Juma Makumbusya mkazi wa Kijiji cha Kitanda, alisema, elimu inayotolewa na kitengo cha kifua kikuu imewezesha wazazi kutambua dalili kwa watoto wadogo, ikilinganishwa na miaka ya nyuma.