Samwel Mwanga-Maswa
WALIMU na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwatigi wilayani Maswa Mkoa wa Simiyu, wako hatarini kuambukizwa magonjwa ya mlipuko kutokana na kujisaidia vichakani, baada ya shule kukosa vyoo kwa miezi 10.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea shule hiyo jana Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo,Martin Paul alisema tatizo hilo limekuwa la muda mrefu, licha ya kutoa taarifa kwa Serikali ya kijiji,hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.
Alisema walimu wanane na wanafunzi 340, wanalazimika kujisaidia vichakani kutokana na choo kilichokuwepo kujaa,kisha kubomoka hali ambayo inaweza kusababisha kupata magonjwa ya kuhara na kipindupindu.
“Walimu walioko shuleni ni wanane,tuna wanafunzi 340, hatuna choo kilichokuwepo kimejaa na kubomoka,tunajisaidia vichakani na ukizingatia shule hii haina hata nyumba ya mwalimu tuko hatarini kupata magonjwa ya mlipuko,”alisema.
Alisema inafikia hatua kwa walimu na wanafunzi ambao hawapendi kujisaidia vichakani kuomba ruhusa kwenda kujisaidia mjini Malampaka umbali wa kilomita 8 kutoka shuleni, hivyo kusababisha wasihudhurie vipindi kwa ufasaha.
Mwanafunzi,Marry Edward alisema vyoo vilijengwa tangu shule ilipoanzishwa mwaka 1979, vimekuwa havifanyiwi ukarabati wala kujengwa vipya jambo ambalo limesababisha kuchakaa kiasi kwamba havifai kutumika baada ya kubomoka.
“Ukiviona vyoo vyetu utashangaa, kuta zimebomoka na sakafu imeharibika,vingi vinatiririsha maji machafu pembeni na kusababisha vigeuke kuwa mazalia ya nzi, mende na wadudu wengine wanaotambaa”alisema .
Alisema ni vizuri idara ya elimu ikachukua uamuzi wa kuifunga shule hiyo kutokana na hali kuwa mbaya.
Diwani Mteule wa Kata ya Malampaka,Mashala Deus alisema tayari ametoa taarifa kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo na hivyo kuhaidiwa kupatiwa fedha kwa ajili ya ujenzi.
Kaimu Ofisa Elimu ya Wilaya ya Maswa,Bakari Juma alikiri kuwepo tatizo hilo na kusema analifuatilia kunusu afya za walimu na wanafunzi.