Ramadhani Hassan -Dodoma
SERIKALI imesema maandalizi ya kupishwa Rais mteule Dk. John Magufuli yamekamilika.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini,Msemaji Mkuu wa Serikali,Dk.Hassan Abassi alisema Dk. Magufuli ataapishwa Alhamisi Uwanja wa Jamhuri na kushuhudiwa na wageni mbalimbali kutoka nje na ndani ya nchi wamethibitisha kushiriki.
“Nitoe taratibu za Serikali,baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kukamilisha taratibu zao, mgombea wa urais kukabidhiwa cheti chake, ataapishwa Uwanja wa Jamhuri hapa Dodoma,”alisema.
Alisema Serikali itaendelea kutoa taratibu za wageni ambao watashiriki, ambapo mpaka sasa wamepokea salamu kutoka zaidi ya nchi 10, ikiwemo Rais wa China, XI Jingping.
Alisema salamu zingine ni Uganda,Kenya,Afrika Kusini,Burundi na Zimbambwe.
Alisema burudani mbalimbali zitakuwepo katika sherehe hizo kama za ngoma za asili,wasanii muziki wa kizazi kipya.
“Niwaombe wananchi wa Dodoma na mikoa ya jirani tunaomba sana ifikapo saa moja kila mmoja awe amefika,”alisema.