Mwandishi Maalumu, Arusha
SERIKALI imezindua mfumo mpya wa ufuatiliaji na utekelezaji wa mapendekezo ya hoja za ukaguzi (GARI-ITS) kwa Wakala wa Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma ili kuimarisha udhibiti na usimamizi wa fedha za umma .
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya mfumo jijini Arusha jana, Mkurugenzi wa Ubinafsishaji, Ufuatiliaji na Tathmini Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mohamed Nyasama aliyemwakilisha Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka alisema mafunzo ya mfumo huo kwa Wakaguzi wa Ndani wa Wakala wa serikali, taasisi na mashirika ya umma nchini katika Chuo cha Uhasibu Arusha.
Alisema mfumo unatarajiwa kuimarisha mifumo ya ndani ya udhibiti na usimamizi madhubuti ya fedha za umma katika wakala za serikali,taasisi na mashirika ya umma.
“Ofisi yangu ilibaini uwepo wa wingi wa hoja za ukaguzi hasa kutoka ukaguzi wa ndani, ukaguzi wa nje (CAG) na maagizo yanayotolewa na Kamati za Kudumu za Bunge,” alisema Nyasama aliyesoma hotuba ya Msajili wa Hazina.
Aliwataka watendaji wakuu wa wakala wa Serikali na mashirika ya umma kusimamia vema na kudhibiti fedha za umma.
Alisema serikali inataka kunufaika na utekelezaji wake uliofanyika katika taasisi ,Wakala na mashirika ya umma ili kuchangia ukuaji wa mapato na hivyo kutoka huduma bora kwa wananchi .
Mkaguzi Mkuu wa Ndani kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Magdalena Kirumba alisema wakaguzi wa ndani wamejipanga kutumia mfumo huo, kwani utaongeza ufanisi wa kazi.
Alisema mfumo huo utasaidia taasisi kuwasilisha taarifa za ukaguzi za kila robo mwaka na taarifa za mwaka kwa wakati.
Wakaguzi wa ndani 472 kutoka taasisi za umma na mashirika ya umma 236 watajengewa uwezo juu ya mfumo huo mpya.