Na JANETH MUSHI- ARUSHA
MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro ameonya baadhi ya watu waliojipanga kufanya vurugu kipindi hicho na kuwa jeshi hilo limejipanga kuwadhibiti na kuwachukulia hatua za kisheria.
Aliwahakikishia wananchi kuwa uchaguzi utafanyika katika hali ya amani na utulivu bila kuwa na tatizo lolote, huku jeshi hilo likijipanga kusimamia haki na amani.
IGP Sirro aliyasema hayo jijini Arusha jana, wakati akizungumza na askari 710 wakiwemo polisi,Uhamiaji,Magereza na mgambo.
Alisema wamepata taarifa kuna vikundi
vya watu wachache wanaotaka kuleta fujo na kusababisha uvunjifu wa amani katika kipindi cha uchaguzi huo mkuu wa Oktoba 28,mwaka huu.
“Tunaendelea vizuri na tunaona kampeni ndiyo zinakaribia kumalizika. Tumejipanga vizuri na tutafanya kazi kwa pamoja,niwahakikishie wana Arusha tutafanya kazi kwa kusimamia amani na haki ili kuhakikisha tunapata viongozi kwa ajili maendeleo ya mkoa wetu na nchi yetu kwa ujumla.
“Niwaombe nina taarifa kuna vikundi vya watu wachache wanataka kuleta uvunjifu wa amani,wasijaribu kufanya hivyo kwani watajiingiza kufanya makosa na
tutawashughulikia kabla ya siku yenyewe,” Alisema siku za nyuma katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Arusha yalikuwa na vurugu kipindi cha chaguzi na kuwa jeshi hilo limejipanga kuhakikisha linadhibiti hali hiyo
isijitokeze.
“Najua Arusha miaka ya nyuma ilitokea
tokea fujo ni mahali ambapo tumepanga kuweka askari wa kutosha wa kiraia,operesheni wote kuhakikisha kwamba arusha inakuwa shwari,”alisema na kuongeza
“Niombe wananchi wakisikia kuna mtu anataka kufanya uvunjifu wa amani watoe taarifa ili washughulikiwe,askari peke yake hawezi kusimamia amani na utulivu tushirikiane kwa pamoja,”alisema.