32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Malasusa awataka wanawake wasikubali kunyanganywa haki ya kupiga kura

Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

ASKOFU wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa, amewataka Watanzani hususan wanawake kutokukubali kupokonywa haki yao ya kikatiba ya kupiga kura.

Dk. Malasusa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua semina ya wake wa maaskofu wa makanisa wanachama wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania inayolenga kuwajengea uwezo.

Alisema hakuna haja kwa mtu kumfanyia maamuzi mtu mwingine kwa kumlaghai na fedha au zawadi nyingine, jambo ambalo linaondoa haki ya msingi huku akisisitiza kuendelea kudumisha amani.

“Mwanamke ana uwezo wa kubadilisha hali ya sasa ilivyo, hivyo hatuna sababu ya mtu mwingine kukupigia kura wewe kwa kukulaghai na chumvi au hela, hivyo ni muda kwa akina mama kuamka na kufanya maamuzi kwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huu.

“Lakini pia niwatake akina mama mkawe mawakala wazuri wa kutafuta amani, kwani amani ndiyo mtaji mzuri wa maendeleo, hivyo mkawe nguzo muhimu katika kuhimiza amani hususan katika kipindi hiki cha uchaguzi,” alisema Dk. Malasusa.

Aidha aliwataka wote ambao wameumizwa katika kipindi hiki cha kampeni kumuomba Mungu ampe amani katika kipindi hiki.

“Amani ni kitu cha lazima, mahala ambapo hakuna amani wahanga wakubwa wamekuwa ni wanawake na watoto, hiki ni kipindi cha kuomba sana kama kuna yeyote ambaye ameumizwa katika kipindi cha kampeni basi nikumuomba Mungu ampe amani katika kipindi hiki.

“Ni lazima tuwaambie watu wavumiliane, kwani katika Tanzania tunaamini kwamba amani ndiyo mtaji wa maendeleo na fedha ni matokeo, hivyo mtambue kuwa kila kura ina nguvu yake hivyo akina mama msiuze utu wenu,”alisema Dk. Malasusa.

Kwa upande wake, Esther Mhagachi kutoka Jumuhiya ya Kikrito Tanzania, Idara ya Maendeleo ya Wanawake, Watoto na Jinsia, alisema lengo la semina hilo ni kuwajengea uwezo wanawake ambao nao watapeleka mafunzo hao kwenye maeneo yao kwa lengo la kuilinda jamii na madhara ya ukatili wa kijinsia.

“Tunawajengea uwezo katuika ukatili wa kijinsia kutokana kwmaba kumekuwapo na ongezeko kubwa la vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto na changamoto kubwa inakuja kwamba siyo wote wana elimu ya kukabiliana na vitendo hivyo.

“Hivyo tunaamini kuwa elimu hii ikiwamo ile ya kushiriki katika uchaguzi mkuu bila kukubali kulaghaiwa itawafikia wanawake wengi zaidi na kuwa na jamii yenye amani na upendo,” alisema Esther.

Aidha, aliwataka wazazi kuwa makini na malezi ya watoto wao kama ambavyo wamekuwa wakizingatia mahitaji yao muhimu hatua aliyosema kwamba itasaidia kupunguza vitendo vya ukatili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles