Na AVELINE KITOMARY
USINGIZI ni hali ambayo mifumo ya mwili inafanya kazi kwa viwango vya chini kidogo hivyo kupata muda wa kuweza kujisafisha na kutoa sumu kutokana na shughuli nyingi ambazo mtu anazifanya akiwa macho.
Binadamu anapofanya kazi mbalimbali wakati wa usingizi ndio muda mwili unajisafisha na kujiweka katika hali ambayo huwa tayari kuanza siku nyingine hivyo usingizi ni muhimu kiafya.
Wataalam wa afya mara nyingi wanashauri kuwa ili mtu aweze kulala vizuri basi inambidi alale saa zisizopungua sita hadi nane.
Kwa watoto na vijana wanaokua na kwa watu wazima wakiwamo Wazee mahitaji ya usingizi yanaweza yakawa tofauti lakini kwa ujumla saa sita hadi nane yanahitajika kulala katika siku moja.
Lemery Mchome ni Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo, Uti wa mgongo na Mishipa ya fahamu kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa(MOI) katika makala hii ya afya ya Jamii anaeleza matatizo ya usingizi ambayo ni sababu za mtu kukosa au kuwa na usingizi mwingi.
MATATIZO YA USINGIZI
Dk. Lemery anasema matatizo ya usingizi yako ya aina nyingi katika jamii ambapo kwa kawaida kuanzia asilimia 15 hadi 20 ya watu wazima wanakuwa na matatizo ya usingizi.
Anasema matatizo hayo yamegawanyika katika sehemu mbili ambayo ni kushindwa kupata usingizi na kulala kupita kiasi.
“Hapa mtu unaweza ukapanda kitandani unakaa muda mrefu kabla ya kupata usingizi na hata ukipata baada ya muda mchache usingizi ukipotea huwezi kuupata tena.
“Na unaweza kukuta mtu anasema anapata usingizi lakini anakuwa kama vile hajalala kutokana na kuwa anasikia kila kinachoendelea hivyo unakuwa kama usingizi wajuujuu tu.
“Pia kunatatizo lingine la kulala muda mrefu hata mtu akiamshwa bado anausingizi mzito yaani unaweza kunyanyua godoro ukamuweka chini asisikie mpaka labda aamke kuna aina hii ya matatizo ya usingizi,”anabainisha Dk. Lemery.
Anaongeza; “ Haitakiwi mtu kulala saa 12 hadi 14 na kuendelea hilo ni tatizo na linahitaji matibabu pia.
Anaeleza kuwa kunatatizo lingine la mtu kukosa pumzi anapolala hivyo kufanya kushtuka kutoka usingizini na kutafuta hewa (Sleep upning).
“Na kuna ile maarufu kwa watu wengi utakuta mtu umelala huku anatembea anaweza akatoka chumbani, akatoka nje akazunguka nyumba lakini huyu mtu amelala ukimwasha anashtuka hii inafahamika kama (sleep walking) nayo pia ni tatizo,”anaeleza Dk. Lemery.
MSONGO WA MAWAZO, MAZINGIRA SABABU
Kwa mujibu wa, Dk. Lemery msongo wa mawazo na shughuli za kila siku huweza kuwa sababu za mtu kupata matatizo ya usingizi.
“Tatizo la kwanza ni mawazo (cycological stress) inaweza kusababishwa na kazi unazofanya au hata mahusiano vinaweza vikawa kwa njia moja au nyingine zina athari katika mfumo wa mawazo kwahiyo mtu anakosa usingizi.
“Huenda mawazo hayo hayana majibu au unasubiria mtihani ambao hauji kuna vitu vingi ambavyo vinaweza kusababisha ukawa na mawazo mengi hii inaweza kuleta shida ya usingizi,”anaeleza.
Aidha, Dk. Lemery anabainisha sababu nyingine kuwa ni mazingira duni ya kulala.
“Unalala kwenye watu wengi wakati wewe unapata usingizi wao ndo kwanza wanaanza kupiga kelele au wanaanza kufanya shughuli zingine haya ni mazingira duni lakini pia taa zenye mwanga mkali au unalala kwenye jua kuna mwanga huwezi kupata usingizi.
“Usafi wa chumba unacholala, nguo unazotumia zikiwa hazina usafi zinaweza kuchangia kutokupata usingizi wa kutosha,”anafafanua.
Dk. Lemery anaeleza kuwa kutokuwa na ratiba maalum ya kulala huweza kuwa sababu za kutokupata usingizi wa kutosha.
“Kama muda wako wa kulala ni saa tatu au nne usiku lazima wakati huo uwe umepanda kitandani hii mara nyingi inakuwa ni tatizo kubwa na inasababisha watu kutokupata usingizi.
“Lakini kuna watu wengine ambao wao hawapatagi usingizi kutokana na saa chache kabla ya kulala mfano mtu anaangali mechi ya mpira timu yake ikashinda akashangilia sana akawa na furaha alafu saa hiyo anatakiwa kulala mtu kama huyo hawezi kupata usingizi.
“Atakuwa na shida ya kupata usingizi pale atakapokuwa amekwenda kulala au mwanafunzi amepata matokeo ya kufaulu na ni saa nne usiku huyu atapata matatizo ya kulala,”anasema.
Anafafanua zaidi kuwa, ufanyaji mazoezi muda mfupi kabla ya kulala huweza kumfanya mtu akashindwa kupata usingizi kwa wakati unaotakiwa.
Hali anayosema kuwa hutokea kutokana na mfumo wa usingizi kuathiriwa.
MATUMIZI YA SIMU MUDA WA KULALA HAIFAI
Kwa mujibu wa, Dk. Lemery tatizo la usingizi linatibika kulingana na aina ya tatizo hivyo ni bora muhusika akamuona mtaaalamu wa afya.
“Wakijua tatizo lako wataalam watakushauri ufanye mabadiliko yapi ili uweze kupata usingizi au kama imeshindakana inabidi kutumia dawa watakuambi ni za dawa za aina gani, kwa muda gani na kwa kiwango gani.
“Usijichukulie matibabu mwenyewe kwa sababu unaweza ukafanya hali kuwa mbaya zaidi,” hapa anasisitiza.
Anaeleza kuwa katika matibabu pia mabadiliko ya tabia yatahusishwa kama vile utaratibu wa muda wa kulala.
“Matumizi ya simu inaweza kuwa sababu mmoja wapo ya mtu kutokulala muda ambao ameupanga utakuta mtu anapitiwa kutokana na kuchati muda mrefu na kuathiri muda wa usingizi hivyo ni bora mtu anapolala anaweka simu mbali ili kulala kwa wakati.
“Vitu vingine mfano kutumia kompyuta mpakato kitandani na unataka upate usingizi itakuwa sio rahisi au kuangaliaa luninga ukiwa kitandani na unaangali mpira lakini unajua kuwa unatakiwa kulala hilo linaweza kuwa tatizo kulala kwa muda unaotakiwa,”anabainisha.
EPUKA VYAKULA NA VINYWAJI HIVI
Dk. Lemery anasema ni lazima wakati wa jioni watu kukwepa matumizi ya vyakula au vinywaji ambavyo vinachangamsha mwili.
“Mfano unakunywa kahawa nyingi halafu unataka kupata usingizi inaweza kuleta shida, asilimia 90 ya watu wakinywa kahawa mapigo ya moyo yanaenda mbio, wanatoa jasho na wanakuwa wako macho kwa muda mrefu basi hii kahawa na vyakula vya kafeni viepukwe wakati unakwenda kulala,” anasema.
Anakitaja kitu kingine cha kuepukwa kuwa ni pamoja na kufanya mazoezi muda mfupi kabla ya kulala ili mifumo ya mwili ijiandae kwa usingizi.
“Mazoezi ni muhimu na tuyafanye kwa muda maalum katika wiki lakini mazoezi yasiingiliane na ratiba ya usingizi.
“Tenganisha mazoezi na muda wa kulala angalau saa nne hadi nane ndipo ratiba ya kulala ifiki hii ni muhimu,epuka kufanya mazoezi mazito fanya mepesi mepesi, pia unapozidi kuwa mtu mzima hadi miaka 60 matatizo ya usingizi yanaongezeka zaidi ukawa hupati usingizi au unalala sana.
“Haya matatizo ya watu wazima ni tofauti na yanatakiwa kutibiwa kwa namna ambayo ni tofauti kwa ushauri kwa watu kamahawa wakiwa na matatizo wafatilie kwa muda na kuwaona wataalamu wapate ushauri ili waweze kusaidiwa,”anashauri Dk. Lemery.
USINGIZI HUSAIDIA KUTUNZA KUMBUKUMBU
Dk. Lemery anasema wakati mtu akiwa amelala mifumo ya mwili kama ubongo, mifumo ya fahamu, mifumo ya upumuaji, mifumo ya moyo na usukumaji wa damu, mifumo ya chakula,haja kubwa, mkojo, mifupa, misuli na mifumo ya kinga ya mwili huanza kujiandaa kwa siku nyingine.
Kwa mujibu wa daktari huyo usingizi kwenye mfumo wa fahamu husaidia kutunza kumbukumbu vizuri na kuboresha umakini.
“Lakini pia kwenye mifumo ya mifupa na misuli inaondoa sumu ambayo imekuwa ikijirundika wakati unafanya shughuli mbalimbali.
“Na kwa mifumo ya chakula, kinasukumwa vizuri wakati ukiwa umelala na chakula kinanyonywa kile kilicho kwenye utumbo vile virutubisho vyote vinachukuliwa wakati huo.
“Lakini pia na mifumo ya homoni ya mwili inajitengeneza na kujiweka vizuri kwa ajili ya kuanza siku nyingine na kuwezesha mwili kufanya vile inavyotakiwa,”anabainisha Dk. Lemery.
Anasema kwa wakati huo mifumo ya kinga mwili inapata muda wa kujiweka sawa kwani kipindi hicho sumu zinaondolewa mwilini na kingamwili kutengenezwa.
“Mfumo wa kinga unapata muda mzuri wa kuweza kujiandaa kwa ajili ya kulinda mwili kwahiyo unaona wakati huo mifumo yote inajiweka tayari kwa ajili ya kujisafisha na kuanza kazi mpya siku inayofuatia.
UKUAJI MZURI KWA WATOTO
Dk. Lemery anasema baadhi ya tafiti zinaonesha kwamba watoto wakilala wanaongeza homoni za ukuaji (growth hormon) .
“Hii inazalishwa kwa kiwango kikubwa kipindi wakiwa wamelala kwenye usingizi mzito na hii inasaidia watoto kukua vizuri ukilinganisha na watoto kulala masaa machache chini ya masaa sita.
“Usingizi unasaidia sana kwenye ukuaji wa watoto kwenye kiwango cha kimo kinachohitajika na pia kuwa na uzito ambao unahitaji.
“Kwa watoto ambao wanasoma shule kwa siku nzima wanakuwa wamesoma vitu vingi vile vitu haviwezi kuwepo kama kumbukumbu kwa muda mfupi inabidi wakati wakiwa wamelala muda wa kutosha ndipo ubongo unafanya kazi taratibu ya kuchukua zile kumbukumbu na kuziweka sehemu ambapo zinakaa kwa muda mrefu na inakuwa rahisi kuzikumbuka,”anabainisha.