20.5 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Matumizi ya simu kitandani yanavyoathiri usingizi

Na  AVELINE  KITOMARY 

USINGIZI  ni hali ambayo mifumo ya mwili inafanya kazi kwa viwango vya chini kidogo hivyo  kupata muda wa kuweza kujisafisha na kutoa sumu kutokana  na shughuli nyingi ambazo mtu  anazifanya akiwa macho. 

Binadamu anapofanya kazi mbalimbali wakati wa usingizi ndio muda mwili unajisafisha na kujiweka katika hali ambayo huwa tayari kuanza siku nyingine hivyo usingizi ni muhimu kiafya. 

Wataalam wa afya mara nyingi wanashauri kuwa ili mtu aweze kulala vizuri basi inambidi alale saa zisizopungua sita hadi nane. 

Kwa watoto  na vijana wanaokua na  kwa watu wazima wakiwamo Wazee mahitaji ya usingizi  yanaweza yakawa tofauti lakini kwa ujumla saa sita hadi nane yanahitajika kulala katika siku moja. 

Lemery Mchome ni Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo, Uti wa mgongo na Mishipa ya fahamu kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa(MOI) katika makala hii ya afya ya Jamii anaeleza matatizo ya usingizi ambayo ni  sababu za mtu kukosa au kuwa na usingizi mwingi. 

MATATIZO YA USINGIZI

Dk. Lemery anasema matatizo ya usingizi  yako ya aina nyingi  katika jamii ambapo  kwa kawaida  kuanzia asilimia 15 hadi 20  ya watu wazima wanakuwa na  matatizo ya usingizi. 

Anasema matatizo hayo  yamegawanyika katika sehemu mbili  ambayo ni kushindwa kupata usingizi na kulala kupita kiasi.

“Hapa mtu unaweza  ukapanda kitandani  unakaa muda mrefu kabla ya kupata usingizi na hata ukipata  baada ya muda mchache usingizi ukipotea  huwezi kuupata tena. 

“Na unaweza kukuta mtu anasema anapata usingizi lakini anakuwa kama vile hajalala  kutokana na kuwa anasikia kila kinachoendelea hivyo unakuwa kama usingizi wajuujuu tu.

“Pia kunatatizo lingine la kulala muda mrefu hata mtu akiamshwa bado anausingizi mzito yaani   unaweza kunyanyua godoro  ukamuweka chini asisikie mpaka labda aamke kuna aina hii ya matatizo ya usingizi,”anabainisha Dk. Lemery.

Anaongeza;  “ Haitakiwi mtu kulala saa 12 hadi 14  na kuendelea hilo ni tatizo  na linahitaji matibabu pia.

Anaeleza kuwa kunatatizo lingine la mtu kukosa pumzi anapolala hivyo kufanya kushtuka kutoka usingizini na kutafuta hewa (Sleep upning). 

“Na kuna ile maarufu kwa watu wengi utakuta mtu umelala huku anatembea anaweza akatoka chumbani, akatoka nje akazunguka nyumba lakini huyu  mtu amelala ukimwasha anashtuka hii inafahamika kama (sleep walking) nayo pia ni tatizo,”anaeleza Dk. Lemery.

MSONGO WA MAWAZO, MAZINGIRA SABABU

Kwa mujibu wa, Dk. Lemery msongo wa mawazo na shughuli za kila siku huweza kuwa sababu za mtu kupata matatizo ya usingizi.

“Tatizo la kwanza ni mawazo (cycological stress) inaweza kusababishwa na kazi unazofanya au hata mahusiano vinaweza  vikawa kwa njia moja au nyingine zina athari  katika mfumo wa mawazo kwahiyo mtu anakosa usingizi. 

“Huenda mawazo hayo hayana majibu au unasubiria  mtihani ambao hauji kuna vitu vingi ambavyo vinaweza kusababisha ukawa na mawazo mengi hii inaweza kuleta shida ya usingizi,”anaeleza. 

Aidha, Dk. Lemery anabainisha sababu nyingine kuwa ni mazingira duni ya kulala.

“Unalala kwenye watu wengi wakati wewe unapata usingizi wao ndo kwanza wanaanza kupiga kelele  au  wanaanza kufanya shughuli zingine haya ni mazingira duni lakini  pia taa zenye mwanga mkali au unalala kwenye jua kuna mwanga huwezi kupata usingizi. 

“Usafi wa chumba unacholala, nguo unazotumia zikiwa hazina usafi zinaweza kuchangia kutokupata usingizi wa kutosha,”anafafanua. 

Dk. Lemery anaeleza kuwa kutokuwa na ratiba maalum ya kulala huweza kuwa sababu za kutokupata usingizi wa kutosha.

“Kama muda wako wa kulala ni saa tatu au nne usiku lazima wakati huo  uwe umepanda kitandani hii mara nyingi inakuwa ni tatizo kubwa na inasababisha watu  kutokupata usingizi.

“Lakini kuna watu wengine ambao wao hawapatagi usingizi kutokana na saa chache kabla ya kulala mfano mtu anaangali mechi ya mpira timu yake ikashinda akashangilia sana akawa na furaha alafu saa hiyo anatakiwa kulala mtu kama huyo hawezi kupata usingizi.

“Atakuwa na shida ya kupata usingizi pale atakapokuwa amekwenda kulala au  mwanafunzi amepata matokeo ya kufaulu na ni saa  nne usiku  huyu atapata matatizo ya kulala,”anasema.

Anafafanua zaidi kuwa, ufanyaji mazoezi muda mfupi kabla ya kulala huweza kumfanya mtu akashindwa kupata usingizi kwa wakati unaotakiwa.

Hali anayosema kuwa hutokea kutokana na mfumo wa usingizi kuathiriwa.  

MATUMIZI YA SIMU MUDA WA KULALA HAIFAI 

Kwa  mujibu wa, Dk. Lemery tatizo la usingizi linatibika kulingana na aina ya tatizo hivyo ni bora muhusika akamuona mtaaalamu wa afya.

“Wakijua tatizo lako wataalam watakushauri ufanye mabadiliko yapi ili uweze kupata usingizi au  kama imeshindakana  inabidi kutumia dawa watakuambi ni za dawa za aina gani, kwa muda gani na kwa kiwango gani. 

“Usijichukulie matibabu mwenyewe kwa sababu  unaweza ukafanya hali kuwa  mbaya zaidi,” hapa anasisitiza. 

Anaeleza kuwa katika matibabu pia mabadiliko ya tabia yatahusishwa kama vile utaratibu wa muda wa kulala.

“Matumizi ya simu inaweza kuwa sababu mmoja wapo ya mtu kutokulala muda ambao ameupanga utakuta mtu anapitiwa kutokana na kuchati muda mrefu na kuathiri muda wa usingizi hivyo ni bora mtu anapolala anaweka simu mbali ili kulala kwa wakati.

“Vitu vingine mfano kutumia kompyuta mpakato  kitandani na unataka upate usingizi itakuwa sio rahisi au kuangaliaa luninga  ukiwa kitandani na unaangali mpira lakini unajua kuwa unatakiwa kulala hilo linaweza kuwa tatizo kulala kwa muda unaotakiwa,”anabainisha.

EPUKA VYAKULA NA VINYWAJI HIVI 

Dk. Lemery anasema ni lazima wakati wa jioni watu kukwepa matumizi ya vyakula au vinywaji ambavyo vinachangamsha mwili.

“Mfano unakunywa kahawa nyingi halafu unataka kupata usingizi inaweza kuleta shida, asilimia 90 ya watu wakinywa kahawa mapigo ya moyo yanaenda mbio, wanatoa jasho na wanakuwa wako macho kwa muda mrefu basi hii kahawa na vyakula vya kafeni viepukwe wakati unakwenda kulala,” anasema.

Anakitaja kitu kingine cha kuepukwa kuwa ni pamoja na kufanya mazoezi muda mfupi kabla ya kulala ili mifumo ya mwili ijiandae kwa usingizi.

“Mazoezi ni muhimu  na tuyafanye kwa muda maalum katika wiki  lakini mazoezi yasiingiliane na ratiba ya usingizi.

“Tenganisha mazoezi na muda wa kulala angalau saa nne hadi nane ndipo ratiba ya kulala ifiki hii ni muhimu,epuka kufanya mazoezi mazito fanya mepesi mepesi, pia unapozidi kuwa  mtu mzima hadi miaka 60 matatizo ya usingizi yanaongezeka zaidi ukawa hupati usingizi au unalala sana. 

“Haya matatizo ya watu wazima ni tofauti  na yanatakiwa kutibiwa kwa namna ambayo ni tofauti kwa ushauri kwa watu kamahawa wakiwa na matatizo wafatilie kwa muda na kuwaona wataalamu wapate ushauri ili waweze kusaidiwa,”anashauri Dk. Lemery. 

USINGIZI HUSAIDIA KUTUNZA KUMBUKUMBU 

Dk. Lemery anasema wakati mtu akiwa amelala mifumo ya mwili  kama ubongo, mifumo ya fahamu, mifumo ya upumuaji, mifumo ya moyo na usukumaji wa damu, mifumo ya chakula,haja kubwa, mkojo, mifupa, misuli na mifumo ya kinga ya mwili huanza kujiandaa kwa siku nyingine.

Kwa mujibu wa daktari huyo usingizi kwenye mfumo wa fahamu husaidia kutunza kumbukumbu vizuri na kuboresha umakini. 

“Lakini pia  kwenye mifumo ya mifupa na misuli inaondoa sumu  ambayo imekuwa ikijirundika wakati unafanya shughuli  mbalimbali.

“Na kwa mifumo ya chakula, kinasukumwa vizuri wakati ukiwa umelala na chakula kinanyonywa kile kilicho kwenye utumbo vile virutubisho vyote vinachukuliwa wakati huo.
“Lakini pia na  mifumo ya homoni ya mwili inajitengeneza na kujiweka vizuri kwa ajili ya kuanza siku nyingine na kuwezesha mwili kufanya vile inavyotakiwa,”anabainisha Dk. Lemery. 

Anasema kwa wakati huo mifumo ya kinga mwili  inapata muda wa kujiweka sawa kwani kipindi hicho  sumu zinaondolewa mwilini na kingamwili kutengenezwa.  

“Mfumo wa kinga unapata muda mzuri wa kuweza kujiandaa kwa ajili ya kulinda mwili kwahiyo unaona wakati huo mifumo yote inajiweka tayari kwa ajili ya kujisafisha  na kuanza kazi mpya siku inayofuatia.

UKUAJI MZURI KWA WATOTO 

Dk. Lemery anasema baadhi ya tafiti zinaonesha kwamba watoto wakilala wanaongeza homoni za ukuaji (growth hormon) .

“Hii  inazalishwa kwa kiwango kikubwa kipindi wakiwa wamelala kwenye usingizi mzito na hii inasaidia watoto kukua vizuri ukilinganisha na watoto kulala masaa machache chini ya masaa sita. 

“Usingizi unasaidia sana kwenye ukuaji wa watoto kwenye kiwango  cha kimo kinachohitajika na pia kuwa na uzito ambao unahitaji.

“Kwa watoto ambao wanasoma shule kwa siku nzima wanakuwa wamesoma vitu vingi vile vitu haviwezi kuwepo kama kumbukumbu kwa muda mfupi inabidi wakati wakiwa wamelala muda wa kutosha ndipo ubongo unafanya kazi taratibu ya kuchukua zile kumbukumbu na kuziweka sehemu ambapo zinakaa kwa muda mrefu na inakuwa rahisi   kuzikumbuka,”anabainisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles