25 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Hoja za wagombea zinajibu mahitaji sekta ya afya?

Na YOHANA PAUL

SERIKALI ya awamu ya tano chini ya, Dk. John Magufuli kwa kipindi cha miaka mitano inaeleza kufanya maboresho makubwa kwenye sekta ya afya katika nyanja za uboreshaji wa miundombinu ya vituo vya afya, zahanati na hospitali.

Taarifa kutoka Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa serikali ya awamu ya tano  imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za wilaya 71 na hospitali za mikoa 10.

Pia, taarifa zinaeleza kuwa kumekuwa na ukamilishaji wa ujenzi wa hospitali za rufaa za kanda tatu, kutoa ajira kwa watumishi wa afya wapya 14,479 ikiwemo madaktari 1,000 na kuongeza idadi ya watumishi wa afya kutoka watumishi 8,6152 hadi 163,100.

Aidha, ndani ya kipindi hiki cha miaka mitano serikali ya awamu ya tano imeeleza kuongeza bajeti ya vifaa tiba  na dawa ambapo bajeti imeongezeka kutoka shilingi bilioni 31 hadi sh bilioni 270 ambayo imesaidia kununuliwa magari ya kubebea wagonjwa 117 na kufanikiwa kusomesha madaktari bingwa 301 ambao wamewezesha kuimarisha matibabu ya kibingwa ya moyo, masikio, kansa na ubongo.

Kutokana na hatua hizo, takwimu za Wizara ya Afya zimebainisha, idadi ya kina mama wanaojifungulia katika vituo vya afya imeongezeka kutoka asilimia 64 hadi kufikia asilimia 83 hivi sasa, huku vifo vya watoto wachanga ikipungua kutoka wastani wa vifo 25 hadi saba kwa kila vizazi hai 1,000, na kupunguza idadi ya rufaa za matibabu kwenda nje ya nchi kwa asilimia 95.

Mbali na maendeleo hayo yaliyofikiwa katika sekta ya afya ndani ya kipindi cha miaka mitano (2015-2020), inaelezwa kuwa bado zipo baadhi ya changamoto ambazo zimeendelea kuwa kikwazo cha upatikanaji kwa wakati wa huduma bora za afya kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitalini.

Katika kipindi hiki cha kampeni, vyama vya siasa vikiwa kwenye hatua ya lala salama ya kuomba kuchaguliwa kuchukua uwakilishi wa wananchi, wagombea wamejipambanua kwa namna tofauti wakinadi sera zao kuelezea mipango na mikakati yao watakavyotatua kero zilizopo kwenye sekta ya afya.

Wagombea ubunge jimbo la Nyamagana Kupitia vyama vitatu vinavyoongoza kwa sasa nchini yaani Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na ACT WAZALENDO kwa nyakati tofauti wametumia majukwaa kuelezea jinsi wanavyoenda kutatua changamoto zilizopo kwenye sekta ya Afya jimboni hapa.

Stanslaus Mabula ni Mgombea Ubunge Jimbo la Nyamagana (CCM) ambaye pia ni mbunge aliyemaliza muda wake akiwa kwenye moja ya mikutano yake ya kampeni anasema, siku zote maendeleo ya sekta ya afya imekuwa moja ya kipaumbele chake kikubwa kipindi alipokuwa mbunge na hata wakati huu wa kampeni.

Anasema  kwa kipindi chake akiwa Mbunge wa Nyamagana, yeye kwa kushirikiana na serikali wameweza kufanya maboresho makubwa katika hospitali ya wilaya ya Nyamagana kiasi cha Kujenga mazingira rafiki ya upatikanaji huduma kwa wanaume, wanawake na watoto.

Mabula anasema amefanikisha ujenzi wa jengo la wodi ya wazazi kwa gharama ya Sh. Millioni 153 ambapo litasaidia kutatua changamoto za malazi kwa mama na mtoto.

Anasema pia amefanikisha ujenzi wa maabara katika zahanati ya Fumagila, kata ya Kishiri pamoja na kuwezesha ujenzi wa jengo la upasuaji kwa gharama ya sh. Milioni 120.

Anasema ujenzi wa jengo la upasuaji unaenda kuokoa maisha ya mama na mtoto kwa kiasi kikubwa kwani kina mama wajawazito wenye uchungu pingamizi wataweza kufanyiwa upasuaji na kuwahakikishia usalama wao na watoto.

Mabula anaeleza hadi sasa tayari wameshakamilisha ujenzi wa wodi ya wanaume katika hospitali ya wilaya pamoja na kuboresha miundombinu ya upatikanaji wa huduma bora kwa wagonjwa ikiwemo kuongeza vitanda 30.

Anasema akipata nafasi ya kurejea kukalia kiti cha Ubunge jimbo la Nyamagana ataendelea kufanyia maboresho zahanati na vituo vyote vya afya viwe na uwezo wa kutoa huduma bora za afya kabla ya kukimbilia hospitali ya wilaya na hata kabla ya kipewa rufaa ya kuelekea hospitali ya rufaa ya mkoa Sekou Toure na hosptali ya rufaa ya kanda Bugando.

Mgombea huyo wa Ubunge kupitia CCM anahitimisha kwa kuishukuru serikali kwa kuwezesha maboresho hayo  na kuwahakikishia wananchi wa Nyamagana kuendelea kutoa kipaumbele cha maendeleo kwenye sekta ya afya kufikia adhima ya maisha salama kwa mama na mtoto.

Kwa upande wake Mgombea ubunge jimbo la Nyamagana kupitia CHADEMA,  John Pambalu anasema ingawa taarifa zinaonyesha kuna maboresho makubwa yamefanywa kwenye sekta ya afya nchi nzima lakini huduma za afya zilizopo jimboni humo bado haziridhishi.

Anasema ili huduma za afya ziwe zenye kuridhisha na za kiwango kinachohitajika ni lazima kuwepo na maboresho kwenye nyanja kuu tatu muhimu ambazo ni miundombinu ya kutolea huduma, vifaa tiba pamoja na wafanyakazi wa kutosha wenye taaluma na weledi kwa maana ya madaktari na wauguzi.

Pambalu anasema ukifanya uchunguzi utabaini mbali na maboresho yanayotajwa kufanyika kwenye sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa majengo ya kutolea huduma lakini bado kuna mapungufu makubwa kwenye nyanja hizo kuu tatu za utoaji huduma.

Anasema iwapo atapata dhamana ya kuwa mwakilishi wa jimbo la Nyamagana atahakikisha anahamasisha wabunge wengine kuishinikiza serikali kuongeza bajeti ya sekta ya afya pamoja na kutoa kipaumbele cha ajira kwa wahudumu wa afya kwani ushahidi upo wazi watumishi wa afya hasa madaktari hawatoshi nchi nzima ikiweno jimboni Nyamagana.

Anasema moja ya kipaumbele chake kikubwa iwapo atapewa dhamana ni kupanua zahanati zote jimboni humo kufikia hadhi ya vituo vya afya na kuongeza vifaa tiba vya kutosha ili kuongeza uwigo wa upatikanaji wa huduma za tiba kwa makundi yote kwa kuwa ujenzi wa majengo ya zahanati na vituo vya afya bila vifaa tiba vya kutosha siyo kigezo cha maboresho ya huduma za afya.

Akiongelea namna atakavyopunguza vifo vya mama na mtoto Pambalu anasema atahakikisha anaongeza ujenzi wa wodi za wazazi kwenye vituo vya afya na hospitali ya wilaya na kuweka uhakika wa upatikanaji wa vifaa tiba.

Anasema uwepo wa vifaa tiba utasaidia kuondoa changamoto wanazokutana nazo kina mama ikiwemo kutoa uhakika wa huduma za afya zinazotolewa zisiwe bora huduma bali ziwe ni huduma bora.

Pambalu anasema maboresho ya huduma za afya pia yanahusisha elimu ya afya kwani siku zote huduma za afya haziwezi kutoa matokeo chanya kama jamii haina uelewa wa kutosha juu ya masuala ya afya na kuahidi akichaguliwa kuwa Mbunge wa Nyamagana, ofisi ya mbunge itashirikiana na Taasisi za Serikali na zisizo za serikali (NGOs) kutoa elimu ya afya ya uzazi hasa kwa vijana na wanawake.

Pambalu anahitimisha kwa kusema katika kipindi chake cha uongozi suala la maboresho ya huduma za afya litaenda sambamba na elimu ya afya kwani elimu ndiyo kinga bora siku zote ambapo itaongeza uelewa kwenye jamii na kupunguza vifo vya wajawazito kwa kuongeza mahudhurio ya kliniki na hata kuwashawishi kujifungulia hospitali badala ya majumbani.

Mgombea Ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha ACT-WAZALENDO, Chagulani Adamu naye anasisitiza kuwa msingi mkuu wa maboresho ya huduma za afya ni upatikanaji wa elimu ya afya na watoa huduma wa kutosha.

Anasema hadi sasa taarifa zinaonyesha ni asilimia 19 pekee ya wajawazito jimbo la Nyamagana ndiyo wanatajwa kujifungulia kwenye vituo vya afya na hospitalini huku idadi kubwa ya kina mama wajawazito wakiendelea kujifungulia majumbani mwao, na hayo yote ni matokeo ya ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi kwenye jamii.

Anasema akipata nafasi ya kuchaguliwa kuongoza jimbo la Nyamagana atakuwa na nafasi ya kushirikiana na asasi mbalimbali za kiraia kutilia mkazo suala la elimu ya uzazi pamoja na kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kama majukwaa ya kufikisha elimu hiyo ambayo pia itawekewa mkazo zaidi kwa mabinti mashuleni ili kupiga vita mimba za utotoni.

Anasema atapigania maslahi ya wahudumu wa afya walipwe kulingana na ukubwa wa kazi yao kwani kuwa na idadi kubwa ya madaktari na wauguzi siyo kigezo cha kutatua kero za afya bali maslahi ya wafanyakazi yanapaswa kupewa kipaumbele ili kuwaongezea molari na umakini wa kazi yao.

Chagulani anahitimisha kwa kuahidi kuwa akipewa ridhaa ya kuongoza jimbo la Nyamagana atahakikisha vituo vyote vya afya vinatoa huduma zote kwa masaa 24 ili kupanua uwigo wa upatikanaji wa matibabu kwa wenye uhitaji muda wote ikiwemo wajawazito wanaohitaji kujifungua.

Maridhia Ngemela mkazi wa jimbo la Nyamagana yeye ni mama wa watoto wawili anasema amesikia kuhusu hoja za wagombea juu ya maboresho ya huduma ya afya hususani huduma ya mama na mtoto.

Anasema ni kweli uboreshwaji mkubwa umefanyika lakini bado kuna changamoto ya vifaa tiba, elimu ya afya ya uzazi na gharama kubwa kwa kina mama wanaojifungulia hospitalini.

Anasema yeye amebahatika kupata mtoto mapema mwaka huu, lakini ukweli ni kwamba alijionea gharama kubwa ambazo zinajumuisha kufungua faili, kulipia sindano, glovu, mipira na kitanda ambapo anaomba kiongozi yeyote hasa wabunge watakaobainika kupata nafasi za uongozi wapiganie wizara ya afya ipunguze gharama hizo au itoe muongozo  ili kuepusha sintofahamu wanayokutana nayo kina mama juu ya gharama za uzazi.

Maridhia anasema pia suala la elimu ya afya ya uzazi ni lazima liwekewe mkazo na viongozi watakaopata nafasi kwani kwa maeneo anayoishi amejionea kina mama wengi ambao ingawa wana watoto zaidi ya mmoja lakini bado hawaelewi dalili za uzazi usiogope salama.

Aisha Seleman mama wa watoto watatu anasema alipata mtoto wa mwisho mwaka 1994 na hadi kufikia leo amejionea maboresho makubwa kwenye sekta ya afya ingawa kitu cha muhimu kwa viongozi watakaopata nafasi wanatakiwa kuwekea mkazo ni uboreshwaji wa miundombinu na upatikanaji wa vifaa tiba kwa kuwa hivyo vyote ndiyo vinawapa uwezo madaktari na wauguzi kutoa huduma bora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles