Na Ashura Kazinja-Morogoro.
WITO umetolewa kwa wanasiasa wote nchini kufanya siasa za kistaraabu na kuepuka matusi katika kipindi hiki cha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwenzi Oktoba mwaka huu.
Wito huo ulitolewa jana na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Morogoro, Jacob Mameo, wakati wa ufunguzi wa semina ya kuwajengea uwezo wanawake wakristu ambao ni viongozi wa dini, juu ya haki za kijinsia mjini Morogoro.
Akizungumza katika semina hiyo Askofu Mameo aliwataka wanasiasa na mashabiki wa siasa kote nchini kuitunza amani ya nchi kwa kuepuka kampeni za matusi.
“Tunawaomba wanasiasa wafanye kampeni zao kistaarabu,waseme sera zao na waache matusi na vurugu,” alisema Askofu Mameo.
Katika hatua nyingine Askofu Mameo aliwataka wanawake viongozi wa kikristu kuzungumza na wanawake wenzao na kuwaeleza umuhimu wa kushiriki uchaguzi na kuacha ushabiki sambamba na kuliombea Taifa.
“Wanawake mnatakiwa kusikiliza sera za wagombea kwa makini, acheni ushabiki na mpige goti kuliombea taifa ili lifanye uchaguzi wa amani”. alisema Askofu Mameo.
Naye Ofisa Programu Idara ya Maendeleo ya Wanawake, Watoto na Jinsia Jumuiya ya Kikristu Tanzania, Ester Muhagachi alisema wanawake ni wahanga wakubwa pindi inapotokea vurugu na hivyo wanapaswa kuwashauri vizuri waume na watoto wao kushiriki kampeni za kisiasa kistaarabu na kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.
“Sisi akina mama ndio wahanga wakubwa ikiwa itatokea machafuko na vita, pia ni wahanga wakubwa wa matokeo yatakayotokana na kuchagua viongozi wasiofaa ambao hawawezi kutuletea maendeleo,” alisema Ester.
Ester aliongeza kusema kuwa huu ni wakati ambao wanawake kote nchini wanapaswa kuwa makini na kusikiliza sera za wagombea ili waweze kufanya maamuzi sahihi ifikapo siku ya kupiga kura.
“Pamoja na kuliombea Taifa kuwa na uchaguzi wa amani, akina mama tunapaswa kuzungumza na watoto wetu, wajiepushe na vurugu sambamba na kujitokeza kwa wingi kupiga kura kuamua hatima ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla,” alisema Ester.