Na KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi imemtia hatiani na kumuhukumu kwenda jela miaka 30 mfanyabiashara Shaban Kalikuta kwa kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Mshtakiwa huyo alitiwa hatiani mbele ya Jaji Lilian Mashaka baada ya Mahakama kujiridhisha kwamba Jamhuri imethibitisha kosa bila kuacha shaka.
Mshtakiwa alikamatwa Agosti 29 mwaka 2001 katika mtaa wa ufipa Kinondoni Dar es Salaam akiwa na dawa za kulevya gram 238.24 aina ya heroin hydrochloride.
Upande wa Jamuhuri ulikuwa na mashahidi 8 na vielelezo 5 ili kuthibitisha kesi.
Baada ya kuchambua ushahidi kwa ujumla wake mahakama imeona kwamba upande wa Jamhuri umethibitisha kesi bila kuacha shaka.
Jaji Mashaka alimtia hatiani mshtakiwa na kumuhukumu kwenda jela miaka 30.
Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili Costantine Kakula na Batilda Mushi na kwa upande wa utetezi uliwakilishwa na Wakili Abraham Senguji.