Grace Shitundu
UFUGAJI wa ng’ombe wa maziwa ni moja ya kati ya shughuli zinazoweza kuwakomboa wafugaji.
Ili kupata faida kutokana na shughuli hii ya ufugaji, wafugaji wanashauriwa kuzingatia kanuni wanazoshauriwa na wataalamu katika sekta ya mifugo.
Uzalishaji wenye faida kwa ng’ombe wa maziwa huhitaji uangalizi wa karibu, unaowezesha kutambua ni wakati gani ng’ombe ana joto na yuko tayari kupandwa au kufanya uhimilishaji.
Mfugaji yoyote anatakiwa kutambua ni wakati gani ng’ombe anakuwa na joto la kuhitaji kupandwa au kufanyiwa uhimilishaji.
Pamoja na mbinu ya kuhimilisha kupigiwa chapuo kila mahali bado wafugaji wengi wanazalisha mifugo yao kwa kuacha wapandane wenyewe.
Hata hivyo kuna baadhi ya wafugaji wamekuwa wakikumbana na changamoto ya mifugo yao kutokuwa na uhitaji wa kupandwa.
Kuna mambo mbalimbali yanayohusiana na mazingira, afya ya ng’ombe na lishe yanaweza kuathiri uhitaji wa ng’ombe kupandwa.
Miongoni mwa mambo yanayoathiri uhitaji wa ng’ombe kupandwa ni pamoja na:
Banda
Hili ni jambo ambalo linaweza likachukuliwa kwa jambo la kawaida kwa kuweka banda ambalo ni si banda bora.
Ili ng’ombe wawe na uhitaji wa kupandwa ni muhimu kuwa mpangilio wa banda linaloruhusu ng’ombe kuingiliana au kuwa pamoja wakati wote kwani hutoa mwanya kwa ng’ombe kupandwa na tabia ya kusimama hudhihirika kwa urahisi.
Sakafu
Tendo la kupanda hufanyika mara nyingi zaidi ikiwa ng’ombe wapo katika eneo la udongo au kwenye nyasi badala ya sakafu ya saruji.
Hali ya utelezi, tope pamoja na kukosekana kwa nafasi ya kutosha huzuia kupandana.
Matatizo ya miguu
Matatizo ya miguu au kidonda miguuni hufanya ng’ombe kutopenda kupandwam huwa na kiwango cha chini cha kupandisha na hushindwa kuonye
sha ushirikiano kwani hukwepa zaidi kupata maumivu.
Joto
Joto ni hali ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa ng’ombe kupandwa.
Kwa kawaida, ng’ombe huwa katika joto mara moja kila baada ya siku 17 hadi 25 na ng’ombe jike huonyesha ishara ya kwanza ya joto ndani ya wiki tatu hadi baada ya kuzaa.
Wataalamu wanaeleza kwamba wakati muafaka wa kumshughulikia ng’ombe ni kati ya siku 45 hadi 90 baada ya kuzaa.
Kushindwa kutambua joto ni chanzo kikubwa cha urutubishaji hafifu hivyo ni muhimu mfugaji kuweka kumbukumbu ya taarifa zote za joto
Ng’ombe huonyesha zaidi kuhitaji kupandwa hasa katika kipindi cha baridi kuliko kipindi cha joto.
Muda wa kupandisha
Muda wa kupandisha ni jambo la msingi la kuzingatia, baadhi ya wafugaji wamekuwa hawazingatii hili hivyo kufanya mifugo yao kutokuwa na hamu ya kupandwa kwa kuwa wakati wanahitaji inawezekana wasipate mazingira ya kufanya hivyo.
Kupandisha mara nyingi hufanyika wakati wa asubuhi au mapema wakati wa jioni, ng’ombe akionekana kuwa kwenye joto kabla ya 12:00 asubuhi ni lazima apandishwe siku hiyo hiyo, wakati ng’ombe aliyeonekana kwenye joto baada ya mchana ni lazima kupandishwa mapema siku ya pili.
Namna ya kumfahamu ng’ombe aliya na joto
Mfugaji anatakiwa kumchunguza ng’ombe husika kwa ukaribu zaidi hasa katika kipindi cha awali cha dalili za joto.
Ng’ombe kusimama anapopandwa na wenzake au dume, hiyo ni dalili tosha kuwa yupo katika wakati muafaka na joto linalostahili kupandwa au kufanyiwa uhamilishaji.
Pia ng’ombe wanahitaji nafasi ya kutosha ili kuchangamana, muda wa wastani wa joto la kusimama ni kati ya saa 15 hadi 18, lakini pia huweza kutofautiana kutoka saa nane hadi 30.
Kupanda ng’ombe wengine, ng’ombe anayeonesha tabia hii huweza kuwa katika joto au kukaribia joto.
Kutokwa ute; Hii ni dalili isiyofungamana moja kwa moja na joto la kusimama.
Ute huzalishwa kutoka katika mfuko wa uzazi na hujilimbikiza pamoja na majimaji mengine katika uke kabla na muda mfupi baada ya kipindi cha joto kupita.
Kuvimba na wekundu katika uke; dalili hizi huonekana kabla ya joto na hubaki kwa muda mfupi baada ya joto
Kutokutulia; Ng’ombe anapokuwa katika hali hii huwa hatulii, huhangaika, hukosa kupumzika na hata hula kidogo sana kuliko wengine.
Kunusa: ng’ombe anapokuwa kwenye joto hunusa na kulamba uke wa ng’ombe wengine mara kwa mara.
Mambo ya msingi
Kuna mambo ya msingi ambayo mfugaji anashauriwa kuyazingatia anapofanya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ili kuhakikisha anazalisha kwa wingi.
Uchaguzi wa aina bora ya ng’ombe ni jambo la msingi kabla ya kuanza kufuga hivyo mfugaji anatakiwa kufahamu aina ya ng’ombe bora wanaoweza kumfaa.
Miongoni mwa aina za ng’ombe ambazo mfugaji anashauriwa kuchagua ni pamoja na Fresian, Guersey, Jersey, Ayrshire na Brown swiss
Miongoni mwa aina hizo Fresian ndio aina inayopendwa sana kwani ndio aina ambayo inatoa maziwa mengi sana kuliko aina zingine zilizo bakia.
Pia katika mambo muhimu mfugaji anatakikwa kuhakikisha ng’ombe wanaoshwa kwa dawa ili kupunguza kushambuliwa na wadudu ambao wanaweza kusababisha maambukizi ya magonjwa, na wanaweza kuoshwa kila wiki kutokana na ratiba ambayo mfugaji amejipangia.
Lazima banda liwe safi ili kuzuia maambukizi ya magonjwa kama FOOT ROUT na usafi unaweza kufanyika kila siku asubuhi au jioni.
Ng’ombe lazima apewe chakula na maji safi ili kuongeza uzalishaji.
Pia ni lazima kuwatibu au kuchukua hatua pale ng’ombe anapoonekana kua na ugonjwa ili kuepusha maambukizi kwa wengine na pia ili kumuokoa.