30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Watano kunyongwa kwa kumuua Dk. Mvungi

 KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

WATUHUMIWA watano wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kumuua aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Nchini , Dokta Sengondo Mvungi huku mmoja akiachiwa huru.

Mahakama Kuu ilifikia kutoa hukumu hiyo jana mbele ya Jaji Seif Kulita baada kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka. 

Hukumu hiyo imetolewa baada ya mchakato wake kuchukua miaka takribani saba

Waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa ni Msugwa Matonya, Miyanda Mlelwa maarufu kama White na Paulo Mdonondo. 

Wengine ni aliyekuwa mlinzi wa Dk. Mvungi, Longishu Losingo na John Mayunga maarufu kama Ngosha. 

Upande wa mashitaka ulikuwa na jumla ya mashahidi 16 pamoja na vielelezo 15. 

“Mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka inawahukumu kunyongwa hadi kufa watuhumiwa watano na inamwachia huru Juma Kanungu , baada ya kujiridhisha kwamba upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake,”alisema.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwakilishwa na jopo la mawakili watatu ambao ni Wakili wa Serikali Mwandamizi Cledo Lugaju, Lilian Lwetambula na Veronica Mtafya. 

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao kwa pamoja walidaiwa kuwa Novemba 3, mwaka 2013 walifanya kosa hilo la mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha sheria na kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Ilidai kuwa siku ya tukio, katika eneo la Msakuzi Kiswegere lililopo eneo la Wilaya ya Kinondoni, washtakiwa hao kwa pamoja walimuua kwa kukusudia Dk Sengondo Mvungi.

Desemba 22, 2013, washtakiwa hao na wengine walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka ya mauaji.

Upelelezi wa kesi hiyo ulipokamilika washtakiwa wanne waliachiwa huru, jalada likahamia Mahakama Kuu kwa kesi kuanza kusikilizwa.

Novemba 22, 2018, wakati kesi hiyo inataka kuanza kusikilizwa DPP aliwasilisha hati akionyesha hana nia ya kuendelea na shauri hilo, washtakiwa wakaachiwa huru.

Muda mfupi baada ya kuachiwa walikamatwa tena na kusomewa upya mashtaka hayohayo na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na baada ya tararibu za kisheria kukamilika ilihamishiwa Mahakama Kuu kwa kusikilizwa.

Dk Mvungi mbali na kuwahi kuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alikuwa alikuwa msomi aliyebobea katika masuala ya sheria.

Pamoja na kutoa mchango mkubwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba alikuwa mstari wa mbele kupigania haki za binadamu, kazi aliyoifanya kwa moyo.

Dk Mvungi, alifariki dunia Afrika Kusini alikopelekwa kwa ajili ya matibabu baada ya kujeruhiwa vibaya na watu walipovamiwa nyumbani kwake Kibamba, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Novemba 3 mwaka 2013.

Alipelekwa nchini Afrika Kusini, Novemba 7, 2013 kwa matibabu zaidi baada ya kulazwa kwa siku tano kwenye Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (Moi) jijini Dar es Salaam.

Dk Mvungi, ambaye aligombea urais mwaka 2010 kwa tiketi ya NCCR- Mageuzi, alijeruhiwa vibaya kichwani na sehemu nyingine za mwili wake baada ya kukatwa mapanga na wavamizi hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles