28.2 C
Dar es Salaam
Monday, July 4, 2022

HUYU ZUCHU HUYU, NYIE MWACHENI

 MWANDISHI WETU 

HAKUNA kitu kinachoitwa bahati kwenye maisha kwa sababu bahati ni matayarisho yanapokutana na wakati sahihi ndio hapo unaona mtu anapaa kimafanikio kwa haraka tofauti na matarajio ya wengi. 

Kwani ni wasanii wangapi wanasimamiwa na lebo zenye pesa lakini hatuwasikii. Ni kwa sababu hawana maandalizi ya kile wanachofanya ndio maana hata watumie gharama kiasi gani bado wanaendelea kubaki chini, hawatoboi. 

Ila tunaona wale waliojifanyia matayarisho na wakakutana na wakati sahihi, wakiachia ngoma moja tu wanatoboa, kila shabiki wa muziki atafahamu kuwa kwenye ‘game’ kuna ingizo jipya la msanii. 

Hali hiyo imemkuta Zuchu, msanii mpya wa WCB anayejiwekea rekodi kadhaa ambazo bila shaka hata yeye mwenyewe zinamshangaza. Anateleza tu na kila siku amekuwa gumzo kwa muziki wake kuandika rekodi mpya mpya. 

Ni miezi mitano sasa tangu atambulishwe lakini habari zake zimepenya mpaka nje ya Bongo ambako si rahisi kwa msanii mdogo kufika kwa haraka kiasi hicho. 

Kama nilivyosema hapo awali kwamba maandalizi yanapokutana na wakati sahihi hutokea kile kinachoitwa bahati ni dhahiri kuwa Zuchu alishafanya maandalizi ya kutosha na alivyokutana na WCB wakamtambulisha wakati sahihi kilichobaki ni historia. 

Hasa ukizingatia WCB wamebobea katika kuwapa thamani wasanii wao, hawana jambo dogo wanapotambulisha bidhaa zao. Hata kama ukiwa ni msanii wa kawaida ila ukiingia WCB, lazima uwe mkubwa kwa viwango vya kukubalika ndani na nje ya Bongo. 

Ukiacha kukubalika mpaka na viongozi wakuu wa nchi kama vile Rais Magufuli, Zuchu amefanikiwa kuliteka soko la mtandao. Ukichungulia kwenye mitandao ya kusikiliza, kununua na kupakua muziki utaona jinsi ambavyo mrembo huyu amekuwa na nguvu kubwa kwa kila ngoma anayoachia tofauti na wasanii wengi wapya. 

Zuchu ambaye ndani ya miezi miwili alikuwa tayari amefikisha wafuasi (subscribers) 200,000 kwenye chaneli yake ya YouTube, aliwekwa kwenye orodha ya tamasha la One Africa Festival ya watawala wapya wa muziki Afrika akiwa na kina Sho Madjozi wa Afrika Kusini, Rema, Fireboy, Oxlade na Joeboy wa Nigeria. 

Mitandao ya muziki kama Boomplay Music, Audiomack, Apple Music, iTunes, Spotify, Deezer, Tidal, Pandora, Amazon Music na mingineyo, Zuchu alifikisha idadi ya wasikilizaji wa EP yake ya I Am Zuchu zaidi ya milioni 21 ndani ya miezi miwili. Siyo mchezo. 

Juzi kati Zuchu alitajwa na jarida moja nchini Kenya kama ni toleo la kike la Diamond Platnumz hali kadharika mtandao wa kuuza muziki duniani, Apple Music hivi karibuni ulimtaja kama mmoja ya wasanii wa kutazamwa zaidi barani Afrika. 

Wiki hii Zuchu na bosi wake, Diamond Platnumz, wameweka rekodi mpya kupitia kolabo zao mbili, Litawachoma na Cheche, nyimbo ambazo zimetazamwa na watu zaidi ya milioni 1 ndani ya saa 24. 

Mara kadhaa tumeona msanii akiingiza wimbo mmoja kwenye mzunguko wa kusikilizwa ila ni nadra kuona msanii mmoja akiingiza ngoma zaidi ya moja kwenye ‘trending’ katika mtandao wa YouTube. 

Kwa Zuchu imewezekana na hii inatajwa kama rekodi ya kwanza kwa msanii wa muziki kutrendi YouTube kuanzia namba moja hadi tatu kwa audio mbili na video moja tangu mtandao huo uanzishwa mwaka 2006. 

Yaani video ya Cheche na audio za Cheche na Litawachoma, zimeweka rekodi hiyo ya kipekee ambayo inaweza kuchukua muda mrefu kuvunjwa na msanii mwingine. 

Zuchu na Diamond Platnumz wameendelea kuwa gumzo na kuchochea tetesi za kutoka kimapenzi kwa kile walichokiimba kwenye wimbo, Litawachoma na kile walichokionyesha kwenye video ya Cheche. 

Litawachoma ni ngoma fulani hivi kali ambapo humo ndani Diamond Platnumz anamwimbia mtoto mzuri jinsi ambavyo amebadilika, ameacha tabia mbaya na ameamua kutulia kwenye hilo penzi. 

Pia Cheche ni ngoma kali ya kuchangamka ambayo humo ndani Diamond na Zuchu wameitendea haki kwa kucheza huku ukaribu wao ndani ya video ukiacha maswali zaidi kwa mashabiki wao. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
195,637FollowersFollow
545,000SubscribersSubscribe

Latest Articles