27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

TRA: Wafanyabiashara acheni kumbukumbu za biashara zenu zizungumze

Na MWANDISHI WETU-KIGOMA

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wafanyabiashara Mkoa wa Kigoma kutozisemea biashara zao na badala yake waache kumbukumbu wanazotunza ziseme zenyewe kuhusu makadirio ya kodi. 

Hayo yamezungumzwa leo mkoani hapa na Afisa Msimamizi Mkuu wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA makao makuu, Julias Mjenga wakati akizungumza na wafanyabiashara alipowatembelea katika maeneo yao ya biashara.

Amesema utunzaji wa kumbukumbu za biashara ndio lugha kuu ya biashara hivyo kila mfanyabiashara anatakiwa kutunza kumbukumbu za biashara zake ili zimuwezesha kukadiriwa kodi kwa urahisi pasipo kuonewa.

Amesema katika mkoa wa Kigoma, wafanyabiashara wamekuwa na  hamasa kubwa ya kutaka kujua masuala mbalimbali ya kodi na kwamba katika kampeni ya elimu ya kodi ya mlango kwa mlango inayoendelea wanatarajia kuwafikia wafanyabiashara mbalimbali katika maeneo yao ya biashara ili kuwapa elimu. 

“Mambo tunayokutana nayo ni kwamba wafanyabiashara wengi hawana utaratibu wa kutunza kumbukumbu zao na sisi tunachofanya ni kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kutunza kumbukumbu za biashara zao pamoja na utoaji wa risiti,” amesema Mjenga.

Amesema iwapo watatunza kumbukumbu zao za biashara itawawezesha kuwa na hoja pindi watakapofika katika ofisi za mamlaka ya mapato kupeleka malalamiko yao iwapo watakuwa hawajaridhishwa na makadirio watakayokuwa wamekadiriwa.

Naye Nelson Nashozi ambaye ni mfanyabiashara mkoani Kigoma amesema kuwa amefurahia elimu ya utunzaji wa kumbukumbu za kila siku biashara na kwamba itawawezesha kupata makadirio halali ambayo hayatawaumiza na kuua mitaji yao.

Amesema pamoja na elimu waliyopata lakini ameitaka mamlaka hiyo kujenga mahusiano mazuri baina yao na wafanyabiashara ili kuwawezesha kulipa kodi kwa hiyari na kwamba bila wafanyabiashara kulipa kodi nchi haiwezi kupata maendeleo. 

Mfanyabiashara mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Pelesi Lusiga, amesema awali kabla ya kupata elimu ya kodi alipokuwa akiwaona maofisa wa TRA aliwafananisha na polisi ambao alihisi walifika kwaajili ya kumkamata lakini kutokana na uelewa alioupata anawashauri wafanyabiashara wenzake kutowakimbia na badala yake wanatakiwa kuwasikiliza na kutoa maoni yao.

Amesema elimu ya utunzaji wa kumbukumbu aliyoipata itamsaidia wakati wa kukadiriwa kodi na kwamba kwa jitihada zinazofanywa na TRA zitakuwa na matunda mazuri iwapo mahusiano mazuri baina yao na wafanyabiashara yataimarishwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles