25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

Mzee Moyo Nassor 1933- 2020

NA OSCAR ASSENGA- TANGA

ALIYEWAHI kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ya Zanzibar na mmoja wa waasisi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Mzee Hassan Nassor Moyo, amefariki dunia saa saba usiku wa jana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Bombo na kuzikwa unguja Zanzibar jana.

Mtoto wa Marehemu, Mohamed Hassan Moyo, alisema mwili wa baba yake uliondoka Tanga saa tatu asubuhi jana kwa ndege.

 Mohamed ambaye pia ni katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Muheza, alisema baba yake alikimbizwa hospitali ya Bombo usiku wa kuamkia Agosti 17 mwaka kutokana na kuugua ghafla kifua na kubana pumzi ambayo haikuwa ikitoka vizuri.

“Baba hakuwa akiugua na hakuugua kwa muda mrefu, alianza kubanwa na kifua na baadaye akaanza kupata shida ya kupumua, ilipofika saa 7.00 usiku ndipo akafariki”alisema Mohamed.

Mwili wa marehemu ulizikwa jana jioni kwenye eneo la Fuoni Unguja kisiwani Zanzibar.

Jana baada ya kutolewa kwa taarifa za kifo chake, Rais wa awamu ya tatu  HYPERLINK “https://twitter.com/jmkikwete” Jakaya Kikwete kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter aliandika “nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mzee Hassan Nasoro Moyo. 

“Tumepoteza mmoja wa viongozi wetu mashuhuri. Atakumbukwa daima kwa mchango wake muhimu katika kuendeleza Mapinduzi ya Zanzibar na kudumisha Muungano wetu. Innalillahi Wainna Ilaihi Rajioun.”

Harakati za siasa 

Mzee Moyo alikuwa mwanachama wa Chama cha Afro Shirazi (ASP) tangu kilipoanzishwa Februari 5, 1957, baadaye Februari 5, 1977 akajiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwa na kadi namba 7.

Mzee Moyo ndiye alikuwa Mratibu Mkuu wa Maridhiano ya Zanzibar ya Novemba 5, 2009 yaliyowakutanisha Rais Mstaafu wa Zanzibar (awamu ya sita), Dk Aman Abeid Karume na Maaalim Seif Sharif Hamad katika kutafuta mbinu ya kuondoa tofauti iliyokuwepo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Maridhiano hayo yalileta faraja kwa wananchi wa Zanzibar, hasa katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. 

Afukuzwa CCM

Mwaka 2015 Mzee Moyo alivuliwa uanachama wa CCM, hatua iliyofikiwa na Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa wa Magharibi, Unguja viswani Zanzibar.

Tuhuma zake

Miongoni mwa makosa yalioorodheshwa na chama hicho yanayomhusu Mzee Moyo ni pamoja na lile la kuhudhuria mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika Februari 9 mwaka 2014 katika uwanja wa Tibirinzi uliopo Pemba.

Inaelezwa kuwa alipopanda jukwaani, alisema anamuamini Maalim Seif Sharif na kumkubali Mwenyekiti wa CUF.

Kosa lake jingine alilifanya Aprili 6 2014 katika kongamano lililoandaliwa na CUF. Siku hiyo Mzee Moyo anadaiwa alisema Muungano haukuletwa na ufalme na mkataba wa Muungano haujulikani ulipo.

Anadaiwa pia kutamka kuwa wajumbe wote waliokuwapo katika lililokuwa Bunge la Katiba walipaswa kutetea Zanzibar na Tanganyika na akaonya kuwa wakileta Katiba mbaya wananchi wataikataa.

Kosa jingine la Mzee Moyo kwa mujibu wa CCM, lilifanyika Aprili 30 2014, aliposimama jukwaani katika mkutano ulioandaliwa na CUF na kusema Serikali tatu ndiyo msimamo wa Zanzibar.

Kutokana na tuhuma hizi na nyinginezo, CCM wanasema Mzee Moyo alikiuka taratibu za Chama cha Mapinduzi.

Kwa mujibu wa taratibu hizo za kikatiba, mwanachama anatakiwa kuhudhuria na kutoa maoni yake katika mikutano ya chama.

Ajibu waliomfukuza

Wakati akifukuzwa, Katibu wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziza Ramadhani Mapuri, alinukuliwa akisema Mzee Moyo amefukuzwa kutokana na mwenendo wake usiozingatia maadili ya chama chake.

Baada ya kufukuzwa, Moyo alinukuliwa na vyombo vya habari akisema “sijashtushwa wala kushangazwa na uamuzi wao, maana wenye kufanya hivyo ni watoto wadogo na hawajui wanachokifanya.

 “Mimi siwezi kurudi nyuma asilani kwa sababu ninachokitetea ni maslahi ya Zanzibar. Kwa hivyo, nitaendelea kukitetea na kukiamini kile nilichosimamia,” anaeleza.

Alisema uamuzi uliotolewa na CCM wa kumvua uanachama anauchukulia kama ni wa kitoto, kwani  yeye hakuzaliwa  CCM na wala hakuna wa kumzuia asiwe na maoni tofauti.

 “Hatuwezi kuwa na maoni na mtazamo wa aina moja, kila mmoja ana mtazamo wake na mimi huu ndiyo mtazamo wangu, kwa hivyo siwezi kubadilika. Waache  wanifukuze lakini mimi siogopi kwani sikuogopa wakati wa Mzee Karume nilipokuwa nikisema…eeeeh nitaogopa sasa hivi?

 “Basi na tukubaliane kutokukubaliana haidhuru lakini hawawezi kunifunga mdomo nitaendelea kutetea Zanzibar iwe na mamlaka yake kamili na kamwe sitorudi nyuma

“Mimi hata mara moja sikuwahi kusema au kutamka kwamba nilikuwa mmoja wa waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964, na hata mara moja sikuwahi kusema au kutamka kuwa mimi ni mjumbe wa kamati ya watu 14. Ninachosema mimi ni mmoja wa waanzilishi wa Baraza la Mapinduzi na serikali yake ya mwaka 1964”alisema.

Nassor Moyo ni nani?

Alizaliwa mwaka 1933, alipata elimu yake ya msingi kuanzia mwaka 1940 hadi 47 katika Shule ya Mnazi Mmoja iliyopo kisiwani Unguja.

Mwaka 1955 alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa chama cha wafanyakazi huku yeye akichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa kwanza.

Mwaka 1960, alikwenda nchini Urusi kwa mafunzo ya uongozi wa vyama vya wafanyakazi kwa mwaka mmoja, kabla ya kuteuliwa na chama cha Afro Shirazi Party (ASP) kugombea ubunge wa jimbo la Mwangapwani bila ya mafanikio.

Nyadhifa Serikalini

Mzee Moyo aliteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi kuanzia mwaka 1964 hadi 1985.

Aidha kutoka mwaka 1964 hadi 1985, alikuwa waziri katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alikuwa waziri mdogo wa kazi (1964); Waziri wa Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Aprili – Septemba 1964); Waziri wa Kilimo Zanzibar (1964 hadi 1967); Waziri wa nchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1972-1977); Waziri wa mambo ya Nchi (1977-1980 ) na Waziri wa Kilimo Zanzibar ( 1980-1985).

Uzoefu wake kisiasa

Alijiunga na chama cha Afro Shirazi Party (ASP) mwaka 1957 na kuwa mjumbe wa Kamati Kuu na NEC ya chama na Katibu Mipango kuanzia 1972-1977.

Mwaka 1977, aliteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya watu 20 waliounda Chama Cha Mapinduzi. Alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na NEC ya CCM 1977-1992 na baadaye mwaka 1987 hadi 199, aliteuliwa kuwa Katibu wa Mkoa wa Dodoma. Alistaafu rasmi shughuli za kichama na kiserikali mwaka 1996.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,750FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles