NA MWANDISHI WETU – SIMIYU
WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), umeiasa jamii kuzingatia kusajili cheti au vyeti vya watoto kisheria pale wanapotaka kuasili mtoto au watoto.
Hayo yalielezwa juzi katika viwanja vya Nanenane mkoani Simiyu na ofisa habari wa Rita, Grace Kyasi.
Alisema kuwa inafahamika katika jamii ya kitanzania wapo watoto wanaokulia katika vituo vya kulelea watoto yatima, aidha ni kwa sababu ya wazazi kufariki au hawajulikani walipo.
Pia wazazi kukosa uwezo wa kuwapatia matunzo watoto licha ya kuwa wazima.
Grace alisema kutokana na hilo, wapo watu wazima ambao wana shauku ya kuwa na mtoto hata wa kuasili na hiyo ni kwa sababu ya pengine kutojaaliwa kuwa na watoto wa kuwazaa.
“Hivyo kuna utaratibu wa kufuata kisheria ili kuweza kuasili mtoto au watoto hao kwa kuzingatia sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009, ambayo imeweka utaratibu ili kuweza kusaidia watu wanaotaka kuasili mtoto/watoto kisheria.
“Kuasili mtoto maana yake ni utaratibu wa kumpatia mtoto aliyekosa mazingira ya kifamilia kupata matunzo ya kudumu ya kifamilia,” alisema Grace.
Alisema jumla ya vyeti 863 vimesajiliwa na Rita kutokana na watu mbalimbali kuleta maombi ili kuwasajili na kupata cheti cha kuasili mtoto kisheria katika ofisi hizo.
Grace alisema mhitaji anatakiwa kwenda Rita makao makuu ili kuwasilisha nakala ya uamuzi kutoka Mahakama Kuu na pia cheti cha kuzaliwa cha mtoto anayeasiliwa.
“Ni muhimu jamii kujua umuhimu wa kusajili cheti cha kuasili mtoto kwani kitasaidia katika kumpatia mahitaji yake ya msingi kama vile elimu, chakula, malazi na masuala ya afya kwa ujumla kama ambavyo watoto wengine wanapata katika jamii,” alisema Grace.
Alitaja moja ya haki za mtoto anazotakiwa kupata ni kulindwa jambo ambalo watoto wasiokuwa na wazazi wamekuwa wakiteseka kwa kuishi mazingira ambayo si rafiki, ambayo hayana ulinzi na kusababisha kufanyiwa vitendo viovu na watu wasiokuwa na maadili kama vile kubakwa na kunyanyaswa kijinsia.
Grace alisema hata hivyo iwapo mtu atasajili cheti cha kuasili, sheria itamchukulia kuwa ni sawa na mzazi wa mtoto husika, hivyo itasaidia pia kupunguza wimbi la watoto wa mitaani wanaoongezeka kila kukicha.