HADIJA OMARY LINDI
Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), imesema itaendelea kuwaunga mkono wakulima wa mikoa ya Lindi na Mtwara moja kwa moja katika kuwapa mikopo ya pembejeo.
Hayo yameelezwa na Ofisa masoko wa benki hiyo, Nasoro zaid alipokuwa akizungumza na Mtanzania Digital juu ya namna Benki hiyo inavyoshiriki katika kuwasaidia wakulima wa mkoa huo katika maonyesho ya wakulima nane nane kanda ya Kusini katika Viwanja vya Ngongo Manispaa ya Lindi yanayoendelea hivi sasa.
Zaid amesema kwa kutambua shuguli zinazofanywa na wakulima benki hiyo imeamua kutoa mikopo ya pembejeo na matrekta kwa wakulima yenye lengo la kuwasaidia kuongeza tija ya uzalishaji katika kilimo chao.
Amesema kwa mwaka 2018/19 benki yao imewakopesha wakulima fedha zaidi ya bilioni nne kwa ajili ya kununua pembejeo za kilimo pamoja na maandalizi ya mashamba ambapo kwa mwaka huu tayari imekopesha shilingi bilioni moja na kuongeza kuwa mikopo hiyo inaongezeka ama kupungua kulingana na mahitaji ya wakulima katika msimu wa mazao husika.