27.5 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Wananchi waipongeza TRA kutoa leseni za udereva

Wananchi wapongeza na kufurahia huduma ya kutoa leseni za udereva ambazo zinatolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika Maonesho ya Kilimo Ufugaji na Uvuvi -Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nyakabindi Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupokea leseni zao za udereva, baadhi ya wenye leseni wameipongeza TRA kwa uamuzi wa kutoa huduma hiyo ambayo inapatikana kwa urahisi na haraka.

“Sikutegemea kama nitapata leseni yangu haraka namna hii. Kwa kweli nawapongeza sana”, amesema Rayner Nicholause ambaye ni mkazi wa Dodoma.

Naye Andes Seiya mkazi wa Arusha amesema kwamba huduma ni nzuri kwani amepata leseni yake ndani ya siku moja baada ya kulipia. “Tunaomba huduma hii iboreshwe huko mikoani kwani kama imewezekana hapa katika maonyesho kwanini cihukue muda mrefu kupata leseni ya udereva katika ofisi za TRA?” alisema Seiya.

Kwa upande wake Nelson Mnyanyi ambaye ni Mkazi wa Dar es Salaam amesifu utoaji wa huduma katika banda la TRA na kusema kwamba ni huduma bora na zinatolewa  haraka na hivyo kuokoa muda. “Baada ya kupata taarifa kwamba leseni yangu ipo tayari nifike niichukue baada ya kulipia sikuamini. Nawashukuru na nawapongeza sana”, alisema Mnyanyi.

Mbali na kutoa leseni za udereva, huduma nyingine ambazo TRA inazitoa katika maonesho ya Nanenane ni pamoja na kutoa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa wafanyabiashara na watu binafsi, kutoa ankara za Kodi ya Majengo, kutoa elimu ya kodi katika shughuli za kilimo na elimu ya kodi kwa ujumla.

Aidha huduma nyingine ni kutoa maelezo ya fursa za masomo ambazo zinapatikana katika Chuo cha Kodi (ITA) ambacho kinamilikwa na TRA pamoja na namna ya kutuma maombi katika chuo hicho.

TRA kama ilivyo taasisi zinazoshiriki maonesho ya Nanenane imeboresha huduma zinazotolewa katika banda lake ili kuwaongezea wananchi uelewa kuhusu masuala ya kodi na hatimaye kuongeza uhiari wa kulipa kodi ambayo ndio tegemeo la taifa katika kuwahudumia wananchi na kuboresha miundombinu pamoja na kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Maonesho ya Nanenane yenye kauli mbiu, ‘Kwa Maendeleo ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi Chagua Viongozi Bora’, yanafanyika katika viwanja vya Nyakabindi Wilaya ya Bariadi katika Mkoa wa Simiyu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles