26.9 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

CUF yampitisha Lipumba kugombea urais, wapata mgombea Zanzibar

CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

BARAZA kuu la Chama  cha Wananchi (CUF ), limemteua kwa mara ya tano , Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mgombea urais wa Tanzania wa chama hicho kwa upande wa Tanzania na kujizolea kura  755 ambapo wajumbe waliohudhuria ni zaidi ya 700.

Kwa upande wa Zanzibar kura zilikuwa 734 ambapo Mussa Haji Kombo aliibuka na kura 538 akifuatiwa na Mohamed Habibi Mnyaa aliyeambulia kura 100 na Rajab Mbarouk Mohamed kura 84.

Awali katika mkutano huo mkuu uliofanyika jana jijini Dar es Salaam na kukutanisha wajumbe zaidi ya 700 kutoka Bara na Zanzibar.

Akifungua mkutano huo, Lipumba ambaye pia ni mwenyekiti chama hicho alisema “katika uchaguzi huu tunaingia tukiwa na nia moja ya dhati kushinda kwa kishindo na si kujaribu, tutahakikisha tunafanya kampeni za kistaaabu.”

Lipumba alitaja vipaumbele vya CUF endapo ikishika dola katika uchaguzi huo kuwa ni pamoja na kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa ili kuimarisha demokrasia ya kweli ikiwamo upatikanaji wa katiba mpya, uhuru wa kutosha wa vyombo vya habari na fursa ya kujieleza.

Kipaumbele kingine ni kufuta umaskini katika nyanja zote, kutokomeza njaa na kuhakikisha lishe bora kwa wajawazito na watoto, kutoa huduma bora za afya na kudhibiti vifo vya wajawazito na watoto.

“Tutahakikisha bajeti ya Wizara ya Afya inapanda na kufikia asilimia 15 ndani ya miaka 10 ijayo sambamba na kuandaa miundombinu, wataalam, vifaa tiba na vipimo vya kutosha kwa maradhi yote,”alisema Lipumba.

Pia atahakikisha Serikali yao inawahudumia wazee waliotumikikia taifa kwa miaka yote, kuwasaidia walemavu na kuwawezesha kupata ajira ikiwa ni pamoja na kutenga fungu maalum la kuwasaidia kupata vifaa vya kuwapunguzia dhidi ya ulemavu.

Lipumba aliongeza kuwa kipaumbele kingine ni usimamizi wa elimu bora na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kusimamia maendeleo ya kiuchumi nchini, usimamizi makini katika sekta ya kilimo na maendeleo ya viwanda, kuimarisha miundombinu na kuhamasisha uwekezaji na usimamizi wa rasilimali za taifa na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.

Lipumba katika historia ya vyama vingi vya siasa na nafasi ya ugombea urais Bara ilianza mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na mwaka huu.

Ikumbukwe mwaka 2015, Lipumba hakupata fursa ya kugombea nafasi hiyo kwakuwa vyama vya upinzani viliungana na kusimamisha mgombea kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao kwa pamoja waliridhia kumpitidha Edward Lowassa kuwa mgombea wa nafasi ya urais.

Kufuatia uteuzi wa mgombea huyo chama hicho kiliingia kwenye mtarafuku na kusababisha mgawanyiko uliozaa CUF Lipumba na CUF Maalum ambapo kwa Sasa baadhi ya wanachama wametimkia vyama vingine na CUF Lipumba ikiendelea.

Hata hivyo baada ya muda mchache mgombea huyo wa Urais, Lowassa kupitia Ukawa alirejea Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kwa upande wake, Mnyaa alisema amekuwa Mbunge kwa miaka 10, mbunge kiongozi wa CUF bunge lililopita na mpiganaji mkubwa wa chama hicho na ana uzoefu wa kutosha kupambana na CCM Zanzibar na kuchukua madaraka ya urais.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Msajili wa vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza alivitaka vyama vya siasa nchini kutumia hekima na busara katika uchaguzi mkuu ujao na kuacha lugha za matusi katika kunadi sera za vyama vyao.

Alisema Rais Dk.John Magufuli alisema uchaguzi ujao utakuwa huru na haki hivyo ni vema vyama vya Siasa navyo vikaunga mkono kwa kuwapata Wagombea kwa njia sahihi pamoja na kuzingatia miongozo mbalimbali ya uchaguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles