22.7 C
Dar es Salaam
Sunday, July 3, 2022

Mkapa shujaa wangu – JPM

Elizabeth Hombo -Dar es salaam

RAIS Dk. John Magufuli ameongoza waombolezaji kuaga kitaifa mwili wa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa huku akisema kiongozi huyo alikuwa shujaa wake na mtu muhimu katika historia ya maisha yake.

Shughuli hiyo ya kuaga kitaifa ilifanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ambako maelfu ya waombolezaji wakiwamo viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi walijitokeza. 

Mkapa ambaye aliongoza nchi kwa miaka 10 mfululizo kuanzia mwaka 1995 hadi 2005, alifikwa na mauti kwa mshtuko wa moyo Alhamisi ya Julai 23, mwaka huu katika moja ya hospitali jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli akihutubia taifa katika shughuli hiyo, mara kadhaa alikuwa akitulia na kutokwa machozi hadharani, hasa alipoanza kuelezea mazungumzo yake ya mwisho na Mkapa.

“Nilipata fursa ya kuongea na mzee Mkapa kwa simu akiwa hospitalini saa chache kabla hajafariki, nakumbuka aliniambia John usiwe na wasiwasi naendelea vizuri, sikujua kwamba maneno yale yalikuwa ya kuniaga, kazi ameikamilisha. Namshukuru Mungu kwa zawadi ya Mkapa,” alisema Rais Magufuli huku akitoa kitambaa kufuta machozi. 

Alisema hakuna mtu anayeweza kumwelezea vizuri Mkapa zaidi ya alivyojieleza mwenyewe kwenye kitabu chake cha ‘My Life, My Purpose’. (Maisha Yangu, Dhamira Yangu).

“Kama ambavyo nimekuwa nikisema bila Mkapa huenda mimi nisingekuwepo hapa nilipo, ni mtu muhimu katika historia ya maisha yangu.

“Hata nilipopatwa na shida au kupambana na changamoto mbalimbali hakuniacha, hakutaka nianguke.

“Mzee Mkapa alinilea kama mtoto wake, alikuwa ni shujaa wangu, alinionyesha upendo, hata kwenye shida Mzee Mkapa hakuniacha kamwe, hakutaka nianguke, alinilea kama mtoto wake. Wakati wote alikuwa ananionyesha upendo, hivyo basi kuondoka kwake ni pigo kubwa kwangu, nimepoteza mtu muhimu katika maisha yangu.

“Saa nyingine machozi yanakuja tu, msinishangae sana, hata mzee Kikwete (Jakaya Kikwete) nilimuona juzi anadondosha machozi, tena Kikwete ni Kanali lakini alitoa chozi, kwa hiyo msinishangae mimi,” alisema Rais Magufuli.

Vilevile Rais Magufuli alisema kuwa kifo cha Mkapa ni pigo kubwa kwa taifa kwa kuwa ilizoeleka katika matukio mengi ya kitaifa amekuwa akiungana na marais wastaafu; Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete.

Aidha alisema Mkapa alikuwa na vipaji vya kiuongozi vya kulea na kukuza na kwamba hata yeye aliibuliwa na kiongozi huyo.

Pia alisema Mkapa ndiye aliyemwibua Kikwete baada ya kumteua kuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa miaka 10 na baadaye akawa mrithi wake.

“Yeye alimwibua Rais wa sasa wa Zanzibar, Dk. (Ali Mohamed) Shein baada ya kifo cha Makamu wa Rais, Hayati Omari Ally Juma na alimwibua Dk. Hussein Mwinyi kama mnavyofahamu hivi sasa ni mgombea urais Zanzibar, hii inadhihirisha Mzee Mkapa alikuwa na uono wa kuona viongozi.

“Mzee Mkapa alimwibua Dk. Hussein Ali Mwinyi ambaye kwa sasa ni mgombea urais Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyekuwa mwandishi wake wa hotuba Balozi Ombeni Sefue, baadaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi,” alisema Rais Magufuli.

Kiongozi huyo wa nchi aliwasili mkoani Mtwara jana jioni tayari kwa maziko yatakayofanyika leo katika Kijiji cha Lupaso wilayani Masasi. 

DANIEL OLE NJOOLAY 

Awali, aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daniel ole Njoolay alisema alipoteuliwa na Rais Mkapa alishtuka, lakini alimuuliza kwa nini amemteua.

Aidha alisema wakati wa uhai wake, Mkapa alipenda kuambiwa ukweli hata kama mchungu kwake.

“Aliponiteua kwenye nafasi ya ukuu wa mkoa nilishtuka sana, siku ile anaapisha nilimuuliza kwanini umeniteua wakati sijawahi kufanya kazi serikalini?” alisema Njoolay bila kueleza majibu aliyopewa na Mkapa.

Kuhusu aliyoyafanya akiwa kwenye nafasi hiyo katika uongozi wa Rais Mkapa, alisema alimshauri  kugawa Mkoa wa Arusha na Manyara na alisimamia ujenzi wa shule nyingi za sekondari jambo lililomfurahisha.

Alisema pia aliweza kuboresha mazingira kwa kupanda miti mingi mkoani humo na baadaye alihamishiwa Mkoa wa Mwanza ambao nao aliuboresha na kujenga shule za kata na Mkapa alipofika mkoani humo alishangaa idadi ya shule zilizojengwa kwa nguvu za wananchi.

Aidha Njoolay alisema aliboresha na kuipanua Hospitali ya Sekou Toure kwa nguvu za wananchi na Mkapa alifurahi na alizidi kumwamini.

Njoolay alisema Mkapa alipenda kuambiwa ukweli hata kama ni mchungu na kwamba aliweza kumshauri kutohitimisha kampeni eneo la Karatu kama ilivyokuwa imepangwa kutokana na kwamba CCM haijashinda na alikubali.

“Nilimwambia kule Karatu si vizuri kuhitimisha kampeni bado hatujashinda, lakini yeye (Mkapa) alihoji mbona kuanzia kule uwanja wa ndege wanasema lazima tushinde?” alisema Njoolay.

Aliongeza kuwa siku ya uchaguzi walianguka na siku ya sherehe Ikulu Mkapa aliwachekesha kuna waganga wa kienyeji wanaoweza kutabiri akirejea Karatu.

CHRISTOPHER OLE SENDEKA 

Naye aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher ole Sendeka alimzungumzia Mkapa kama kiongozi madhubuti na makini asiyeyumbishwa.

Alisema alitimiza wajibu wake ipasavyo na aliweza kuieleza dunia maamuzi ya nchi kupeleka jeshi Uganda kupigana na Idd Amin kutokana na kusikiliza vyema misimamo ya Baba wa Taifa, hayati Julius Nyerere.

Sendeka alisema Mkapa alikuwa na uwezo mkubwa kujieleza na kutokana na kumfahamu kwa karibu, alijua alikuwa na misimamo na alikiri alikabidhiwa nchi ikiwa salama na angeiacha salama.

Kuhusu uongozi wake kwenye CCM, alisema Mkapa aliamini katika misingi ya katiba na kanuni za chama, akiweka mbele masilahi ya nchi, kufuata utaratibu na kuamini wagombea wenye sifa.

Mara baada ya shughuli ya kuagwa kumalizika katika viwanja hivyo, mwili huo umesafirishwa kwenda kijijini Lupaso wilayani Masasi katika Mkoa wa Mtwara kwa maziko yatakayofanyika leo.

MWAKILISHI WA KENYA 

Katika hatua nyingine, ndege iliyokuwa imembeba mwakilishi wa Kenya, Samuel Poghisio aliyekuwa anakuja nchini kumuaga Mkapa ililazimika kurejea Kenya.

Akizungumza kwenye shuguhuli hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema hadi muda huo hawajapata taarifa kutokana na ndege hiyo kulazimika kurudi Kenya kabla ya kutua Tanzania kama ilivyokusudiwa.

SALAMU ZA RAIS WA BURUNDI

Kwenye shughuli hiyo, Waziri Mkuu wa Burundi, Jenerali Alain Guillaume alifikisha salamu za rambirambi za rais wa taifa hilo, Jenerali Evariste Ndayishimiye.

“Rais Ndayishimiye na Burundi yote wanawafariji Watanzania katika kipindi hiki kigumu, muhimu ni tueendelee kumwombea Hayati Mkapa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
195,588FollowersFollow
545,000SubscribersSubscribe

Latest Articles